Jumatano, 2 Machi 2016

Thamani ya Neno la Mungu!



Neno la msingi; Zaburi 119; 72 “Sheria ya kinywa chako ni njema kuliko maelfu ya dhahabu na fedha.” Sheria inayotajwa hapo ni neno la Mungu mwandishi wa Zaburi hii analiona neno la Mungu kuwa ni jema kuliko maelfu ya dhahabu na fedha maana yake ni kuwa katika ujuzi wake na maarifa aligundua kuwa thamani ya neno la Mungu inazidi thamani ya fedha na dhahabu.

 Neno la Mungu lina thamani kuu kuliko dhahabu na fedha

§  Madhara ya kutokujua uthamani wa Neno la Mungu.
§  Uthamani wa Neno la Mungu.

Madhara ya kutokujua Uthamani wa Neno la Mungu.
Kwa kukosa maarifa watu wengi wameshindwa kufahamu uthamani wa neno la Mungu, Mwandishi wa zaburi 119;72 alifahamu thamani ya neno la Mungu kuliko wengi wetu ni kweli kuwa neno la Mungu lina thamanikubwa kuliko maelfu ya dhahabu na fedha, Watakatifu wengi waliotutangulia kwenda mbinguni walikuwa na ushuhuda kama huo kuhusu Neno la Mungu, walijua kuwa neno la Mungu lina tahamani kubwa kuliko vyote vilivyotamanika, iwe ni dhahabu, madini ya marijani au rubi ama fedha, vyote hivi havilingani na thamani ya mafundisho ya neno la Mungu au hekima itokanayo na ufahamu wa neno la Mungu Mithali 8;10-11,3;13-15, ni muhimu kumbuka kuwa mtu aliye tajiri akiitumia fedha kununua vyote anavyovitamani anapokufa huviacha duniani na haendi na chochote Zaburi 49;16-17. Kwa msingi huo ni muhimu kwa kila Mtu kuwa naufahamu wa neno la Mungu ambalo lenyewe ni la milele.

Uthamani wa Neno la Mungu.
Watu wengi ambao hawajui uthamani wa neno la Mungu hawatengi muda wa kuwa na saa chache za kulisikia na kulisoma neno la Mungu badala yake hutenga muda wote katika kujishughulisha na utafutaji wa fedha na kujihusisha na anasa za Dunia, Neno la Mungu likitiliwa maanani lina uwezo wa kutufikisha katika uzima wa milele na milele lakini endapo hauatalijali hata kama tunaweza kufanikiwa sana katika utajiri wa ulimwengu huu tunaweza kujikuta tunaingia katika Hasara na mateso ya milele na milele Mfano wa Lazaro na Tajiri Luka 16;19-24. Ni muhimu basi kila mtu aliyeokolewa akatoa kipaumbele kwa maswala ya kujitajirisha kwa Mungu Luka 12; 16-21. Kujitayarisha kwa Mungu ni kuwa katika hali ya kuwa na Muda wa kujifunza Mapenzi yake na kuyatendea kazi, juhudi ambazo tunaweza kuzielekeza katika kujitafutia mali zinaweza pia kuelekezwa kwa kiwango Fulani katika kujitafutia hekima ya neno la Mungu ambalo nalo tunapaswa kulitafuta  kama fedha au hazina iliyositirika Mithali 2;2-5 kwa msingi huo ni muhimu sana kwetu kuhakikisha kuwa tunawekeza katika kujitafutia kumjua Mungu kupitia neno lake  na hata kutumia mapato yetu katika kujipatia ufahamu wa neno la Mungu Mithali 4;4,7, kukubali kugharimika kufika katika siku za mafundisho hata kama yanapatikana mbali na pale tulipo Mathayo 12;42 Kristo alipendezwa na Malikia wa sheba aliyetoka mbali kwaajili ya kusikiliza hekima ya Sulemani atafurahishwa nasi endapo tutatafuta hekima yake kwa gharama Yoyote, wakati mwingine tunaweza kupata vikwazo kadhaa kwaajili ya kuitafuta kweli, unaweza kupigwa na Mumeo kwa sababu tu ya kuja kuyasikiliza maneno ya Mungu au wazazi wakakupinga katika hatua za mwanzoni upinzani huo ni jambo la kawaida hatimaye  Mungu ataupa hekima na namna ya kushinda, lazima tukumbuke kuhangaika kwaajili ya nafsi zetu kwani hatimaye siku ya mwisho kila mtu atatoa hesabu yake mwenyewe, hatutakuwa na udhuru kuwa nani alikuzuia usiyasikiemaneno ya Mungu ambayo tumejifunza kuwa ni ya thamani kulio fedha Warumi 14;12. Bwana ampe neema kila mmoja wetu kuyapenda, kuyatafuta na kuyatendea kazi maneno yake na kutenga Muda wetu wa kuhudhuria Ibada Bila udhuru wa aina iwayoyote ili tupate kibali kwake. Ukiyajua hayo Heri wewe ukiyatenda Yohana 13;17.

Hakuna maoni: