Jumanne, 22 Machi 2016

Mungu na wakimbizi:


Ni muhimu kufahamu kuwa kuwahudumia wakimbizi ni mpango wa Mungu!, Leo tutachukua Muda wa kutosha kwa kina na upana na urefu kuangalia huduma muhimu kwaajili ya wakimbizi Duniani, Mwaka 2004 pekee karibia watu milioni tatu na nusu walikuwa ni wakimbizi barani Afrika pekee, ambao walikimbia na kuishi nje ya nchi zao, na wengine zaidi ya milioni kumi walikuwa ni wakimbizi ndani ya nchi zao, wengi walikuwa hawakimbii tumatukio ya majanga ya kiasili nlakini walikuwa wanakimbia matatizo ya kisiasa, ugomvi wa kimadaraka, matatizo ya kidini, ukabila na maswala mengineyo je neno la Mungu linasema nini kuhusu wakimbizi, kanisa limewahi kutafakari nini kuhusu wakimbizi? Tutajifunza somo hili kwa kuzingatia vipengele vitatu vifuatavyo:- 

 Kundi kubwa la wakimbizi wakiondoka Syria, wakimbizi nao ni watu


·         Neno la Mungu na wakimbizi
·         Mungu anawajali wakimbizi
·         Wakimbizi na mafundisho ya agano jipya

Neno la Mungu na wakimbizi:

Biblia inatambua kuweko kwa watu ambao wamewahi kukimbia huko na huko mbali na Nchi zao, kaini alikuwa mtu wa kwanza kufahamu madhara ya ukimbizi Mwanzo 4:12,”Utakapoilima ardhi haitakupa mazao yake, utakuwa mtoro na mtu asiye na kikao Duniani” Neno utakuwa mtoro ni sawa na utakuwa mkimbizi. Yakobo na Familia yake waliishimaisha ya ukimbizi kutokana na majanga ya njaa nchini kwao Mwanzo 47:3-4, “Farao akawauliza hao nduguze Kazi yenu ni nini? Wakamwambia Farao, Tumekuja kukaa ugenini katika nchi hii, kwa sababu wanyama wa watumwa wako hawana malisho, maana njaa ni nzito sana katika nchi ya kanaani, Basi twakusihi uturuhusu sisi watumwa wako tukae katika nchi ya gosheni” Yesu pia alikuwa mkimbizi huko Misri kwaajili ya kuokoa Maisha yake yaliyokuwa yakitafuta na mfalme Herode Mathayo 2:13-14. “Na hao walipokwisha kwenda zao tazama malaika wa Bwana alimtokea yusufu katika ndoto, akasema  Ondoka umchukue mtoto na mama yake , ukimbilie Misri, ukae huko hata nikuambie kwa maana Herode anataka amwangamize, Akaondoka akamchukua mtoto na mama yake usiku akaenda zake Misri” ziko sababu mbalimbali na mazingira ya aina mbalimbali yanayoweza kusababisha kila mmoja wetu kuwa mkimbizi kwa namna moja ama nyingine.

Mungu anawajali wakimbizi

Biblia iko wazi kuwa Mungu anawajali wakimbizi, alionyesha kujalia sana maisha ya Kaini hata pamoja na kuwa ukimbizi wake ulisababishwa na makosa yake mwenyewe Mwanzo 4:15. Mungu alimwambia Musa katika Torati kuandaa miji ya makimbilio kwaajili ya wakimbizi watakaokimbilia kutokana na sababu mbalimbali ama ambao watu wangelikuwa wanatafuta kuwaua, Kutoka  21:12-14, Hesabu 35:9-34, Kumbukumbu 4:41-43, 19:3-13, Nyakati 6:42-55. Mungu aliagiza pia kuwa wageni walioambatana na Israel pia wanahitaji kuheshimiwa kimsingi tunapaswa kuwajali aina zote za wakimbizi waliokimbia nchi zao kwa sababu zozote zile ziwe za kisiasa, vita uchumi njaa  na ugumu mwingine wote wanapaswa kuheshimiwa kuhifadhiwa kutunzwa vizuri, kupendwa na kuhifadhiwa,kwa heshima na usawa sawa na raia wengine tukiwahesabu kuwa ni ndugu na jamaa zetu Walawi 25, Isaya 16:1-4, Ezekiel 47:21-23 Lawi 19:33-34.

