Jumanne, 26 Januari 2016

MUNGU ANAWEZA! YESU ANAWEZA! (GOD IS ABLE!)


Ni usemi ambao tunapenda sana kuutumia sisi wakristo katika kutiana moyo kuwa Mungu anaweza!
Ndio tunajua kuwa Mungu anaweza kufanya mambo yote kwa vile tangu utoto tumeambiwa Yasiyowezekana kwa wanadamu kwa Mungu yote yawezekana! Hata wahubiri wa injili wengi wanakazia hilo katika mikutano ya injili bila shaka ni ili kuchochea na kupandisha imani za wasilizaji wao
Swali moja la msingi linasalia litakalotusaidia kutafakari kwa kina usemi huu Mungu anaweza? Sawa anaweza nini
Hili linahitaji majibu, nikifahamu au ukifahamu na tukifahamu kuwa Mungu anaweza nini bila shaka kila mtu akinisalimu au akikusalimu au tukisalimiana Mungu anaweza tutakuwa na ujuzi wa kutosha anaweza kufanya nini? Bilia inaeleza kuwa Mungu anaweza kufanya mambo yote, lakini pia imetaja mambo mengi ambayo Mungu anaweza ni yepi?
1.       Anaweza kuokoa
Waebrania 7:25 Biblia inasomeka hivi Naye,  “kwa sababu hii, aweza kuwaokoa kabisa wao wamjiao Mungu kwa yeye; maana yu hai sikuzote ili awaombee”. Biblia inasema Mungu yaani Yesu anaweza kuwaokoa kabisa wamjiao, kuokoa kunakotajwa hapa, ni kifurushi chenya mahitaji mengi ya kibinadam yoote kwa ujumla ukimuendea Mungu anaweza kukupatia ufumbuzi kwa vile anatuombea Unaona!

2.       Anaweza kutulinda tusijikwae
Yuda 1:24 Biblia inasema hivi “Yeye awezaye kuwalinda ninyi msijikwae na kuwasimamisha mbele ya utukufu wake bila mawaa katika furaha kuu” Yuda hapa alikuwa akizuingumzia na kuwakemea walimu wa uongo wa neno la Mungu, ambao wangewakwaza wengi kwa mafundisho yao na kuwapotosha na kuwaangusha, lakini pamoja na kuweko kwa mafundisho na imani potofu nyingi katika nyakati za leo biblia inatuthibitishia kuwa uko uwezo wa Mungu wa kutulinda na mafundisho potofu na roho zidanganyazo, kama haitoshi pia Yesu ana uwezo wa kutulinda tusianguke mpaka tutakaposimama katika utukufu wake Mbinguni bila lawama  wala mawaa katika furaha kuuu

3.       Anaweza kuwasaidia wanaojaribiwa!
Waebrania 2:18 Biblia inasema hivi “Na kwa kuwa mwenyewe aliteswa alipojaribiwa, aweza kuwasaidia wao wanaojaribiwa.” Unaona msomaji wangu mpezni usiogope! Hakuna jaribu ambalo ni geni kwa Yesu hususani katika swala la mateso, Yesu anajua kipimo cha mateso yako anajua kuwa yanaweza kukufikisha mahali unaweza hata ukamkosea, habari njema ni kuwa anaweza kuwasaidia wanaojaribiwa je umawahi kuhitaji msaada wake akashindwa? Liitie jina lake omba bila kukoma mtegemee tu atakusaidia anaweza kufanya hivyo.

4.       Aweza kuvitiisha vitu vyote chini yake !
Wafilipi 3:20-21 Biblia inatuambia hivi “ Kwa maana sisi, wenyeji wetu uko mbinguni; kutoka huko tena tunamtazamia Mwokozi, Bwana Yesu Kristo;  atakayeubadili mwili wetu wa unyonge, upate kufanana na mwili wake wa utukufu, kwa uweza ule ambao kwa huo aweza hata kuvitiisha vitu vyote viwe chini yake. Ndugu yangu Yesu anauwezo wa kutiiisha kila kitu chini yake nini kimeinuka katika maisha yako? Nini kinakunyima furaha na kukusababishia huzuni? Je unadhani kitaendelea? Hapana Hakitaendelea mtegemee Mungu anaweza kukitiisha kila kilichoinuka chini ya miguu yake

5.       Anauwezo wa kutupa Neema!
2Wakoritho 9:8 Biblia inasema hivi “Na Mungu aweza kuwajaza kila neema kwa wingi, ili ninyi, mkiwa na riziki za kila namna siku zote, mpate kuzidi sana katika kila tendo jema; Unaona mtume hapa Mkuu wa wajenzi mwenzangu anazungumza neema katika mazingira ya utoaji, kama utakuwa na tabia ya utoaji kama biblia inavyoelekeza kwa ukarimu na sio kwa kutafuta sifa hutapungukiwa Mungu atakupa neema na kukujaza kwa wingi, utakuwa na riziki za kila namna na nutabarikiwa zaidi katika kila tendo jema yaani la utoaji

6.       Anaweza kumsimamisha mtu au mtumishi aliyeanguka
Warumi 14: 4 Biblia inasema haya “Wewe u nani unayemhukumu mtumishi wa mwingine? Kwa bwana wake mwenyewe yeye husimama au huanguka. Naam, atasimamishwa, kwa kuwa Bwana aweza kumsimamisha.” Msomaji wangu unaweza kujionea! Wako watu ambao wanamafundisho potofu kuhusu wema na rehema za Mungu wanafundisha kuwa mtu aliyeanguka hawezi kusimama tena, ni mafundisho ya kijinga ni imani ya kipuuzi, lipi lililo jepesi kumwambia aliyelala amka au aliyekufa fufuka? Ikiwa Mungu anaweza kuwafufua wafu kutoka dhambini anashindwaje kumwamsha mwanaye aliyeanguka! Biblia inasema Usihukumu ni Mungu anayeruhusu kwa utukufu wake na anauwezo wa kuhuisha tena, sitii moyo tabia na mwenendo wa kufanya dhambi mara kwa mara kwa kisingizio kuwa Mungu anasimamisha tena, lakini nakataa kama mkuu wa wajenzi mwenye hekima wale wanaosema mtu akianguka hawezi kusimama tena Munu anaweza, anaweza kumsimamisha mtumishi wake aliyeanguka na kamtumia tena kwa viwango vya juu zaidi bila kiburi

7.       Anauwezo wa kufanya zaidi ya yale tuyaombayo na tuyawazayo
Waefeso 3:20 “Basi atukuzwe yeye awezaye kufanya mambo ya ajabu mno kuliko yote tuyaombayo au tuyawazayo, kwa kadiri ya nguvu itendayo kazi ndani yetu; Umeona nataka kukamilisha ujumbe huu kwa Pointi hii ya saba kwa vile namba hii kinabii ni utimilifu wa mambo yote ziko sababu nyingi ambazo Mungu anaweza lakini hii inajumuisha yote, kumbe anaweza kufanya mambo ya ajabu mno kuliko yote tuyaombayo na tuyawazayo hii imanimaliza siwezi kuendelea bila shaka msomaji wangu umepata ufunuo mkuu sana hata nisipokuombea leo, anaweza kufanya mambo ya ajabu mno kuliko yote tuyaombayo na tuyawazayo imani yangu ni kuwa tangu sasa mtu akikusalimu Mungu anaweza utakuwa na ujuzi anaweza nini
Ubarikiwe na Bwana siku njema

Mkuu wa wajenzi Mwenye Hekima
Rev. Innocent Kamote.

Hakuna maoni: