Ni muhimu kufahamu kuwa
Mafundisho kuhusu Ubatizo katika nyakati hizi tulizonazo yamechakachuliwa sana, na hivyo kuliweka kanisa katika wakati mgumu
wa kuamua watu wabatizwe vipi kutokana na kila mtu kubatiza katika namna anayoiona
kuwa iko sahii na kujenga hoja za kibinadamu hata kuliko kuliangalia Neno la
Mungu linasema nini kuhusu Ubatizo, Mungu na ampe neema kila mmoja wetu na moyo
uliopondeka ili wote kwa pamoja tuache tofauti zetu na kuliangalia neno la
Mungu linasema nini kuhusu Ubatizo, tuchukulie kana kwamba tumeokota Biblia na
sisi wote hatujui Neno la Mungu na tunaisoma hiyo Biblia na tunagundua kuwa
tunaweza kumuamini Mungu na tukabatizwa je unafikiri tungebatizwa vipi? Hii ndio aina ya ubatizo ninayotaka kuizungumzia
sawa na Neno la Mungu linavyojieleza na sio sawa na tamaduni za watu na
historia za kipagani.
watu wengi sana hubatizwa pale alipobatiziwa Yesu mto Jordan (Jordan river) huko Israel.
Kwa msingi huo leo tutachukua
Muda pamoja na mkuu wa wajenzi mwenye hekima kuchambua kwa kina somo kuhusu
ubatizo kwa upana na urefu, ili tuweze kufahamu kwa undani kuhusu ubatizo na
kuondoa utata ulioko miongoni mwa jamii ya Kikristo.
Yesu aliamuru kwamba wote watakaomuamini
na kubatizwa wataokoka, Biblia inasema katika Mathayo 28:18-20 “18. Yesu akaja kwao,
akasema nao, akawaambia, Nimepewa mamlaka yote mbinguni na duniani. 19. Basi,
enendeni, mkawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi, mkiwabatiza kwa jina la Baba,
na Mwana, na Roho Mtakatifu; 20. na
kuwafundisha kuyashika yote niliyowaamuru ninyi; na tazama, mimi nipo pamoja
nanyi siku zote, hata ukamilifu wa dahari.” Unaweza pia kuona katika Marko
16:15-16 “Akawaambia, Enendeni ulimwenguni mwote
mkaihubiri injili kwa kila kiumbe, aaminiye na kubatizwa ataokoka asiyeamini
atahukumiwa”
Ni muhimu kwetu basi tukachukua
muda kuchambua agizo hili la Yesu la kubatiza na kuangalia kwa undani kile
tuilichoagizwa ili kukifanyia kazi kama Mungu alivyoagiza. Tutajifunza somo
hili Mafundisho kuhusu Ubatizo kwa kuzingatia Vipengele vitano vifuatavyo:-
- · Maana ya Neno Ubatizo
- · Maana na Historia ya Ubatizo
- · Kanuni na jinsi ya kubatiza
- · Sifa ya mtu anayestahili kubatizwa
- · Namna ya kubatiza.
Maana ya Neno Ubatizo:-
Kwa kuwa tunazungumzia ubatizo ni
vema kwanza tukaelewa asili ya neno Ubatizo
neno Ubatizo tulilo nalo kwa Kiswahili katika kiingereza wanatumia neno “Baptize” au “Baptisms” ambalo kwa asili limetokana na Neno la kiyunani yaani
KIGIRIKI “Baptizo” Batizo, ambalo maana yake ni Kuzamisha au
kudumbukiza, “to dip or sink” or “immerse” pia ubatizo unaweza
kufananishwa na kuchovya kama mtu anavyoweza kudumbukiza tonge la ugali katika
mchuzi, nyakati za Biblia pia lilitumika kumaanisha kuchovya na kufyonza kabisa
asili ya kitu kwa mfano nguo ya kitani ilipowekwa katika rangi ili kuibadili
iwe na rangi ingine ilidumbukizwa katika rangi na nguo hiyo ilitoka ikiwa
imebadilika kutoka weupe wake wa asili kuingia katika rangi iliyodumbukizwa
kwayo tendo hilo pia liliitwa Ubatizo unaweza kuona, hii ndio maana halisi ya
ubatizo hata kwa mujibu wa “Strong
concordance” na “NAS Exhaustive
Concordance” na vyanzo vingine vya
Lugha za kiyunani.
Maana na Historia ya Ubatizo:
Kama tulivyoweza kuona maana ya
Ubatizo hapo juu ni wazi kuwa hii ndio maana halisi ya ubatizo na maana hii
imathibitishwa na hata kukubaliwa kuwa ndio maana halisi ya ubatizo kwa mujibu
wa wataalamu na wasomi wa Lugha ya kigiriki yaani kiyunani, na wanahistoria
waliobobea katika maswala ya kanisa, ingawa ni muhimu pia kufahamu kuwa
wayahudi walioishi nyakati za Kanisa la kwanza walibatiza pia kwenye maji mengi
au kwa kuzamisha kwa kusudi la kuwabadilisha wale waliokuwa mataifa wa kawaida
walioamini katika dini ya kiyahudi ambao waliitwa “Proselyte’s” ubatizo wao ulikuwa na maana ya kuwa wameacha miungu
yao na kumuamini Mungu wa wayahudi, kitamaduni inaelezwa kuwa mwongofu
alisimama katika maji na kisha kuzamisha kichwa chake katika maji huku sheria
au Torati ya Musa ikisomwa, na tendo hilo pia lilimuhesabu kuwa ametakaswa
na na ameanza kuishi maisha mapya kama mtu wa watu wa agano la Mungu.
Katika tamaduni za kiyunani pia
kulikuwako na biashara zilizoshamiri za uuzaji wa nguo za rangi ya zambarau
soma Matendo 16:11-14 nguo hizi
zilikuwa mfano wa batiki zilizamishwa katika sufuria za maji yenye rangi na
hivyo nguo hizo zlifyonza maji na rangi kabisa na kusababisha rangi kupenya
katika nguo na nguo ilitoka ikiwa na rangi iliyokusudiwa kitendo hiki pia
kiliitwa UBATIZO.
Ni wazi kutokana na maana na
historia na tamaduni, swala la kunyunyizia maji au kumwagia maji binadamu kwa
madai kuwa unabatiza haliko katika historia nzima ya kubatiza, lakini liko
katika tamaduni za kitorati za kutakasa kitu au vitu, pia kibiblia swala hilo
halimaanishi ubatizo, Kibiblia kuhani alitakasa vitu au vyombo vilivyotumika
kwa kazi maalumu hekaluni, lakini linapokuja swala zima la Ubatizo kubatiza kwa
kunyunyizia hakuna mashiko ya kihistoria wala ya kimaandiko, kuna uwezekano tu
kuwa aina hii ya ubatizo ilifanywa kwa wagonjwa mahututi ama ambao walikuwa
hawawezi kuelekea eneo la Ubatizo na pia ama kwa kuheshimu watu wenye nyadhifa
kubwa kama wafalme, au pia kwa sa babu ya kubatiza wakristo waliokimbilia
mafichoni wakati wa mateso, hata hivyo kwa sababu zozote zile kama
zilizoainishwa hapo juu, haziwezi kuhalalisha ubatizo huo kuwa wa kibiblia ama
wa kihistoria, na kwa vyovyote vile ubatizo huo sio agizo la kibiblia na uko
uwezekano kuwa uliingizwa kwa mitazamo ya kipagani au kwa kuweko na mwingiliano
wa kipagani.
Iko wazi kuwa ubatizo wa kimaandiko kabisa ambao hata wapagani yaani
watu wasio na dini wakiokota biblia leo wakajifunza neno na kubatizana basi ni
wazi ubatizo halisi utahitaji maji mengi na ya kuzamisha, ambayo ndio maana
halisi ya kibiblia kwa mujibu wa Maandiko Warumi
6:1-4.
Ubatizo unafanana na tendo la kuzika mwanadamu Warumi 6:1-4
Ubatizo ni picha ya wokovu
Ubatizo ni kivuli cha kufanana na Bwana Yesu kiroho
Ubatizo ni alama ya kuoshwa ni alama ya kile ambacho kimekwisha
kufanyika ndani ya moyo Matendo 22:16
Ubatizo ni ushuhuda Wagalatia
3:27
Umuhimu wa ubatizo, kanisa halipaswi kupuuzia swala zima kuhusu
ubatizo, hata ingawa ubatizo wenyewe hauokoi, wala hauna nguvu ya kuokoa, watu
hawabatizwi ili waokoke, lakini wanabatizwa kwa sababu wameokoka, kwa hiyo
ubatizo sio tiketi ya wokovu lakini ni tendo muhimu katika kumkiri Yesu
hadharani na ni muhimu katika kuonyesha utii, kama vile Rais anapoteuliwa anathibitika
kuwa Rais kamili pale anapoapishwa, tunapokuwa tumemuamini Yesu kuwa ni bwana
na mwokozi wetu, kokote pale tunamkiri Yesu kuwa ni bwana na Mwokozi hadharani
kwa kukubali kubatizwa.
Kanuni na Jinsi ya kubatiza
Ni muhimu kufahamu kuwa kanini
kuu ya kubatiza ni kile kilichoagizwa na Bwana Yesu tu Mathayo 28:19 Kubatiza kwa jina lka Baba na la mwana na la Roho
Mtakatifu. Haya ndio Maneno yanayopaswa kutamkiwa mtu anayebatizwa sawa na Yesu
alivyoagiza, mtu anapomwamini Yesu anakiri hadaharani kwa njia ya ubatizo na
mbatizaji atatamka maneno haya Kwa kuwa Fulani…….bin Fulani…..umemwamini Bwana
Yesu Kristo kuwa alikufa msalabani kwaajili ya ondoleo la dhambi na kuwa
amekuwa bwana na mwokozi wa maisha yako kwa mamlaka niliyopewa na Mungu mimi
nakubatiza kwa jina la baba na la Mwana na la Roho Mtakatifu amen!, Maneno
wakabatizwa kwa jina lake Yesu Kristo yaliyotumiwa na petro katika Matendo 2:28, hayawakilishi kanuni ya
kubatizia, bali yanazungumzia Mamlaka ya ubatizo mara baada ya mtu kumuamini
Yesu Kristo, kwa Mfano “Didache”
yaani maandiko ya nyakati za zamani wakati wa mitume yaliyoandikwa mika 100
baada ya Kristo (100 AD) yanataja Ubatizo ulioagizwa na Yesu kama Ubatizo wake
Yesu Kristo lakini katika ufafanuzi wake jinsi walivyobatiza walitumia kanuni
ya kubatiza kwa Jina la Baba na la Mwana na la Roho Mtakataifu, Hivyo kanuni
iliyotumika kubatiza ilizingatia utatu wa Mungu. Paulo anapozungumzia ubatizo
wa wana wa Israel katika bahari ya shamu anataja Ubatizo wake Musa hii
haimaanishi Paulo alikuwa anataja juu ya Kanuni bali mamlaka ya Musa kwa vile
kila mmoja baada ya kuvuka bahari ya shamu alikubali wazi kuwa Musa ni mjumbe
wa Mungu wa Mbinguni kwaajili yao, “1Koritho
10:2” ni katika mtazamo huohuo unapozungumzia ubatizo wa Yesu Kristo
unazungumzia sio kubatizwa kwa jina lake Yesu tu, bali kubatizwa kwa Mamlaka au
agizo lake Yesu Kristo baada ya kumkubali na kumuamini kama kiongozi wetu mkuu
wa wokovu wetu, kubatizwa kwa jina lake Yetu kungemaanisha vilevile kama
alivyoagiza, kubatizwa kwa Jina la Baba , Mwana na Roho Mtakatifu, hivyo si
sahii katika kanuni ya ubatizo kutaja jina la Yehova tu au jina la Yesu tu,
kanuni ya ubatizo inabaki kubatizwa kwa jina la Baba, mwana na Roho, Mtakatifu.
Uatatu wa Mungu ulikuwa ni jambo
muhimu sana kutajwa katika nyakati za mitume kwaajili ya kuwakilisha
upatikanaji wa neema na ushirika na upendo 2Wakoritho
13:14. Aidha tendo la ubatizo nyakati za Biblia na kama ilivyo maana halisi
kibiblia ilikuwa ni lazima lihusishe maji mengi
“Yohana 3:22-23”
Ubatizo kwa kuwa ulifanyika
katika maji mengi ulihusisha kupandana kushuka kutoka majini, wakati wote
Biblia ilipotaja swala la ubatizo au mtu kubatizwa lugha za kushuka na kupanda
kutoka kwenye maji zilitawala kama unavyoweza kuona katika mazingira
yafuatayo:-
-
Marko
1:9-11
-
Mathayo
3:16
-
Matendo
8: 36-39
-
Matendo
16:13-15
-
Matendo
16:30-34
Sifa ya mtu anayestahili kubatizwa:
Watu wenye sifa ya kubatizwa ni
wale ambao kwa moyo wa dhati wametubu dhambi zao kwa kumaanisha kuziacha na
wanaishi maisha ya utakatifu sawa na injili ya Bwana Yesu Kristo, ni watu
waliomwamini Yesu na wameisikia injili na kuiamini, hao wana sifa ya kubatizwa,
Nyakati za kanisa la Kwanza swala la ubatizo liliambatana na maswala makuu
matatu yafuatayo;-
1. Kumwamini
Yesu kwa moyo wako wote kuwa ndiye Mwana wa Mungu Matendo 8:36-39
2. Kuliitia
jina la Bwana yaani kuomba Matendo 22:16
3. Kujiweka
wakfu kutoka matendo maovu na kuishi kwaajli ya Mungu 1Petro 3:20-21
Kwa msingi huo mtu mwenye sifa ya
kubatizwa anapaswa kuwa na sifa za kuweza kuisikia injili, kusikiliza mahubiri,
na kisha kuyaamini na ndipo inapowezekana mtu huyo kubatizwa Marko 16:15-16 “Akawaambia Enendeni ulimwenguni mwote
mkaihubiri injili kwa kila kiumbe, aaminiye na kubatizwa ataokoka asiyeamini
atahukumiwa” Mtu aliye na sifa za kubatizwa ni lazima awe na uwezo wa
kusikia injili na kuipambanua na kuikubali yaani kuiamini na kutubu dhambi zake
yeye mwenyewe, ni lazima ahubiriwe, ni lazima aamini ni lazima akiri ni lazima
aliitie jina la Bwana, ni lazima asikie kutoka kwa muhubiri Warumi 10:10-17 “10. Kwa maana kwa
moyo mtu huamini hata kupata haki, na kwa kinywa hukiri hata kupata wokovu. 11.
Kwa maana andiko lanena, Kila amwaminiye hatatahayarika. 12. Kwa maana hakuna
tofauti ya Myahudi na Myunani; maana yeye yule ni Bwana wa wote, mwenye utajiri
kwa wote wamwitao; 13. kwa kuwa, Kila atakayeliitia Jina la Bwana ataokoka. 14.
Basi wamwiteje yeye wasiyemwamini? Tena wamwaminije yeye wasiyemsikia? Tena
wamsikieje pasipo mhubiri? 15. Tena wahubirije, wasipopelekwa? Kama
ilivyoandikwa, Ni mizuri kama nini miguu yao wahubirio habari ya mema! 16.
Lakini si wote walioitii ile habari njema. Kwa maana Isaya asema, Bwana, ni
nani aliyeziamini habari zetu? 17. Basi imani, chanzo chake ni kusikia; na
kusikia huja kwa neno la Kristo.” Utaweza kuona sifa za namna hiyo
zikijirudia kwa mkazo katika maandiko unaweza kusoma Matendo 8:36-39, Matendo.2:38-41, Matendo 16:14-15, Matendo 16:29-34.
Kwa Msingi huo basi watu wenye sifa ya kubatizwa ni wale wenye uwezo wa
kupambanua injili moyoni wenye uwezo wa kujua mema na mabaya. Kwa kuwa watoto
wadogo hawana dhambi na hawana ujuzi au wezo wa kupambanua jema au baya na
hawana uwezo wa kuamua kuamini au kutokuamini ni wazi tu kuwa ubatizo wa maji
mengi hauwahusu kwa ufupi watoto
hawabatizwi, hii haimaanishi kuwa tunawazuia kuja kwa Kristo au kuingia katika
ufalme wa Mungu hapana Yesu alisema watoto kama hawa ufalme wa Mungu ni wao,
kwa msingi huo wanayo tiketi ya kuingia katika ufalme wa Mungu Mathayo 19:13-14 watoto wadogo huwekwa
wakfu kwa Mungu katika ibada lakini hawabatizwi wao hubarikiwa tu.Luka 18:15-16.
Namna ya kubatiza.
Yeye anayebatiza na wanaobatizwa
watafika nga’mbo ya maji yenye uhai yaani yaliyo safi na yanayotembea na kama
ni kisima kiwe kina uwezo wa kuruhusu maji kuingia mapya na yaliyotumika
kutoka, wataimba kama sehemu ya ibada na baada ya nyimbo maandiko kadhaa au
mojawapo yanayohusiana na ubatizo yatasomwa na kisha Maji yatabarikiwa na eneo
la kubatizia litawekwa wakfu, mbatizazi ataingia katika maji mengi na
kuhakikisha kuwa anasimama vema mahali ambapo ataweza kuwazamisha wanaobatizwa,
wabatizwaji wanaweza kuwa na mavazi maalumu ya kubatiziwa au kuwa na nguo za
kubadilisha mara baada ya kubatizwa, aidha ni vema wakaweko wahudumu wenye nguo
maalumu ambao watawahifadhi wanaobatizwa mara baada ya kupanda kutoka majini
kuwazinga kwa nguo hizo na kuwasindikiza mahali pa kubadilisha nguo kavu,
mbatizaji atakapokwisha kuyatakasa maji kwa kuyaweka wakfu, wanaobatizwa
watajipanga mstari na kuanza kubatizwa kwa zamu ni vema wahudumu wakawa karibu
kabisa na anayebatiza kwaajili ya kutoa msaada wa huduma zinazojitokeza wakati
wa ubatizaji kama woga wa maji, kujazwa Roho Mtakatifu wakati wa kubatizwa na
kuondoka kwa Pepo wabaya wakati wa kubatizwa haya ni matendo ya kawaida ambayo
hujitokeza wakati watu wanabatizwa.
Wanaobatizwa waelekezwe namna ya
kujihami wasinywe maji au maji kuwaingia puani, waelekezwe namna ya kuwa wepesi
na kutokusababisha kuangukia majini tendo la ubatizaji lifanyike kwa utaratibu
bila papara.
Mbatizaji atauliza majina kamili
ya anayebatizwa nakama kuna jina jipya analotaka kulituimia kubatizwa kama
alitokea katika uislamu na imani nyinginezo
Mbatizaji atamuuliza anayebatizwa
kama amemkubali Yesu kuwa Bwana na mwokozi na kama anaamini kazi aliyoifanya
Yesu Msalamabani ikiwa ndivyo mbatizaji atatamka yafuatayo
Kwa kuwa …………………..Umemkubali Yesu
Kristo kuwa Bwana na mwokozi wa maisha yako na kuiamini kazi aliyoifanya
Msalabani kwaajili yetu
Mimi kwa mamlaka niliyopewa
nakubatiza kwa jina la Baba na la Mwana na la Roho Mtakatifu na kisha
atamzamisha kwenye maji, mfano wa mtu anayezikwa ardhini na kisha atamtoa
katika maji, wakati huu kila sehemu ya mwili wa anayebatizwa itapaswa kuzama
kabisa katika maji mfano wa marehemu anavyolazwa, baada ya kitendo hicho
utamuinua kwa haraka na kusimama katika hali ya kawaida na kisha utamuombea
neema kwa maisha yake na kumbariki katika sehemu ya maisha yake ya wokovu na kumuacha aende zake.
Maoni 2 :
Shalom, ningependa kuuliza, kwangu nini ni lazima ubatizo ufanyike kwenye maji yanayotembea? Nini umuhimu wa maji yanayotembea? Na kama mtu amebatizwa kwenye kisima pasipo maji kutembea, je, ubatizo huo si sahihi? Na kama si sahihi, je anahesabiwa kama hajabatizwa? Natamani nielewe zaidi kuhusu ulazima au maana ya maji yanayotembea, msaada tafadhali, shukrani in advance.
Naombeni kujua kwa ndani kuhusu ubatizo maana trh 27 na mimi naenda kubatizwa
Chapisha Maoni