Wakimbizi na mafundisho ya agano jipya

Agano jipya linasisitiza sana kuwahudumia wageni kuwapenda na kuwajali wenye mateso na masikini Mathayo 25:31-40, tofauti ya ndugu na wakimbizi iliondolewa kabisa katika agano jipya Yohana 13:34 kutokana na umoja wa waamini Yohana 17:20-23 na kutokana na udugu na wote kuwa wanafunzi wa Yesu Kristo.
Hivyo ni muhimu kwa kanisa kujihusisha na kuwahudumia wakimbizi punde linapotokea swala la wakimbizi na kukutana na mahitaji yao ya muhimu haraka , kama usalama, upendo, chakula mavazi, malazi, maji safi,madawa, Kumbuka kuwa Yesu atakuja kubagua Kondoo na mbuzi kwa misingi ya namna tunavyowajudumia wengine au wenye uhitaji Mathayo 25:31-46, bila huduma hizi ni vigumu kwa wakimbizi kuikubali injili, wanyarwanda wana usemi usemao “Inda irimo ubusa ntigira amatwi” yaani tumbo tupu halina masikio, Ni muhimu kanisa likakumbuka hilo likakumbuka kuwahubiri injili lakini pia kusikiliza injili kutoka kwao ikiwa wanauwezo wa kuhudumu ili kuwalea na kukuza huduma zao punde warudipo au kuwa wamisionari katika taifa letu, hivi ndivyo nyakati za kanisa la kwanza walivyofanya pia Matendo 8;1-4, 18:1-2, Hali hii itainua heshima yao na kuwatia moyo, kanisa pia linapaswa kufanya kitu cha ziada sio tu kuwaletea maji katika birika bali kuwaelekeza namna wanavyoweza kuchimba visima wenyewe ili kujipatia maji, kanisa linapaswa pia kujihusisha katika swala zima la kuangalia chanzo cha ukimbizi na kukishughulikia hii ina maana kuwa kanisa linapaswa kujishughulisha na swala la kufanya upatanisho na kutafuta majibu ya matatizo ili kuyatatua na watu waweze kurejea katika nchi zao kwa amani badala ya kuiacha kazi hiiikafanywa na serikali zaidi, Kanisa ni lazima lisimamie demokrasia, Haki, upatanisho na mswala ya uongozi kwa ujumla, unaweza kufikiri kuwa kazi hii ni ya kiserikali zaidi nay a kijamii zaidi kuliko ya kiroho, lakini nataka nikuambie kuwa ni ya Kiroho zaidi na inapaswa kanisa kuwa sambamba na mashirika ya kiserikali na yasiyo ya kiserikali yanayojihusisha na huduma kwa wakimbizi

Ni muhimu kuwahudumia vema wakimbizi wao pia ni binadamu, kuna historia za kutisha kuwa sehemu nyingine wakimbizi wanabakwa, wanakataliwa, wanawekewa uzio, au wanafanyiwa hila wafe,n.k. hivi karibuni katika nchi ya Syria kutokana na vita kumekuwa na wakimbizi wengi wanaokimbilia ulaya na wengine wanapitia Libiya lakini wengi wamefanyiwa hila wakikimbia kuokoa maisha yao wengine wameuawa na mataifa mengine yameingia hofu ya kuwapokea Mungu isaidie Dunia kuwa mahali panapofaa kukaa ni wajibu wetu kupiga vita kila kinachosababisha watu kukimbia nchi zao na kujaribu kutatua migogoro iliyoko Duniani ili kila Nchi ipate Ustawi unaokusudiwa na Mungu.

Yeye aliye na sikio na alisikie neno hili ambalo Roho aliambia kanisa.

Hakuna maoni: