SEHEMU YA 1:
KITABU CHA DANIELI.
SOMO
LA 1: KUPITIA YA KITABU CHA DANIELI:
A; D A N I E L I:
Lengo la 1; - Eleza Historia fupi ya Danieli.
Danieli – jina lake lina maana “Mungu
ndiye Hakimu wangu”. Alikuwa
mmojawapo wa mateka waliochukuliwa na mfalme Nebukadneza katika mwaka 605 KK.
Kutoka Yerusalemu na kupelekwa Babeli.
Aliishi kipindi chote cha utumwa cha miaka 70 huku akiwa nabii na
mwandishi wa Kitabu cha Danieli.
Tunamfahamu Danieli jinsi alivyokuwa mcha Mungu, tukisoma Eze.14:14-20. Inavyoonekana alitokea na ukoo wa daraja la
juu huko Yerusalemu. Danieli hakuwahi
kuoa, inawezekana alifanywa towashi kwa sababu alifanya Kazi katika Kasri la mfalme.
B. KITABU CHA DANIELI:
Lengo la 2 : Taja tarehe na makusudi ya kuandikwa kitabu
hiki.
Kitabu hiki kiliandikwa kati
ya mwaka 536 – 530 KK. Kikiwa na makusudi mawili.
1.
Kuwatia moyo mabaki huko Babeli kuwa utumwa ulikuwa
sio mwisho wa taifa lao.
2.
Kuwaonyesha watu wa Mungu kuwa Mungu ndiye mtawala
wa mataifa yote.
-Yesu amekithibitisha kitabu kuwa kiliandikwa na Danieli.
Lengo la 3: Eleza mgawanyo wa Kitabu hiki:
Kitabu
hiki kimegawanyika katika sehemu kuu tatu:
1.
Historia fupi ya Danieli toka Yerusalemu hadi
Babeli –(Dan. 1:1-21)
2.
Ujumbe wa Danieli kuhusu utawala wa Mungu juu ya
mataifa yote (2:1)
3.
Maono ya Danieli (8:1 -
12:13)
Sura ya kwanza iliandikwa kwa lugha ya Kiebrania wakati sura zingine
zimeandikwa kwa lugha ya Kiaramu.
Lengo la 4: Eleza mambo maalum ya kipekee yaliyomo katika
Kitabu cha Danieli
Kitabu cha Danieli kina mambo
ya kipekee nane. Nayo ni:-
- Kitabu kifupi kuliko vitabu vya Manabii wote ambacho watu wanasoma na kujifunza mno.
- Unabii wa Danieli umenukuliwa sana katika A/Jipya.
- Ni kitabu cha Apokilasi cha A/Kale kinachoelezea mambo ya siku za mwisho.
- Ni kitabu pekee kinachoelezea ujio wa kwanza wa Masihi katika Dan. 9:24-27
- Kinaelezea zaidi maisha ya Mwandishi, Tabia, Hekima na Maombi yake.
- Kina maombezi ambayo ni mfano wa maombezi ya kuwasamehe watu wa taifa lake kwa kumkumbusha Mungu ahadi zake.
- Habari za Danieli na rafiki zake zinapendwa mno.
- Maandishi yaluiyoandikwa na kutangaza yamekuwa methali inayotumiwa sana leo.
Lengo la 5: elezea Dola na mji wa Babeli na makusudi ya huduma ya
Danieli.
Mji wa Babeli ulijengwa
Kusini kando ya mto Efrata. Hali ya hewa
na maumbile ya asili yalifanya mji wa Babeli uwe na watu wengi. Mfalme Nebopolasa alikuwa ndiye mwanzilishi
wa Dola ya Babeli na kukuzwa sana na mtoto wake aitwaye Nebukadneza.
Dola ya Babeli
ilipokuwa na nguvu ikaiangusha Ashuru na kuteka Palestina na Misri. Kutokana na 2Nyak. 36:15-17, Yuda
ilichukuliwa uhamishoni kwa sababu waliacha sheria ya Bwana. Mungu akawahukumu watu wake kwa kuwaweka
katika utumwa mikononi mwa Wakaladayo.
Danieli aliinuliwa kuwa Nabii ili awatie moyo mabaki waliokata tamaa kuwa
Mungu ndiye anamiliki na kuiongoza historia.
MASWALI:
- Kitabu cha Danieli kiliandikwa mwaka gani?
- Makusudi ya kuandikwa kwa kitabu hiki ni:
(a) _____________________________________
(b) _____________________________________
- Kitabu hiki kimegawanywa katika sehemu ngapi?. Zitaje.
- Taja mambo manne ambayo ni ya kipekee katika Kitabu hiki.
- Dola ya Babeli ilikua zaidi katika kipindi cha mfalme _______________
SOMO LA 2: UCHAMBUZI WA KITABU CHA DANIELI.
PAMBANO LA
KWANZA MAPAMBANO DHIDI YA MASWALA YA
IMANI (11-21)
Lengo la 1: Eleza pambano la
kwanza la Imani la Danieli na rafiki zake.
Je, walishindanaje?, nini matokeo ya
kushinda kwao?
Baada ya Danieli kufika Babeli, mfalme Nebukadneza aliamua Danieli na
wenzake wapate elimu ya Ukaldayo
kuhusiana na lugha na mila za Babeli. Hii itawafanya watumike vizuri. Ili kutimiza kusudi hili, mfalme Nebukadneza
alifanya mambo yafuatayo:-
Kwanza: Aliwapa
uraia wa Babeli kwa kubadili majina yao kama ifuatavyo:
Kiebrania:
- Danieli (Mungu ni Hakimu wangu – Belteshazzar (Mwana wa Bel)
- Hanania (Mungu ni mwenye Neema) –Shadrack (Uvuvio wa Rachi)
- Mishaeli (Nani kama Mungu) – Meshaki (nani kama Shaki)
- Azaria (Mungu anasaidia) – Abdinego (mtumishi wa Nebo)
Pili: Aliamua
kuwapa vyakula ambavyo vilitolewa kwa miungu, ili wawe na afya nzuri. Katika hili, Danieli na wenzake waliamua
kutojitia unajisi kwa kula vyakula vilivyotolewa kwa miungu. Wakaomba wale mboga na maji kwa muda wa siku
kumi. Mungu akawajalia wakaonekana wana
afya nzuri zaidi kuliko wenzao. Kwa
ajili ya kumcha Mungu, Mungu aliwapa
hekima na ufahamu katika masomo yao.
Je, tunajifunza nini kutokana na tabia, mwenendo, na Imani ya Danieli?
Msingi wa jaribu lao la
kwanza ilikuwa ni kuwafanya hao Vijana waikane imani yao na kuishi kama
Wababeli. Hawa vijana hawakukubali. Mara nyingi Jumuiya tunazoishi zinataka tufanane
nazo bali kama watu wa Mungu tuishi kati yao tukiwa tunamcha Bwana.
PAMBANO LA
PILI: UCHAWI DHIDI YA HEKIMA YA MBINGUNI
(Dan. 2:1-49)
Lengo la 2: Tambua vitu vilivyokuwemo katika sanamu aliyoiona mfalme Nebukadneza.
Mungu alimwonyesha mfalme Nebukadneza ndoto iliyohusiana na falme mbalimbali
zenye nguvu. Hizi falme
zingehusika sana kwa Taifa la Israeli.
1.
Kichwa cha Dhahabu – Dola ya Babeli (mamlaka) –
Dan. 2:37
2.
Kifua na mikono ya fedha – Dola ya Uajemi na Umedi
(Serikali ya Seri) – Dan. 2:39.
3.
Tumbo na viungo vya shaba – Dola ya Uyunani
(utamaduni ) – 2:39
4.
Miguu ya chuma – Dola ya Rumi – 2:39
5.
Nyayo zilizo nusu chuma na nusu udongo – Jumuiya ya
Mataifa 10 chini ya mpinga Kristo – 2:40
6.
Jiwe lisilochongwa na mwanadamu – Ufalme wa miaka
elfu wa Yesu Kristo – 2:42.
Lengo la 3: Eleza umuhimu wa ndoto ya Nebukadneza na
Nyakati za Mataifa.
Sanamu hii
inaelezea mambo yatakayotokea katika historia.
Kipindi hicho ni kuanzia mfalme Nebukadneza hadi kurudi mara ya pili kwa
Yesu Kristo. Nyakati za mataifa ni
wakati nchi ya Israeli itakapokaliwa na mataifa mengine.
Pili, Ndoto hii ni muhimu kwani lilikuwa shindano kati ya uchawi dhidi
ya Hekima ya Mungu. Mfalme Nebukadneza
alitaka kukumbushwa ndoto aliyoota
kwanza halafu aambiwe tafsiri. Wachawi
walipoitwa walishindwa kuielezea na kuhukumiwa kifo. Katika mistari ya 17-28
tunaona hali nzuri ya Kiroho ya Danieli na rafiki zake.
-
Walimwomba Mungu ili afunue ndoto hii (17,18)
-
Walimshukuru Mungu baada ya kupata jibu (19-23)
-
Walimpa utukufu Mungu katika yote (27,28)
Matokeo yake:-
(a) Mfalme Nebukadneza alitambua uwezo wa Mungu wa Danieli
(b) Danieli alipewa zawadi kubwa nyingi.
(c) Akapandishwa cheo cha Uliwali
(d) Rafiki zake nao wakaongezewa cheo.
Je, Tunajifunza nini katika pambano hili?
PAMBANO LA TATU: KUABUDU SANAMU DHIDI YA KUMWABUDU MUNGU
(Dan. 3:1)
Lengo la 4: Eleza matokeo ya ushindi wa vijana watatu wa Kiyahudi:
Mfalme Nebukadneza
badala ya kunyenyekea na kumwabudu Mungu aliyemwonyesha ndoto hii, anaamua
kutengeneza sanamu. Anaamuru watu wote
waisujudie. Watu wote wanasujudu isipokuwa
Shadrack, Meshaki na Abednego. Matokeo
yanakuwa hivi.
-
8-12 – Viongozi wenzao wanawashtaki
-
13-15 – Mfalme Nebukadneza anawapa nafasi ya
kutekeleza agizo ili kuepuka hukumu.
-
16-23 – Hukumu inatekelezwa kwa kutupwa kwenye
tanuru la moto.
-
24-27 – Bwana anajifunua na kuwaokoa watu wake.
Matokeo ya ushindi huu unaleta mema:
(a) Mfalme Nebukadneza anamtambua Mungu kuwa ndiye amewaokoa.
(b) Watu wanaamriwa kutomnenea lisilopasa Mungu wa Shadraka, Meshaki na
Abednego.
(c) Vijana hao watatu wakabandikwa vyeo.
Je, tunajifunza nini katika vita hivi?
Kuwa tayari kufa kwa ajili ya Yesu Kristo kuliko
kumwasi Mungu kwa kuogopa mateso. Mungu
mwenyewe ana uwezo wa kutuokoa katika mateso hayo.
PAMBANO LA NNE: KIBURI CHA MFALME DHIDI YA UTAWALA WA MUNGU.(Dan.
4:1-37)
Lengo la 5:
Je, tunapata kweli gani katika Dan. 4?
Katika sura hii mfalme Nebukadneza anaeleza ushuhuda wake.
4:18 – Anaelezea ndoto yake ya mti
uliokua sana na baadaye kukatwa.
19-27 - Danieli anaeleza tafsiri ya
ndoto kuwa mfalme Nebukadneza kuondolewa
ufalme na kula majani kama mnyama wa porini kwa miaka saba.
28-36 - Mfalme anaelezea kutimia kwa
ndoto aliyoota
37 - Mfalme anamtambua Mungu.
Ukweli tunaopata hapa ni kuwa
Mungu anahusika katika kung’oa na kuweka
Wafalme na viongozi mbalimbali. Je, tunapata fundisho gani?
(a) Kabla Mungu hajaleta hukumu humpa maonyo ili ajirekebishe
(b) Mungu hapendi mtu aliye na kiburi, hivyo humshusha.
PAMBANO LA TANO: KUFURU YA MWANADAMU DHIDI YA UTAWALA WA Mungu (Dan. 5:1-31)
Lengo la 6: Eleza dhambi ya
Belshazzar.
Karamu hii
ilifanyika mwaka 539 KK, wakati wa
mfalme Belshazzar.
Alitawala Babeli wakati baba yake Naboduis alikuwa anaongoza vita sehemu
nyingine. Wakati huu mji ulikuwa
umezingirwa na majeshi ya Wamedi na
Waajemi. Matukio wakati wa karamu:
-
Karamu
yaandaliwa na watu wasifu miungu yao – 5:1,2
-
Akiwa amelewa aagiza vyombo vya hekalu la
Yerusalemu viletwe na kutumiwa –(Mst. 2-4)
-
Kitanga chaandika maneno na wenye hekima kujaribu
kusoma (Mst.5-8)
-
Danieli aletwa kusoma na kutafsiri maandishi (Mst.
9-31)
Maandiko: MENE, MENE TEKELI , NA PERESI
MENE – Mungu ameuhesabu ufalme wako na kuukomesha.
TEKELI – Umepimwa katika mizani nawe umeonekana
kuwa umepunguka.
PERESI – Ufalme wako umegawanyika nao wamepewa
Waamedi na Waajemi.
Dhambi ya Belshazzar ilikuwa ni kufanya dhambi kwa
makusudi kutumia vyombo vitakatifu vya hekalu la Yerusalemu. Alikuwa amesikia na kumfahamu Mungu huyo.
Je, tunajifunza nini? Tusifanye dhambi kusudi kwani
tutakuwa tunamkufuru Roho Mtakatifu.
PAMBANO LA SITA:
WIVU DHIDI YA BARAKA ZA MUNGU JUU
YA MTU WAKE.(Dan.
6:1-28)
Lengo la 7: Eleza jinsi Mungu anavyowatetea watu wake.
Danieli anapewa
uongozi tena katika ufalme wa Dario huko Babeli. Huyu Dario siyo yule mfalme mkuu anayetajwa
katika Agano la Kale, huyu inawezekana
alikuwa kiongozi aliyewekwa na mfalme Koreshi kusimamia utawala. Wawili waliomo katika Baraza la uongozi
wanamwonea wivu Danieli kutokana na utendaji mzuri wa kazi. Matukio yanakuwa ifuatavyo:
-
Wanamshawishi mfalme kuandaa sheria ya kutokuomba kwa
Mungu ila kwa mfalme kwa siku 30. (4-9)
-
Daniel aendelea kuomba na akamatwa na kutupwa
katika tundu la simba(10-17)
-
Mungu amwokoa Danieli na maadui kuadhibiwa (18-24)
Matoke ya ushindi wa Danieli mfalme Dario anawataka watu kumheshimu
Mungu wa Danieli. Pia Danieli akaendelea
kufanikiwa.
Je, tunajifunza nini katika sehemu hii?
Mtu anapomtegemea Mungu, Mungu humfanikisha na kukutana mahitaji yake.
MASWALI:
- Lengo la jaribu la kwanza lilikuwa lipi ?. Je, walishindaje jaribu?
- Taja maana ya vitu vilivyomo katika sanamu aliyoiona mfalme Nebukadneza.
- Matokeo ya ndoto aliyoota mfalme Nebukadneza ni:-
(a) _____________________________
(b) _____________________________
(c) _____________________________
(d) _____________________________
- Nini matokeo ya ushindi ya vijana watatu katika Danieli sura ya 3?
- Unapata fundisho gani kutokana na adhabu ambayo Mungu anayoitoa kwa mfalme Nebukadneza? (4:1-37)
- Ni dhambi gani aliyoifanya mfalme zbelshazar? (Dan. 1:1-3)
- Kuna faida zipi za mtu kumtegemea Mungu?
SOMO LA 3 : MTAWALA WA ULIMWENGU ANAYEKUJA:
A. MAONO YA WANYAMA WANNE (Dan.
7:1-28)
Lengo la 1: Linganisha ndoto ya Nebukadneza (2) na Maono
ya Danieli – sura 7:
Kichwa
cha Dhahabu Dan.2:37
|
Simba
mwenye mabawa matatu ya tai Dan.7:4
|
Babeli
Dan.2:37
|
Kifua na mikono ya fedha Dan. 2:39
|
Dubu na mifupa mitatu ya mbavu kinywani – Dan. 7:5
|
Uajemi
Ilizishinda Misri, Ashuru, Babeli. Dan. 2:39
|
Tumbo na
viuno vya shaba 2:39
|
Chui
mwenye mabawa manne 7:6
|
Uyunani
|
Miguu ya
chuma 2:40
|
Mnyama wa
kutisha 7:7
|
Rumi - 7:23
|
Nyayo
nusu chuma, nusu udongo –2:41
|
Pembe 10
na pembe ndogo 7:8
|
Mataifa
na Mpinga Kristo – 7:24
|
Jiwe
lisilo kazi ya mwanadamu – 2:42
|
Mfano wa
Mwanadamu –7:13-14
|
Yesu
Kristo na Ufalme wa miaka elfu – 7:26-28
|
Maono haya
yalionwa na Danieli wakati wa mfalme Belshazar.
Maono haya yanayoonyesha kuwa mfumo wa utawala wa kibinadamu utatoweshwa
na ufalme wa Mungu utasimamishwa milele.
Kabla ya Yesu kutawala atakuja mpinga Kristo na kujitangaza kuwa mungu
na kuwatesa watakatifu. Atatawala kwa
miaka mitatu na nusu baada ya kuwaondoa
wafalme 3 kati ya 10. Baada ya
hapo ataangamizwa na Kristo kutawala pamoja na watakatifu .
B. MAONO YA KONDOO MUME NA
BEBERU (MBUZI DUME) – Dan. 8:1-27.
Lengo la 2: Elezea vitu na mifano
katika maono haya. Eleza umuhimu wake katika
unabii
wa Kibiblia.
Maono ya yalionwa wakati wa mfalme Belshaza. Sura hii inaonyesha kuinuka
na kuanguka kwa Dola za Uajemi na Uyunani.
1.
KONDOO MUME – 539-333 KK – Ana pembe mbili ndefu
ambazo ni Uajemi
na Umedi. Pembe ndefu zaidi ni Uajemi – utawala ulikuwa
mkubwa.
2.
BEBERU - 33
– 165 KK – Huyu ana pembe moja kati ya macho yake. Hii ni
Dola ya Uyunani ikiongozwa na Alexander- iliangusha ufalme wa
Uajemi. Pembe nne zilizozuja ni wafalme
waliozuka baa ya Alexander kufa.
(a) Kasanda - Makedonia
(b) Lysichus – Asia ya Kati
(c) Seleucus – Syria
(d) Ptolemy – Misri
3.
Mfalme anayetokeza mwisho wa ufalme wa Uyunani ni
Antonio Epifawe ambaye mkali, jeuri,
mdanganyifu na mwenye nguvu. Alilinajisi
hekalu la Mungu kwa kutoa vitu najisi.
Lakini baada ya siku 2300 za dhabihu ya asubuhi na jioni (siku 1150)
Antonio alitimuliwa katika mwaka 165 KK, hekalu likatakaswa.
C. MAOMBEZI YA DANIELI (Dan.
9:1-23)
Lengo la 3: Eleza umuhimu wa kuombea yale Mungu
aliyoahidi kutimiza.
Katika mwaka wa kwanza wa kutawala mfalme Dario mwaka 539 KK. Danieli
kwa kusoma vitabu aligundua kuwa myda wa utumwa wa miaka 70 umeisha kama
alivyotabiri Nabii Yeremia, ili yatokee.
Danieli anaomba na kutubu dhambi za watu wake. Matokeo ya maombi yake, Mungu anampa maono na
maelezo ya majima Sabini.
Je, tunajifunza
nini? Inatupasa kuombea mambo yale Mungu
aliahidi kutufanyia ili yapate kutokea na kuonyesha zaidi yaliyoko mbele yetu.
D. MAJUMA SABINI -9:24-27
Lengo la 4: Fafanua haya Majuma Sabini:
1.
Tangu kutolewa amri ya kujengwa mji na kuujenga
itachukua majuma saba ambayo ni miaka 49 (Ezra na Nehemia)
2.
Kipindi cha pili ni cha majuma 62 kutoka mji
kujengwa hadi kukataliwa kwa Masihini miaka 434.
3.
Kipindi cha mwisho ni juma moja lijalo wakati wa
mpinga Kristo ambapo Mungu atashughulika na Israeli kama taifa. Israeli wataumiliki mji mtajkatifu katika
kipindi cha kwanza cha miaka 3 na nusu na kipindi xha pili kitamilikiwa na watu
wa mataifa (Ufu. 11:2). Israeli itateswa
sana.
4.
(a) Dan. 9:24-27 inahusika na watu wa Danieli na
mji Mtakatifu maana yake
Israeli na mji wa Yerusalemu.
(b)
Majuma Sabini ni miaka 490 iliyogawanywa sehemy kuu tatu:
Majuma 7 (miaka 49), majuma 62 (miaka 434), na juma moja (miaka 7)
(c) Kuangamizwa kwa mji na patakatifu pake ni
mwaka 70 AD., ambapo
Warumi
waliuangamiza Yerusalemu na hekalu lake.
(d) Danieli hakioni kipindi cha Kanisa kwa sababu
Mungu alitaka aonyeshwe
mambo yanayohusiana
na taifa la Israeli.
5.
Katika Juma la 70 Wana-Israeli
(a) Watafanya agano na mpinga Kristo
(b) Baada ya miaka 3 na nusu agano litavunjika, mpinga Kristo ataondoa
uhuru wa kuabudu.
(c) Kutokana na mateso mwatamhitaji Masihi.
6.
Katika Majuma 70 mambo haya yatafanyika kwa ajili
ya Yerusalemu na Israeli
(a) Kukomesha dhambi
(b) Kusamehe uovu
(c) Kuleta haki ya milele
(d) Kutia mhuri maono na unabii
(e) Kupaka mafuta patakatifu sana.
- MARUDIO NA MAPIITIO:
Lengo la 5: Eleza jinsi maendeleo
ya Ufunuo katika Dan. 2,7,8,9,na umuhimu Wake.
Maendeleo ya ufunuo katika Dan. Sura 2,7,8,9,
inaanzia kwenye maelezo ya jumla katika sura ya 2 na katika sura zingine
tunaelezwa kwa undani zaidi jinsi mambo yatakavyokuwa. Umuhimu wa maendeleo ya ufunuo hatua kwa
hatua unatufundisha kuwa ili tuipate kweli lazima tusome na kupiitia sura yote.
MASWALI:
- Chora jedwali na ulinganishe ndoto ya mfalme Nebukadneza (Dan. 2:1-42) na maono ya Danieli katika sura ya saba.
- Katika Dan. 8:1-27
(a) Kondoo mume ni nani?
(b) Beberu ni nani?
- Je, kuna umuhimu gani wa kuombea mambo ambayo Mungu ameahidi kutufanyia?
- Chora mchoro unaofafanua majuma Sabini.
SOMO LA 4: SIKU ZIJAZO ZA TAABU:
A. UTUKUFU
WA YESU KRISTO.
Lengo la 1: Taja vitu
vinavyofanana na maono aliyoyaona Yohana katika Ufunuo na yale ya Dan.10:5,6.
VITU
|
DANIELI
|
UFUNUO
|
MAANA
|
Mavazi
|
Nguo za
Kitani (Mst.5)
|
Vazi
lililofika miguuni (Mst.13)
|
Hekima
|
Mshipi
|
Dhahabu
(Mst.5)
|
Dhahabu
(Mst. 13
|
Thamani
mno.
|
Macho
|
Taa za
moto (Mst.6)
|
Mwali wa
moto (Mst.14)
|
Ana uwezo
wa kuona
|
Sehemu ya
chini
|
Rangi
kama ya shaba (Mst.6)
|
Shaba
iliyosuguliwa (Mst.15)
|
Imara
|
Sauti
|
Kama ya
umati wa watu (Mst.6)
|
Ya maji
mengi (Mst.15)
|
Mamlaka
na Nguvu
|
Umuhimu wa maono haya yalikuwa
na lengo lifuatalo:
1.
Kuwatia moyo na kuwapasha watu wa Mungu juu ya
mambo yajayo
2.
Maono haya yalimpa kuelewa yale yaliyotabiriwa muda
yatakapotimia.
3.
Maono haya yalikuwa jibu la maombi ya Danieli ya muda
wa siku 21.
Maono haya Danieli aliyapata mnamo mwaka wa tatu wa utawala wa mfalme
Koreshi wa Uajemi.
B. MAPAMBANO YA
KIROHO –Da. 10:13-21.
Lengo la 2: Elezea vita vya Kiroho vinavyofunuliwa katika
sura hii.
Sura hii inatoa mfano wa upinzani dhidi ya Mungu unaotawala katika anga
hili. Majibu ya maombi ya watumishi
yanacheleweshwa kutokana na upinzani wa wakuu wa giza wanaowapinga malaika
watakatifu waletao majibu. Asifiwe Bwana
kwani hakuna mamlaka inayoweza kuzuia maombi yetu kwenda kwa Mungu. Tukivumilia majibu yanaweza kuletwa. Katika sura hizi tunajifunza kuwa kuna
malaika wa Mungu wanaosimama kwa niaba ya mataifa wakiongozwa na Mikaeli.
C. MTIRIRIKO WA
HISTORIA KUTOKA DOLA YA UAJEMI NA UMEDI HADI MWISHO WA NYAKATI.
1.
UAJEMI NA UYUNANI (Dan.11:1-4)
Lengo la 3: Onyesha mambo muhimu katika unabii kuhusiana na Uajemi na Uyunani.
Wafalme wane:
(a) Koreshi – 539 –529 KK – miaka10 (Ezra 1:1)
(b) Artashasta – 529 – 522 KK – miaka 7 (Ezra 4:7.)
(c) Ahasuero (Xerxes)
(Dario Hystaspes) – 521 – 486 KK – miaka 35 (Esta 1:1)
(d) Eexes I – 486 – 468 KK – miaka 18.
(Huyu ndiye aliyekuwa tajiri kuliko wafalme wote. Utajiri wake na jeshi la watu 800,000
lilimchochea kupigana na Wayunani.
Katika vita hivi alishindwa vibaya na Wayunani au Wagriki. Dola ya Uajemi ilidumu kwa miaka 200
(Mst.3,4) – 538 – 333 KK.Mfalme hodari ni Alexander wa Ugriki aliyeupindua na
kuangusha dola ya Uajemi katika mwaka 333.
Alifariki mwaka 323 KK bila kuwa na wana wa kutawala. Dola ya Ugriki iligawanyika katika sehemu kuu
nne chini ya wakuu wa majeshi:
(i) Kasanda -
Makedonia
(ii) Lysmauhus – Asia
(iii) Selukia – Syria
(iv) Ptolemy – Misri
N.B: Katika unabii wa sura wafalme wawili
wanahusika:
-Selukia wa
Syria (Mfalme wa Kaskazini)
-Ptolemy wa Misri
(mfalme wa Kusini)
2.
FALME ZA
PTOLEMY NA SELUKIA HADI ANTIOKIA EPIFANE –Dan.11:5-20.
Lengo la 4: Eleza umuhimu wa Ptolemy na Selukia katika historia ya
Biblia.
Hawa ni muhimu kwa sananu
Israeli ilikuwa kati ya Falme hizi mbili,
hivyo ilihusika sana katika historia yao. Kati ya 323 –178 KK Israeli ilitawaliwa na
Ptolemy mfalme wa Kusini. Hivyo
tuangalie unabii ulivyotumia.
Mst. 5: Ptolemy
I lagus au Soster ni mfalme wa Kusini aliyetawala Misri, Arabia, Libya,
Ethiopia n.k. Selukia I (mshindi) Nikano
alikuwa mfalme wa Kaskazini.
Mst. 6: Ptolemy
II Philadephus alimwoza binti yake Berenise kwa Selukia Antiokia II Theoss
mwenye mke aitwaye Laodice, ili kuleta
mapatano. Baada ya kifo cha mfalme wa
Kusini, Antiokia alimtaliki Berenice na kumrudia mkewe Laodice. Baadaye Laodice akamuua mume wake kwa sumu na
kuwuua Berenice na mtoto wake. Hivyo
mtoto wa Laodice Seleukia Callinicus akatawala.
Mst. 7-9 Ptolemy
III Euergette akamshambulia Seleukia Callinicus na kumshinda na kuteka mateka
ili kulipiza kisasi.
Mst.10-12 Wana
wa mfalme wa Kaskazini ni Selecus (mkubwa aliyeuwawa kwa sumu na Antiokia
aliyetawala kwa miaka 37. Akashambulia
Misri akashindwa na Ptolemy Epifanes.
Mst.13-16 Akishirikiana
na waasi wa Kiyahudi, Antiokia akamshinda mfalme wa Kusini na kuimiliki
Israeli.
Mst. 17 Antiokia
III baada ya ushindi alimpa Ptolemy Epifane dada yake Cleoptra awe mkewe.
Mst.18-19 Antiokia
III alitanua ufalme wake hadi Asia ya Kati na kushindwa na Warumi wakiongozwa
na Seipto.
Mst. 20: Seleukia
Philopater alitawala na kutoza Kodi kwa ukatili akauwawa kwa sumu na mtumishi
wake Heliodorus.
Je, tunajifunza
nini? Mungu ndiye anaweka na kung’oa
wafalme atakavyoYeye.
3.
ANTIOKIA
EPIFANE –Dan.11:21-45
Lengo la 5: Eleza mambo muhimu ya
unabii kuhusiana na Antiokia Epifane
aliyotumia katika Historia.
Mst. 21 – Tabia yake
Antiokia Epifane alikuwa mdanganyifu, mwenye kiburi na mjanja. Yeye alikuwa amewekwa ndani huko Rumi. Alipata ufalme kwa hila alimfanya mtoto wa
kaka yake Demeterio kuwa mfungwa badala yake.
Akatawala Syria kwa kujidai anamshikia madaraka kwa kitambo kidogo.
Mst. 22-24 – Hata shika
mapatano yake bali akishirikiana na watu wachache atavamia Mikoa tayari na
kuteka mali ambayo aliwahawia rafiki zake.
Mst. 25-28 – Antiokia
Epifane atakusanya majeshi na kumshambulia mfalme wa Kusini na kumshinda
Ptolemy Philometer na kufanya mkataba ambao haukudumu.
Mst. 29-30 – Alivamia tena
ufalme wa Kusini, lakini wakati huu alishindwa kwa Ptolemy Philometer
akisaidiwa na Warumi. Warumi walimwamuru
Antiokia kuondoa majeshi yake.
Mst. 31-35 – Baada ya
kurudi kutoma Misri huku ameshinea, hasira zake alizielekeza kwa Wayahudi na
kuondoa shughuli za Ibada katika Hekalu.
Alifanya hivi akisaidiwa na Wayahudi waasi. Akalinajisi
hekalu kwa kutoa vitu
vilivyonajisi. Wayahudi wengine
waliowaaminifu walishikilia Imani yao, Wengi kati yao waliuawa.
Mst. 36-39 – Antiokia
Epifane alimkufuru Mungu Aliye juu kwa kuondoa dhabihu zake na kunajisi Sabato,
hekalu na watu wa Mungu. Pia alidharau
miungu na baba zake na kuleta miungu ya kigeni ya Wayunani (Jupiter olympius)
Mst. 40-43 – Mfalme wa
mwisho Kusini alivamia tena utawala wa Antiokia Epifane , lakini alishindwa
tena. Mfalme wa Kaskazini aliteka mali
nyingi ya Wamisri.
Mst. 44-45 – Habari za
maadui kutoka Mashariki na Kaskazini ni majeshi Waajemi na Waapathi
zikamsumbua. Akaingia na kuwateka
Wayahudi. Lakini aliugua ugonjwa
usioponyeka na kufa.
N.B: Antiokia Wpifane alikuwa
kivuli cha mpinga Kristo atakayekuja.
FALME MBILI:
KUSINI (Ptolemy) KASKAZINI
(Seleukia)
Ptolemy I Soster –323 –285 Seleukia
Nicator – 312-280
Ptolemy II Philadelphus –285-246 Antiokia
I Sater – 280-261
Ptolemy III Euergetes – 246 – 221 Antiokia
II (Theos) – 261 –246
Ptolemy IV Philopator – 221 –204 Selukia
II Callinicus –246-226
Ptolemy V – Epifane – 204 – 181 Selukia
III Ceranus –226-223
Ptolemy VI Philometa –181-145 Antiokia
III 223-187
Selukia
IV –187-175
Antiokia
IV Epifane –175-164
D. WAKATI
WA TAABU – Dan. 11:36-12:13
Lengo
la 6: Taja ushahidi ambao unayaweka
matukio yaliyomo katika Danieli 12 kutoka katika Juma la Sabini.
Dan 11:36 – 45 inazungumzia juu ya kutokea kwa mpinga Kristo atakaye
vamia taifa la Israel na kujitangaza kwamba yeye ni Mungu anayetakiwa kuabudiwa.Atafanya
kazi kwa miaka mitatu na nusu baadaye kuangamizwa.
Ushahidi katika sura 12 unaonyesha kuwa wakati wa taabu utatokea katika
kipindi nusu ya pili ya juma la Sabini.
Kipindi hicho kitakuwa cha miaka 3 na nusu. Kipindi hicho kitaanza wakati mpinga Kristo
amevunja mkataba wa amani na Wayahudi.
Matukio ya wiki
ya sabini ni kama ifuatavyo:-
1.
Kitaanzishwa na ujio wa mpinga Kristo atakayeongoza
mataifa kumi.
2.
Ataweka mkataba wa amani na Wayahudi wa miaka saba. Baada ya miaka 3 na nusu
mkataba utavunjwa.
3.
Atawageukia Wayahudi na kuwatesa kwa lengo la
kuwaangamiza, lakini malaika Mikaeli atawasaidia na watakatifu kuokolewa.
4.
Kabla ya Mungu kuanzisha ufalme wake ataondosha
utawala wa mpinga Kristo.
5.
Watakatifu waovu watafufuliwa kuingia katika aibu
na watakatifu katika baraka ya milele.
MUHTASARI WA MATUKIO MUHIMU:
605 KK – Mateka wa kwanza kupelekwa Babeli akiwemo Danieli na rafiki
zake
597 KK – Mateka wengine wapelekwa Babeli akiwemo Ezekieli
587 KK – Yerusalemu uliangamizwa na watu kupelekwa utumwani Babeli.
587 KK – Koreshi anakuwa mfalme wa Uajemi.
550 KK – Uajemi yaishinda Umedi
539 K K – Uajemi yaishinda Babeli
538 KK – Kundi la kwanza la Wayahudi wakiongozwa na Zerubabeli warudi Yerusalemu. Kazi ya ujuzi wa Hekalu yaanza
516 KK – Hekalu laisha kujengwa.
458 KK – Wakiongozwa na Ezra Wayahudi kundi la pili warudi Yerusalemu.
445 KK – Nehemia aenda Yerusalemu kama Gavana
333 KK – Alexander Mkuu aishinda Uajemi
323 KK – Dola ya Ugriki inagawanyika katika sehemu nne.
301-198 – Palestina ilitawaliwa na Misri
(Ptolemy)
198 –143 – Palestina ilitawaliwa na Syria
(Seleukia)
171 KK – Antiokia Epifane anakuwa mfalme wa Syria
168 KK – Antiokia Epifane alinajisi Hekalu la Wayahudi
165 KK – Wayahudi waliongozwa na Makabayo wanalikomboa Hekalu.
145 KK – Palestina yapata uhuru.
63 -
Dola ya Rumi wateka Palestina
6
- Kuzaliwa
kwa Yesu
31 BK – Kufa na kufufuka kwa
Yesu Kristo
70 BK -
Kuangamizwa kwa Yerusalemu na Warumi.
MASWALI:
- Umuhimu wa maono ya sura ya 10 ulikuwa una lengo lifuatalo:
(a) ______________________
(b) ______________________
(c) ______________________
- Katika sura ya 10:13-21 kuna vitu gani vya kiroho vinavyofunuliwa?
- Taja mambo ambayo wafalme hawa waliwafanyia Wayahudi:
(a) Koreshi ____________________________
(b) Antashasta _________________________
(c) Ahasuero __________________________
- Antiokia Epifane anakumbukwa kwa matendo gani aliyowatendea Wayahudi?
- Taja matukio matano yatakayotokea katika juma la Sabini.
_______________________________________________________________________________________________________________
SEHEMU
YA 2 – KUANZA KWA MATUKIO YA SIKU ZA MWISHO:
SOMO
LA 5: KITABU CHA UFUNUO:
Lengo la 1: Taja mambo matano yanayoelezea chanzo cha
Ufunuo katika sura ya 1:-
Mambo matano yaliyodhihirishwa
katika sura ya 1 ni:-
1.
Ufunuo wa Yesu Kristo 1:1
2.
Ujumbe huu uliwasilishwa kwa Yohana kupitia Yesu
Kristo, malaika na maono – 1:1,10-18
3.
Ujumbe huo uliletwa kwa Yohana – 1:1,4,9,2
4.
Alipewa ujumbe huu akiwa mfungwa katika kisiwa cha
Patmo
5.
Walengwa wa ujumbe yalikuwa makanisa saba katika
Jumba la Asia.
Kitabu hiki kiliandikwa wakati wa utawala wa Domitian aliyetaka watu
wamwabudu kama Mungu. Amri hii ilileta
matatizo na mateso kwa wakristo. Hivyo
kitabu hiki kiliandika katika mazingira haya.
M A K U S U D I:
Lengo la 2: Eleza kusudi la
kuandikwa kwa kitabu hiki>
Kusudi la kuandikwa kitabu hiki liko katika sehemu tatu:-
1.
Nyaraka zilizoandikwa zilikuwa za kukemea makanisa
yaliyoridhia dhambi bila kuikemea.
2.
Kutokana na mateso ya Domitian aliyetaka kuabudiwa
– kitabu hiki kiliandika kuwatia moyo kuvumilia mateso na kuwa waaminifu hadi
kufa.
3.
Kiliandikwa kwa ajili ya Kanisa la Kizazi chake ili
kuwaonyesha waamini juu ya mapambano waliyo nayo dhidi ya majeshi ya
shetani. Jinsi kuja kwa pili kwa Yesu
Kristo kutakavyokomesha utawala mwovu wa mpinga Kristo.
M H U S I K A:
Lengo la 3 : Eleza mhusika mkuu
linazungumzwaje:
Mtiririko wa kitabu
cha Ufunuo ni kuelezea kuja mara ya pili kwa Yesu Kristo (Ufu.1:7). Mhusika Mkuu katika kitabu cha Ufunuo ni Yesu Kristo mwenyewe. Yale aliyokwishafanya, anayofanya sasa na
yale atakayofanya baadaye.
MWANDISHI NA TAREHE:
Lengo la 4: Orodhesha ushahidi wa Uandishi na Tarehe ya Kitabu cha
Ufunuo:
Kitabu hiki
kiliandikwa na Yohana Mtume wakati wa utawala wa Kaisari Domitian mnamo mwaka
kati ya 91-96 BK. Ushahidi tunaopata ni
matumishi ya maneno “Logos” “Nikao” na “Ekkenteo” (kushinda na kuchoma). Pia ushuhuda wa Viongozi wa mwanzo wa kanisa
kama Justin Martyr unathibitisha kuwa mtume Yohana aliandika, ushahidi wa ndani
ya kitabu unahusiana na kuwa kifungoni kisiwani Patmo huko Asia ya Kati.
SEHEMU KUU ZA KITABU:
Lengo la 5: Eleza sehemu kuu za
Kitabu.
Katika Ufu. 1:19 Yesu mwenyewe anaelezea:-
A. Utangulizi – 1:1-8
B. Yale uliyaona 1:9-20
C. Nayo yaliyopo 2-3
D. Yatakayokuwepo baadaye – 4:1-22:6
(a) Kanisa katika Utukufu – 4:1-5:14
(b) Dhiki Kuu – 6:1- 19:21
(c) Miaka elfu -20:1-6
(d) Gogu na Magogu – 20:7-10
(e) Kiti cheupe 2:11-15
(f) Mambo yote mapya – 21:1-22:6
E. Hitimisho - 22:7-21
Maelezo ya Zaidi:
Ni maelezo ya kina kuhusiana na jambo lililokwisha
elezwa tayari.
Sura ya 7 -
Wayahudi 144 na waliovikwa mavazi meupe.
Sura ya10 -
Malaika mwenye nguvu mwenye Gombo au kitabu
Sura 11:1-14 – Mashahidi wawili
Sura ya 12
- Mwanamke, mtoto na Joka
Sura ya 13
- Wanyama wawili
Sura ya
14 - 144,000 (Israeli), mwisho wa Injili
kuhubiriwa, Tangazo la Kuangushwa kwa Babeli, mavuno ya mwisho na shinikizo.
Sura ya 17
- Wanyama wawili na kahaba mkuu
Sura ya 18
- Babeli
MASWALI:
- Chanzo cha Ufunuo ni kipi?
- Taja makusudi matatu ya kitabu cha Ufunuo
- Nani mhusika Mkuu wa kitabu hiki?
- Taja sehemu kuu za kitabu hiki.
SOMO LA 6: KANUNI ZITAKAZOKUSAIDIA KUELEWA UJUMBE WA UFUNUO:
A. MAONI MANNE NA MAANA ZAKE:
Lengo la 1: Tambua njia nne tofauti zinazotumiwa na watu
mbalimbali kutafsiri Kitabu cha Ufunuo:
1. Preterest: Unabii huu ulitimizwa wakati wa
Kanisa la kwanza lilipopitia katika
mateso yaliyoendeshwa na Warumi. Wengine wanaamini kuwa unabii ulitimizwa
mwaka 70 BK wakati Yerusalemu ulipoangamizwa.
2. Historicit: Nabii hizi zinahusiana na watu na
matukio mbalimbali yaliyotokea huko nyuma – km. Napoleon
na kuinuka kwa Uislam.
3. Idealist: Matukio
yanaelezea mifano ya kiroho kuhusiana na mapambano kati ya Mungu na shetani.
4. Futurist : Nabii hizi zinahusiana na matukio halisi yatakayotokea
siku zijazo ili kukamilisha mpango wa Mungu.
B. MAMBO MUHIMU:
Lengo la 2: Eleza kanuni za
kutafsiri ujumbe wa kitabu cha Ufunuo:
Kitabu cha Ufunuo ni cha aina ya
Apokrifa, hivyo:-
(a) Kinatumia ishara na mifano kutoa ukweli
(b) Malaika wanaoelezea matukio
(c) Kinaonyesha ushindi wa Mungu juu ya shetani.
KANUNI ZA KUTAFSIRI NA MAANA ZAKE:
Kanuni Na. 2- Acha Maandiko yatafsiri yenyewe – Eze. 12:1-16
Kanuni Na. 2 – Tumia mwonekano wa unabii – mf. Lk. 4:16-21; Isa. 61:1,2
Kanuni Na 3 – Tambua kutumia mara mbili kwa andiko la unabii
Kanuni Na. 4 – Elewa matumizi ya ishara na mifano.
Aina za mifano Mfano Maana:
Namba moja Mungu
Mbili Kuhakikishwa
Tatu Utatu
Nne Dunia
Sita Mwanadamu,
uovu
Saba Utimilifu
wa Mungu
Kumi Kukamilika
kwa siasa
Kumi
na mbili Mwisho
wa kukamilisha
Wanyama Mwanakondoo Yesu
Farasi Uwezo wa
Kijeshi
Wanyama Mpinga Kristo na
nabii wa uongo
Vyura Mapepo
wachafu
Silaha Yesu
Rangi Nyeupe Utakatifu
Nyekundu Damu vitani
Nyeusi Baa la
Tauni
Zambarau Anasa za Kifalme
Kijani Burudisho
Kijivujivu Mauti.
MASWALI:
1.Taja
maoni manne na maana zake kuhusiana na Uufunuo.
2.
Orodhesha kanuni nne za kutafsiri kitabu cha Ufunuo.
SOMO LA 7: YALE YOHANA ALIYAONA:
A. CHANZO
NA KUSUDI LA UFUNUO:
Lengo la 1: Eleza chanzo cha
Kitabu cha Ufunuo na ujumbe wake.
Chanzo cha ujumbe wa kitabu ni Mungu akiwa na lengo la kuifunua kweli
kwa watumishi wa Mungu. Hivyo
kitaeleweka kwa watu wake kwa sababu wanayo hekima kutoka kwa Mungu.
B. EN TACHEI:
Lengo la 2: Eleza maana ya neno “upesi” - Ufu. 1:1
Yesu alimtuma malaika wake kumwonyesha Yohana
mambo ambayo hayana budi kuja upesi – neno upesi linatokana na neno la Kigriki
“En Tachei” likiwa na maana “mara moja “
upesi, ghafla, wakati wowote.
C MAANA YA “MALAIKA”:
Lengo la 3: Eleza njia mbali mbali za Kibiblia kuhusiana
na neno “Malaika” na
Ujumbe alioonyeshwa Yohana (Ufu.1:2)
Ufu. 1:1 unaonyesha kuwa neno “malaika” lina maana ya mpeleka habari
(tarishi). Hii inaonyesha kuwa Yesu Kristo alifunuliwa kwa Yohana na
malaika. Katika Biblia kuna malaika wa
aina mbili:
Wajumbe wa kimwili na wa
Ki-Mungu. Huyu malaika alitoa ujumbe kwa
kutumia ishara na mifano. Mambo mawili
yaliyofunuliwa ni Neno la Mungu na ushuhuda wa Yesu Kristo.
D. HERI
SABA ZILIZOMO KATIKA UFUNUO (1:3-5)
Hizi
ni baraka za Mungu kwa watu watakaotenda mambo Fulani.
Lengo la 4 : Orodhesha Heri hizo.
1. Ufu. 1:3 - “Heri asomaye na wao wayasikiao
maneno ya unabii huu na kuyashika yaliyoandikwa..”
2. Ufu. 14:13 -Heri wafu wafao katika Bwana,
tangu sasa wapate kupumzika.
3. Ufu. 16:15 - Heri akeshaye na kuyatunza mavazi
yake asiende uchi..”
4.
Ufu. 19:9 -
Heri walioalikwa karamu ya Arusi ya Mwanakondoo
5.
Ufu.20: 6 -
Heri na Mtakatifu ni yeye aliye na sehemu katika ufufuo wa Kwanza
6.
Ufu. 22:7 - Heri yeye ashikaye maneno ya unabii wa
kitabu hiki.
7.
Ufu. 22:14 – Heri wazifuao nguo zao, wawe na amri
kuuendea huo mti wa Uzima.
E. ROHO SABA ZA MUNGU – Ufu. 1:4
Lengo la 5: Onyesha Roho saba ni
nini?
Roho saba za Mungu maana yake ni ukamilifu wa huduma ya Roho Mtakatifu
kwa Kanisa la Mungu.
F. AINA TATU ZA KUJITAMBULISHA
KWA YESU – 1:5,6
Lengo la 6: Eleza jinsi Yesu
anavyojitambulisha.
(a) Yesu ni Shahidi mwaminifu
(b) Mzaliwa kwa Kwanza wa walio hai
(c) Mkuu wa Wafalme wa dunia.
G. ALFA NA
OMEGA –1:8
Lengo la 7: Eleza sababu inayomfanya Yesu aitwe Alfa na
Omega.
Yesu anaitwa Alfa
na Omega kwa sababu herufi za Kiyunani zinaelezea kuwa katika yeye Mungu Baba
aliumba vitu vyote na katika yeye Baba ataleta mwisho wa kila kitu.
H. NENO TAZAMA – 1:7
Lengo la 8: Eleza maana tofauti za neno Tazama, katika kifungu hiki lina
maana ya:
(a) Kuona kwa macho ya kimwili
(b) Kuelewa au kufahamu
(c) Kushangaa na kujiuliza.
I. SIKU YA
BWANA - 1:10
Lengo la 9 : Eleza maana ya siku
ya Bwana.
Katika mstari huu una maana siku ya kwanza ya juma, Jumapili. Yohana alikuwa katika roho
siku hiyo.
J. SAUTI, AMRI
NA MAONO – 1:10-16
Lengo la 10: Elezea Yesu aliyeonwa na Yohana.
Yohana alimwona Yesu katika Utukufu
wake.
a.
Vazi lililofika miguuni - Ukuu wa Yesu kama nabii, kuhani na mfalme.
b.
Kichwa na
nywele zake - Utakatifu,, hekima
na Umilele wa Yesu
c.
Macho kama mwali wa moto- Anajua yote
d.
Miguu kama
shaba iliyosuguliwa -
Hukumu ya Yesu kwa watu
e.
Sauti ya majimaji -
Mamlaka na nguvu za Yesu
f.
Mkono wake wa kuume -
Kujali, msaada na kudhibiti kwa Yesu
g.
Upanga utokao kinywani - Neno lenye mamlaka ya Yesu
h.
Uso kama jua katika nguvu zake – Utukufu , Ukuu na
Utakatifu wake.
K. MAUTI NA KUZIMU -
1:17,18
Lengo la 11 : Eleza neno “Paradiso”, jadili mahali ilipo.
Kufuatana na Maandiko, Paradiso ni mahali pa kuwafariji watakatifu
waliokufa. Wakati wa Agano la Kale
paliitwa kifuani pa Ibrahimu huko kuzimu.
Yesu alipokufa na kufufuka Paradiso ilihamishwa mbinguni. Hivyo kuzimu ni mahali wanapokwenda waovu
wanaokufa.
NYOTA NA VINARA VYA TAA - Ufu. 1:19,20
Lengo la 12: Elezea maana ya
nyota na Vinara.
Nyota saba ni
malaika saba ikiwa na maana ya wachungaji wa Makanisa. Vinara saba ni makanisa
saba (Mst.20) ambayo yamewekwa kuwa nuru ya kumfunua Yesu Kristo kwa watu. Yesu yupo katikati ya vinara kuonyesha uwepo
wa Mungu upo ndani ya kanisa na wachungaji wapo mikononi mwake.
MASWALI:
- Neno “ Malaika” lina maana gani katika Ufunuo.
- Orodhesha heri zilizomo katika Ufunuo
- Siku ya Bwana inayotajwa Ufu.1:10 ni ipi?
- Nini maana ya Alfa na Omega – Ufu.1:8
SOMO LA 8:
NYARAKA KWA EFESO, SMIRNA NA PERGAMO:
Lengo la 1: Orodhesha mambo yaliyomo katika barua
zilizoandikwa kwa.
Makanisa Saba:
a.
Salamu kwa Kiongozi wa kila Kanisa.
b.
Tabia na hali za Yesu Kristo.
c.
Yale Yesu anayajua kwa kila Kanisa
d.
Yale anayoyafurahia katika kila Kanisa isipokuwa Laodekia
e.
Yale Yesu aliyakosoa na kukemea katika kila Kanisa
isipokuwa Smirna na Filedefia.
f.
Ahadi kwa kila Kanisa
g.
Ushauri kwa kila Kanisa kusikia ujumbe
h.
Ahadi kwa washindi
N.B: Jumbe kwa
Makanisa saba inaelezea hali ya Kiroho iliyokuwemo ndani
Ya Makanisa hayo. Hali hiyo inalingana na Makanisa ya vizazi
vyote.
(i)
BARUA KWA KANISA LA EFESO:
Lengo la 2: Eleza Historia na
hali ya Kanisa la Efeso.
Efeso ulikuwa mji na
bandari wenye ibada za sanamu uliozungukwa na mashamba mazuri.
(a) Kanisa lilianzishwa na Paulo katika safari ya tatu ya Utume. Watu wengi
waliokolewa na kuchoma uchawi wao (Mdo.19:1-41). Paulo alifanya kazi Efeso kwa muda wa miaka 3
(Mdo. 20:31)
(b) Baadaye Kanisa hili alilisimamia Timotheo ili kukemea mafundisho potofu
yaliyoletwa na baadhi ya waamini (1Tim. 1:3)
(c) Kanisa lilisifiwa na Yesu kuwa mambo matano mazuri:-
BIDII,UVUMILIVU,KUTOVUMILIA UOVU, KUWAJARIBU WATIITAO MITUME, KUCHUKIA
MAFUNDISHO YA WANIKOLAO.
(d) Lilikemea kwa kupoteza upendo wa kwanza; hivyo lilikuwa katika hatari ya
kutengwa.
Fundisho: Uhusiano
wetu na Yesu uwe wa kwanza kuliko vitu vyote, mfano
Mke, watoto,
kazi, nk.
(ii)
BARUA KWA KANISA LA SMIRNA –2:8-11
Lengo la 3: Eleza hali na mistari
ya Kanisa la Smirna.
(a) Mju wa Smirna ulichukua jina kutokana na manukato yaitwayo Myrrh .
Ulikuwa mji tajiri katika Asia ya Kati
(b) Ulikuwa na Wayahudi wenye nguvu na wapinzani wa Injili.
(c) Kanisa lilikuwa na watu maskini na wenye kupitia mateso. Wayahudi walikuwa wanawatukana Wakristo.
(d) Yesu anaonya kuwa baadhi yao watatupwa gerezani wawe waaminifu mpaka
kufa.
Fundisho: Yesu
Kristo anajua majaribu tunayopitia, anataka tuwe
waaminifu
na atatupa taji ya uzima.
(iii)
BARUA KWA KANISA LA PERGAMO – 2:12-17
Lengo la 4: Eleza hali na Historia ya Kanisa.
(a) Mji wa Pergamo ulikuwa makao makuu ya kisiasa na dini katika Asia ya
Kati. Ndipo palikuwa pa kwanza kuanzisha
kumwabudu Kaisari (kiti cha enzi cha shetani).
(b) Yesu anajitambulisha kwa kuwa na upanga mkali maana yake anakosoa
mafundisho potofu.
(c) Kanisa linasifiwa kwa uaminifu na kushikilia Imani.
(d) Yesu analikosoa kwa kuwavumilia watu wenye Imani potofu.
(Mafundisho ya Ballam – ibada ya sanamu na uzinzi- mafundisho ya
Wanikolao).
Fundisho: Lazima waamini wasipinge imani potofu na
mafundisho potofu.
(iv)
BARUA KWA KANISA LA THIATIRA –2:18-29
Lengo la 5: Eleza hali na
Historia ya Kanisa:
(a) Kanisa lilikuwa katika mji wa viwanda vya nguo vya zambarau. Lydia
alitokea hapa.
(b) Yesu alilisifu Kanisa kwa mambo manne – (UPENDO, IMANI, HUDUMA, SUBIRA)
(c) Yesu analikosoa Kanisa kwa kumridhia Mwanamke nabii wa uongo mwenye
tabia za Yezebeli.
Fundisho: Yesu
anachukua Kanisa likifumbia macho walimu wa uongo
Yesu anaahidi kuwashughulikia wote
wafundishao uongo.
(v)
BARUA KWA KANISA LA SARDI - 3:1-6
Lengo la 6: Elezea Historia na
hali ya Kanisa:
(a) Mji wa Sardi ulikuwa juu ya mlima katika njia kuu ya biashara. Ulikuwa na ngome imara ya kijeshi na tajiri,
uliojengwa na Kaisari Tiberia.
(b) Yesu anajitambulisha kuwa anazo hizo Roho saba, kuonyesha kuwa anafahamu
matendo ndani ya Kanisa. Watumishi wanawajibika kwake.
(c) Kanisa linakemewa kwa kuonekana kwa jina
liko hai , lakini ukweli limekufa.
(d) Baadhi ya waamini walikuwa safi.
Fundisho: Kanisa linatakiwa kuwa
hai Kiroho.
(vi)
BARUA KWA KANISA LA FILEDEFIA – 3:7-13
Lengo la 7: Eleza Historia na hali ya Kanisa
(a)
Kanisa lilikuwa katika mji uliojengwa na mfalme Pergamo. Ulichukua jina la
mjenzi Akalus Phidadefia.
(b) Mji ulikuwa unakabiliwa na matetemeko na makao ya ibada ya kipagani.
Uliitwa Athens ndogo.
(c) Yesu analisifia Kanisa kwa mambo matatu.
·
Linazo nguvu kidogo
·
Limetunza Neno lake
·
Halikujulikana jina la Yesu.
(d) Yesu analiahidi mambo manne:
·
Atawafanya kuwa nguzo katika Hekalu la Mungu
·
Ataandika jina jipya la Mungu juu yao
·
Ataandika juu yao jina la mji wa Mungu
·
Ataandika juu yao jina lake jipya.
(vii)
BARUA KWA KANISA LA LAODEKIA – 3:14-22
Lengo la 8: Eleza historia na
hali ya Kanisa.
(a) Kanisa lilikuwa katika mji tajiri kwa viwanda, nguo na maziwa, madawa na
mabenki.
(b) Mji huu uliopewa jina la malkia Laodekia ulikuwa na bomba la maji
vuguvugu.
(c) Kanisa halina sifa njema Yesu analikemea kwa tabia ya uvuguvugu
iliyo nayo na kulishauri kutubu.
Fundisho: Yesu
hapendi mtu vuguvugu anataka mtu aamue kumfuata
yeye au
hapana.
HALI TATU ZA KIROHO:
1.
Hali ya moto - Mwamini mwaminifu aliyejitoa kikamilifu kwa
Bwana. Ameokolewa na anamfuata Yesu Kristo.
2.
Hali ya uvuguvugu –Ni mtu aliyeokolewa lakini hajafikia kiwango cha Kristo na Injili
yake.Anashika baadhi ya mambo ya Mungu.
3. Hali ya Ubaridi - Mtu anaishi kama
ulimwengu hana hamu ya mambo ya kiroho
na Mungu.
MASWALI:
- Orodhesha sifa zilizotolewa na Yesu kwa kila Kanisa.
- Orodhesha udhaifu unaotolewa kwa kila Kanisa.
SEHEMU YA 3: MAENDELEO YA MATUKIO KATIKA SIKU YA MWISHO:
SOMO LA 9: KANISA NA DHIKI
KUU:
A. MAANA YA USEMI “BAADA YA
HAYO” – 4:1.
Lengo la 1: Eleza maana ya usemi
huu:
Usemi huu unatokana na neno la Kigriki “Meta tauta” likiwa na maana ya
yale yatakayotokea baada ya kipindi cha Kanisa.
B. MLANGO UKAFUNGUKA MBINGUNI –
4:2
Lengo la 2: Eleza juu ya maoni ya kuwa tendo la Yohana kuchukuliwa toka
duniani kupitia mlango uliofunguliwa
kwenda mbinguni kunahusiana na unyakuo wa Kanisa.
1.
Yesu alisikia sauti ya Yesu Kristo, Yohana
anaambiwa “panda hata huku” mara moja.
Mambo yanabadilika mbinguni.
2.
Kunyakuliwa kwa Yohana 4:1-2 kunaonekana
kuwakilisha kunyakuliwa Kanisa kabla ya dhiki Kuu. Hii inadhihirisha ya kuwa Kanisa litaondolewa
kabla ya dhiki kuu.
3.
Pia neno Kanisa halitumiki baada ya sura ya 3 hadi
22.
C. UPEKEE WA
DHIKI KUU:
Lengo la 3: Eleza kwa nini dhiki
kuu ni jambo la pekee katika historia ya Binadamu duniani.
Dhiki kuu ni tukio la pekee katika historia katika dunia , kwa sababu ni
dhiki pekee ambayo inaitwa siku kubwa ya hasira ya Mungu.
D. UNYAKUO WA
KANISA –(1Thess. 4:11-13)
Lengo la 4: Eleza mambo yatakayotokea wakati wa kunyakuliwa Kanisa.
Tunaamini Kanisa litanyakuliwa kabla ya dhiki kuu , kwa sababu hatusomi
neno lolote “Kanisa” kutoka Ufu. 4:1-22.
Hivyo Kanisa halitapitia katika dhiki kuu (1Thes. 5:9). Mambo mawili yatatokea wakati Yesu anakuja
kwa mwaliko mkuu kutoka mbinguni- Baragumu Italia:
(a)
Kwanza, wafu waliolala katika Kristo watafufuliwa.
(b) Pili, walio hai watabadilishwa na kunyakuliwa pamoja na wafu
waliofufuliwa kumlaki Bwana hewani.
N.B: Yesu ataleta roho za waliokuwa katika Bwana pamoja
naye ili kuungana na Miili iliyofufuliwa.
E. MANENO YANAYOTUMIWA KATIKA
KUJA KWA YESU:
Lengo la 5: Eleza maana ya
maneno ya Kigriki yanayotumiwa, maneno
ni:
(a) HARPADZO - Kunyakua
kwa nguvu
(b) EPIPHANELA - Mg’ao
(c) PAROUSIA - Kuja mwenyewe.
F. MAJADILIANO YA MWASWALI
MATATU KUHUSIANA NA SIKU ZA MWISHO (Mt. 24:3)
(a) Mathayo haelezi jinsi Yesu alivyojibu maswali, bali Luka anaelezea
majibu. Siku za mwisho zitaambatana na
usaliti, wakristo wa uongo, chuki na mateso kwa waamini. Pamoja na kurudi nyuma kwa watu, Injili
itahubiriwa duniani pote.
(b) Yesu alielezea matukio ambayo yangetokea mara moja na yale yangetokea
baada ya muda mrefu katika taifa la Wayahudi hasa kuangamizwa kwa hekalu na mji
wa Yerusalemu. Alieleza.
(c) Anaelezea na dalili zitakazoonyesha kuja kwake.
Mt. 24:2-14 – Yesu anaelezea mambo yatakayotokea kabla ya Kanisa
kunyakuliwa:-
1.
Manabii na wakristo wa uongo watakaowadanganya watu
wengi.
2.
Kuongezeka kwa vita, njaa na matetemeko yatakuwa
mwanzo wa utungu.
3.
Mateso yataongezeka zaidi kwa waamini na wengi wao
wataacha imani.
4.
Vurugu, uhalifu na kuasi sheria za Mungu
kutaongezeka.
5.
Injili ya Kristo itahubiriwa duniani pote.
Mt. 24:42-44 - Hakuna ajuaye saa
ya Yesu kuja kunyakua Kanisa. Siku itakuja ghafla kwa waamini na wasioamini.
Mt. 24:15-28 - Yesu anaelezea matukio yatakayotokea wakati
wa kipindi cha dhiki ambayo waliookoka wakati huo watayaona kabla ya Yesu kurudi mara ya pili.
1.
Chukizo la uharibifu lililonenwa na nabii Danieli
2.
Kutokea kwa manabii na wakristo wa uongo watakaowadanganya
hata wateule.
3.
Taabu na dhiki kubwa
4.
Jua na Mwezi kutiwa giza na nyota kuanguka.
5.
Yesu atarudi mara ya pili.
Mt. 25:1-13 – Mfano wa Wanawali Kumi:
Huu mfano unaonyesha unyakuo
utawajia ghafla waamini waaminifu na wasio waaminifu. Yesu anatuasa kuwa hatangojea kanisa lote
lijiandae. Hivyo kila mwamini anatakiwa
kujiandaa kwa kuishi maisha matakatifu na kuwa na Uwepo wa Roho Mtakatifu.
Mt. 25:14-30 - Mfano wa
Talanta:
Hapa Yesu anatueleza kanuni
muhimu zitakazoamua nafasi ya mwamini katika ufalme wa mbinguni. Nafasi na thawabu zitategemea jinsi
ulivyojitoa kwa Bwana na Ufalme wake.
Mt. 25:31-46 – Hukumu ya
Kondoo na Mbuzi:
Kondoo -ni watu waliookoka na wako
hai wakati wa dhiki kuu.
Mbuzi – ni watu waovu waliosalia
wakati wa dhiki kuu.
Hukumu inahusiana na :-
1.
Kutenganishwa kwa watu waliookolewa na watu waovu.
2.
Na matendo ya upendo na huruma kwa wale walioteseka
kwa ajili ya Yesu.
3.
Waovu watatupwa katika ziwa la moto na wenye haki
watakuwa raia katika ufalme wa Mungu.
ANAYEZUIA NA MPINGA KRISTO:
Lengo la 6: Mtambue anayezuia uovu na mpinga Kristo:
(a) Walimu wa uongo wamekuwa wanawaambia Wathesalonike kuwa siku ya Bwana
imekwisha pita. Hivyo waliamini kuwa
wameachwa.
(b) Mambo mawili ambayo lazima yatokee kabla ya dhiki kuu:
(i)
Uasi mkuu utatokea
(ii)
Mpinga Kristo atatokea.
(c) Roho Mtakatifu akitenda kazi kupitia Kanisa ndiye anazuia uasi na Mpinga
Kristo.
(d) Mwovu atakuja katika mamlaka kwa njia ya udanganyifu na kufanya
miujiza. Hivyo watu wengi watampokea kwa
sababu ya kukataa kweli.
(e) Jinsi tunavyoendelea mwisho wa nyakati uasi na uovu unaongezeka. Utafikia kilele wakati wa mpinga Kristo.
MASWALI:-
1.
Kunyakuliwa kwa Yohana kwenda mbinguni kunawakilisha nini?
2. Taja
mambo mawili yatakayotokea wakati wa kunyakuliwa kwa Kanisa.
3. Katika
waraka wa Wathesalonike Paulo anasema yupo azuiaye kutokea kwa mpinga
Kristo. Huyo ni nani?
4. Ni mambo gani Yesu anaelezea katika sura zifuatazo:-
(a) Mt. 24:4-14
(b) Mt. 24:42-44
(c) Mt. 24:15-28
SOMO LA 10(a): MWANZO WA JUMA LA
SABINI:
A. MWENYE
KITI CHA ENZI MBINGUNI – 4:3
Lengo la 1 : Mtambue mwenye kiti cha Enzi mbinguni.
Mwenye Kiti
cha Enzi mbinguni ni Mungu mwenyezi. Anayeishi katika utukufu akiwa amezungukwa
na viumbe vinavyomwabuudu. Upinde wa
mvua ulikizunguka Kiti unaonyesha Ahadi za Mungu.
B. MAELEZO
KUHUSIANA NA WAZEE ISHIRINI NA NNE -
Ufu. 4:4
Lengo
la 2: Elezea na kuwatambua wazee Ishirini na Nne (Ufu. 4:4)
Wazee wamevaa mavazi meupe na taji
za dhahabu vichwani mwao wanaonyesha ni watu waliokombolewa kwa sababu:-
(a)
Mavazi meupe ni kwa ajili ya watu waliokombolewa.
(b)
Taji za dhahabu wanapewa waliokombolewa baada ya kumshinda shetani-3:3
(c) Kufuatana na Ufu.21:12-14 – ukuta wa Yerusalemu una milango 12 yenye
majina ya makabila 12 ya Israeli na misingi 12 yenye majina ya mitume 12.
(d) Hakuna katika Biblia ambapo malaika hutajwa kama wazee.
(e) Kutokana na Ebr. 11:39,40 na Ufu. 21:12-14 inaonekana wazee hao
huwakilisha watakatifu wa Agano la Kale na A/Jipya.
C. VITAMBUE VIUMBE HAI WANNE –
4:6-11
Lengo la 3: Eleza viumbe.
Viumbe hai wane vipo kwa ajili ya kusifu Mungu mwenyezi. Inawezekana viumbe hivi vinawakilisha viumbe
wote. Viumbe vyote vitaleta utukufu na
heshima mbinguni wakati vitakapokombolewa kutoka katika laana.
D. KITABU KILICHOTIWA MHURI - Ufu. 5:1.
Lengo la 4: Eleza maana ya
kitabu hiki.
Kitabu hiki kina umuhimu sana kwa sbabu kina ufunuo wa Mungu kuhusiana
na mambo yatakayokabili dunia na mwanadamu katika siku zijazo. Kinaelezea jinsi watu watakavyohukumiwa,
ushindi wa Mungu juu ya Mungu na watu wake juu ya uovu. Kila muhuri unapovunjwa jambo hutokea.
E. YESU KRISTO MWANAKODOO
ANAYESIFIWA – 5:6-14
Lengo la 5: Eleza maana ya
Mwanakondoo aliyechinjwa.
(a) Kristo anaonekana kuwa ni Mwanakodnoo aliyechinjwa. Hii inaonyesha kujitoa kwake pale msalabani
(Kalvari) kwa ajili ya dhambi za watu.
Ni kitambulisho cha kustahili, nguvu, mamlaka na ushindi wa Yesu juu ya
msalaba.
(b) Pembe saba zinaonyesha nguvu na uwezo wa mtawala.
F. KUFUNGULIWA
KWA MIHURI SITA – 6:1-17.
Lengo
la 6: Taja vitu vinavyotokea baada ya kufungua mihuri sita.
Watu wengi wasioamini kuwa Kanisa litapitia katika dhiki kuu wanaamini
kuwa kufunguliwa kwa mihuri ni mwanzo wa dhiki kuu.
(a)Mhuri wa Kwanza- Mpanda farasi mweupe mwenye uta kinywani ni Mpinga
Kristo.
(b) Mhuri wa Pili - Farasi mwekundu anawakilisha vita na vifo vya kutisha.
(c) Mhuri wa Tatu - Farasi mweusi
unaonyesha njaa na ukame wa kutisha.
(d) Mhuri wa Nne - Farasi wa kijivu
akiwakilisha vita, njaa,tauni na hayawani
(e) Mhuri wa Tano - Watakatifu waliouawa wakiwa mbele ya Kiti cha Enzi.
(f) Mhuri wa Sita - Tetemeko kubwa
linalotikisa ulimwengu mzima.
MASWALI:
1. Je,
Wazee Ishirina na nne ni akina nani?
2. Taja
matukio yanayotokea kila muhuri unapofunguliwa. (Ufu. 6:1-17)
SOMO LA 10 (b): MATUKIO KATIKATI YA DHIKI KUU NA
KUENDELEA:
Lengo la 1: Eleza matukio – dhiki kuu hadi mbingu mpya.
(a) Kufungua mihuri saba na Baragumu saba miaka 3 na nusu ya kwanza.
(b) Vitasa saba katikka miaka 3 na nusu ya mwisho
(c) Ufufuo wa Watakatifu
(d) Utawala wa miaka 1,000
(e) Hukumu ya mbele ya Kiti Cheupe.
(f) Mbingu mpya na nchi mpya.
B. MALAIKA WANNE NA MALAIKA
ANAYETIA MUHURI – 7:1-3
Lengo la 2: Eleza sababu za
kutiwa muhuri wa 144,000.
Malaika wane wanazuia upepo , na kuidhuru nchi. Malaika mwingine anatokea kwa ajili ya
kuwatia muhuri watumishi wa Mungu. Lengo
la kutiwa muhuri 144,000 ni kuwapa ulinzi wakati wa hukumu inapotolewa majeshi
ya pepo waovu yasiwadhuru.
C. WATU 144,000 - 7:4.
Lengo la 3: Eleza ni akina nani
144,000 kutoka makabila kumi na mbili.
Hawa ni Wayahudi
watakaomwamini Kristo wakati dhiki kuu kutoka kabila 12 za Israeli. Muhuri vipajini pao ni kuonyesha kuwa ni mali
ya Mungu na watalindwa na Mungu kutokana nahukumu yake.
D. 144,000 –WATAMBULIWA – 7:5-8.
Lengo la 4:
Eleza sababu zinazofanya makabila mengine yameondolewa:
Majina ya Danieli na Efraimu hayamo katika orodha ya makabila ya
Israeli. Hii inawezekana kwa sababu
makabila haya yaliongoza taifa katika ibada za sanamu na uasi.
E. MKUTANO MKUBWA WA WALIOVAA
MAVAZI MEUPE - 7:9-17.
Lengo la 5: Eleza umuhimu wa watu hawa waliovaa nguo
nyeupe (Ufu.7)
Hawa ni watu walioamini wakati wa dhiki kuu. Wametoka katika kabila
duniani. Watanyakuliwa mwishoni mwa
dhiki kuu na kuhudhuria karamu ya Mwanakondoo.
Ukweli huu unaonyesha watu wataokolewa wakati wa dhiki kuu.
Wazee 24
|
Mkutano
Mkubwa
|
Wameketi
Vitini
|
Wamesimama
mbele ya Kiti cha Enzi cha Mungu
|
Wana Taji
|
Hawana
Taji
|
Wana
vinubi na vyelezo
|
Wameshika
matawi ya mitende.
|
F. MALAIKA ALIYE NA CHETEZO CHA DHAHABU – 8:3,4
Lengo la 6 : Eleza ni nani malaika mwenye chetezo.
Muhuri wa Saba unafunguliwa
kunakuwa na ukimya. Hapa haijulikani
maana y ake. Malaika aliye na chetezo ni Yesu Kristo kwa
sababu katika A/Kale , makuhani peke yao walifunikiza uvumba kuwaombea
watu. Katika A/Jipya Yesu Kristo ndiye
kuhani mkuu, mpatanishi kati ya Mungu na watu.
G. TARUMBETA SITA -
8:6-9:21
Lengo la 7: Eleza ni matukio gani yatakayotokea
wakati wa kupigwa tarumbeta Sita.
Tarumbeta ya 1 – Theluthi 1ya mimea ya nchi itateketea
Tarumbeta ya 2 –
Theluthi1 ya bahari kuwa damu na viumbe na meli Kuangamizwa
Tarumbeta ya 3 – Theluthi 1 ya mito na chemchemi zitatafurika na
watu wengi kufa.
Tarumbeta ya 4 – Theluthi 1 ya jua ikapigwa, na 1 ya Mwezi na 1
ya nyota ili Theluthi itiwe giza.
Tarumbea ya 5 – Majeshi ya pepo waovu kutesa watu wasio na mhuri
wa Mungu kwa miezi mitano.
Tarumbeta ya 6 – Mateka 4 walifunguliwa na kuwa theluthi 1 ya
watu.
Tarumbeta ya 7 - Sauti
kutoka mbinguni kuwa ufalme ni wa Mungu.
N.B: Licha ya
mateso yote haya watu wanakataa kutubu.
MASWALI:
- Taja matukio yanayotokea wakati wa baragumu saba.
- Je, 144,000 waliotajwa hapa ni akina nani?
- Kuna tofauti gani kati ya wazee 24 na mkutano mkubwa?
SOMO LA 11: MAENDELEO YA UNABII.
A. MALAIKA MWENYE NGUVU – 10:1-7
Lengo la 1 : Eleza ushahidi unaoweza kukusaidia kujua
huyu malaika ni nani.
Ushahidi unatuonyesha kuwa huyu malaika mwenye nguvu ni Yesu ni huu
ufuatao:-
(a) Mwonekano wake ni sawa na Yesu wa
Ufunuo - 1:13-15
(b) Kiapo chake anachoapa.Hakuna katika Biblia malaika aliyeapa.
(c) Sauti yake kama simba aungurumapo.Biblia ( Yoel. 3:16) inasema Bwana
anaunguruma kama simba( Hosea 11:10,11;Amosi 3:8) Usemi wa malaika “hapatakuwa
na wakati baada ya haya” (Ufu.10:6-7).
Una maana kuwa yale yaliyokusudiwa hukumu juu ya uovu lazima utekelezwe.
B. YOHANA ATUMWA KUTOA
UNABII - Ufu.10:8-11
Lengo la 2: Eleza maana ya Yohana kula kitabu kidogo.
Kitabu hicho alichokula Yohana kilikuwa na ujumbe uliokuwa unaeleza
kukamilisha kusudi la Mungu kwa watu duniani.
Kilielezea mambo yatakayotokea.
Kujua ujumbe kulikuwa kutamu kama asali, bali baadaye kulisababisha
uchungu ndani ya moyo wa Yohana. Hivyo
Mungu anamwagiza akahubiri ujumbe huo ili watakaomwamini wapate uzima wa milele
na wasioamini wapate kuhukumiwa.
C. MAELEZO ZAIDI KABLA YA
BARAGUMU YA SABA – Ufu.11:1-14
Lengo la 3: Eleza maana ya kupimwa kwa hekalu na
mahusiano yake ni miezi 42.
1.
Kulipima Hekalu –
11:1,2:
Kupimwa
kwa hekalu na madhabahu na kuhesabiwa kwa wanaoabudu kunamaanisha kuwa
E_Wayahudi watajenga hekalu lao.
Kutokana na Agano lao na mpinga Kristo watakuwa na uhuru wa
kuabudu. Katikati ya dhiki kuu mpinga
Kristo atavunja agano na kulinajisi hekalu.
Kipindi cha miezi 42 ambacho ni miaka 3 na nusu mji wa Yerusalemu
utakanyagwa na watu wa mataifa, mpinga Kristo atawatesa na kuwaua Wayahudi
waaminifu. Mwisho wa miaka 3 na nusu
utakamilisha mwisho wa kipindi cha mataifa.
2.
Mashahidi wawili - 11:3-14
Lengo la 4: Eleza kusudi la
Mashahidi wawili, uwezo wao, matokeo ya ushuhuda wao na ni akina nani.
Mashahidi wawili watatokea
ambao watahubiri Injili kwa uwezo mkubwa huku wakileta hukumu na mapigo kwa
wale wanaowapinga. Watahubiri
Injili kwa muda wa siku 1260. Baada ya kumaliza ushuhuda watauawa na mpinga
Kristo ambaye atakuwa amepona jeraha lake.
Miili yao italazwa mitaani na kushuhudiwa na watu kwa njia ya
Televisheni. Baada ya siku tatu, nusu
watafunguliwa na kupaa, matokeo yake kutakuwa na tetemeko kubwa la ardhi
litakaloua watu 7000.
Mashahidi wanadhaniwa na
wanatheolojia kuwa ni Henoko na Eliya kwa sababu hawakuonja mauti walitwaliwa
mbinguni.
Fundisho: Mtumishi wa
Mungu ataondolewa ikiwa amemaliza kazi.
D. KUPIGWA KWA BARAGUMU YA SABA
- 11:15-19
Lengo la 5: Eleza mkazo wa
baragumu lasaba.
Mkazo wa baragumu ya saba ni tangazo la kuwa falme za ulimwengu zimekuwa
ufalme wa Yesu Kristo. Pia inaonyesha
kuwa hukumu inakaribia kumalizika,
“kufunguliwa kwa Hekalu la Mungu mbinguni na sanduku la agano kuonekana
hekaluni mwake”, ina maa lengo la agano ambalo ni ahadi ya ufalme linakaribia
kutimizwa. Mungu anatunza ahadi ya neno
lake. Matetemeko ni dalili ya kuja kwa mwisho.
E. MWANAMKE NA
JOKA.
MWANAMKE ALIYEVIKWA JUA –
12:1-6,13-16.
Lengo la 6:Eleza na kumtambua huyu mwanamke aliyevikwa jua na elezea na
Kukimbia kwake:
Ishara 1: Mwanamke huyu ni taifa la
Israeli lenye makabila kumi na mbili ambamo Masihi kwake.
Ishara 2: Joka lenye vichwa saba na taji
maana yake ni shetani katika nguvu zake. Nyoka mbinguni ni malaika waasi
aliofukuzwa nao kutoka mbinguni. Mtoto aliyenyakuliwa ni Yesu Kristo aliyezaliwa
na kufufuliwa na kupaa kwenda mbinguni.
Naye atatawala mataifa.Mwanamke alikimbia maana yake katikati ya dhiki
kuu Israeli wanakimbia kutoka Utawala wa mateso ya mpinga Kristo . Israeli atakimbilia Perza huko katika nchi Ya
Yordan, na kuhifadhiwa kwa muda wa miaka 3 na nusu. Hawa Waisraeli ni Uzao utakaosumbuliwa (Ufu.
12:13-17)
MASWALI:
- Ni ushahidi gani unaotuonyesha kuwa huyu malaika ni Yesu Kristo?
(a) ________________________
(b) ________________________
(c) ________________________
- Nini matokeo ya ujumbe wa mashahidi wawili (11:3-14)
- Baragumu ya saba inaashiria nini?
- Taja ishara zilizomo katika Ufu. 12:12.
SEHEMU YA 4: MWISHO WA SIKU ZA MWISHO
SOMO LA 12: JOKA NA
VIBARAKA VYAKE.
1.JOKA 12:3-4.
Lengo la 1: Mtambue joka na
shughuli zake.
Huyu anajulikana kama shetani, joka la zamani la Ibilisi. Majina yana maana gani?:-
(a) Joka la zamani – mdanganyifu – Mwa. 3:1-13
(b) Ibilisi - Mjaribu, mwenye hila, mpingaji – Mt.
4:1; Efe. 6:11;
(c) Shetani - mshitaki – 1Pet 5:8; Zek 3:1
2. VITA MBINGUNI - Ufu. 12:7-12; 17:7-18
Lengo la 2: Eleza vita hivyo mbinguni.
Wakati wa dhiki kuu hakutakuwa na mapambano ya kiroho duniani tu , bali
hata mbinguni kutakuwa na vita mbinguni.
Shetani na malaika zake watapigana na Mungu na malaika. Shetani atatupwa chini na kutoruhusiwa mbinguni.
Akiwa na hasira na akijua ana muda mchache
anafanya vita na Waisraeli
waaminifu walioko Israeli wanashindwa na kutetewa na Mungu. Hivyo anawaudhi mabaki wa uzao ambao Wayahudi waliotawanyika
duniani waliomwamini Yesu Kristo.
A. MNYAMA ALIYETOKA BAHARINI –
13:1-10
Lengo la 3: Elezea asili yake, chanzo cha nguvu za
mnyama.
Huyu mnyama ni mtumishi wa shetani, ni mwanadamu aliyetoka katika watu
wa dunia. Baadhi ya wanatheolojia
wanasema ni falme saba ambazo zimesumbua taifa la Israeli yaani-Misri, Syria,
Babeli, Uajemi, Ugriki na Rumi. Pembe
kumi ni viongozi kumi watakaotawala pamoja na mpinga Kristo kwa muda mfupi.
Atatawala kwa nguvu na mamlaka kwa muda wa miezi 42. atakapofufuka au
kupona jeraha lake atataka watu wote wamwabudu.
Atawatesa na kuwaua watakatifu wengi.
Kutokana na uwezo aliopewa shetani atawaunganisha watu kupigana na
Mungu.
B. NABII WA UONGO - 13:11 -18
Lengo la 4 : Elezea kuhusiana na mnyama wa pili.
Huyu mnyama anaonekana kama mwana-kondoo, lakini anasema kama joka. Hii ina maana atajidai mpole, mwenye upendo
na kujali , lakini tabia yake ni ya kishetani.
Huyu ataanzisha kanisa la uongo ambalo litamwabudu mpinga Kristo. Atafanya miujiza minngi na kuwafanya
watu wamwabudu mpinga Kristo. Watauwawa
wale watakaopinga amri hiyo na kuwa waaminifu kwa Yesu Kristo.
C. NAMBA, JINA NA ALAMA YAKE –
13:16-18
Lengo la 5: Jadili alama ya mnyama na umuhimu wake.
Ili kuwadhibiti
wamwabudu mpinga Kristo atatumia silaha ya kiuchumi. Wote wanaotaka kununua na kuuza wawe na namba
au jina la mpinga Kristo pajini pa uso au mkononi. Hivyo namba hiyo itawafanya watu wamkubali au
wampinge mpinga Kristo – wasomi wengi wanahangaika kutafuta jina la mpinga
Kristo lakini wanapingana.
D. KAHABA MKUU - 17:1-6
Lengo la 6: Elezea kweli mbili
kuhusu kahaba na mambo yake katika siku ya mwisho.
Huyu kahaba anawakilisha dini zote za uongo. Katika Biblia kahaba ni mtu anayemwasi Mungu
na kuabudu miungu mingine. Hivyo kahaba
huyu ataikana Imani na Injili ya Yesu Kristo. Hili ni kanisa la uongo litakalomsaidia Kristo
kupata madaraka. Litashiriki katika
kuwatesa watakatifu. Dini na siasa
itatumika kutawala mataifa. Baadaye
mwishoni mpinga kristo atalichukia hili kanisa la uongo. Hivyo ataiangamiza tasisi hii.
E. UNABII
WA SIKU ZA MWISHO - Dan. 9:24
Mambo
sita yatakayokamilishwa katika majuma sabini ni:-
1.
Kumaliza makosa
2.
Kukomesha dhambi
3.
Kusamehe uovu
4.
Kuleta haki ya milele
5.
Kutia muhuri maono na unabii
6.
Kupaka mafuta mahali patakatifu kabisa.
1. MWANAKONDOO NA 144,000 – 14:1-5
Lengo la 7: Zitambue kweli kuhusiana na utambulisho na
tabia za 144,000:
Hali ya 144,000 ni wasafi kiroho, wamekombolewa kutoka duniani
wameandikwa vipajini mwao jina la Baba na wanamfuata Bwana.Hawa ni watakatifu
ambao hawakujinajisi na uchafu wa dhambi na ibada ya mpinga Kristo wala
hawajawahi kusema uongo.Hawa ndio watakao uimba wimbo wa Mwanakondoo.Watakuwa
wamechaguliwa miongoni mwa watakatifu walionyakuliwa kwenda mbinguni kabla ya
dhiki kuu.
2. TANGAZO LA
MALAIKA WATATU – 14:6-13
Lengo la 8: Jadili kwa kifupi
yaliyomo katika matangazo ya malaika watatu.
(a) Malaika wa kwanza anawataka watu wote duniani wamche Mungu kwa sababu
saa ya hukumu imefika.
(b) Malaika wa pili, anatangaza kuanguka kwa Babeli – yaani mifumo ya siasa,
dini na uchumi ya dunia imefika kikomo.
(c) Malaika wa tatu, anawaonya watu wanaokubali kupokea chapa watateswa
katika ziwa la moto milele.
(d) Wale watakaokufa katika Bwana watakuwa heri , kwani watapumzika taabu
zao (mateso na kwenda kwa Bwana).
3. MAVUNO YA DUNIA - 14:14-20
Lengo la 9: Eleza mahusiano ya
mavuno na shinikizo la divai.
Mavuno haya yanahusiana na hukumu.
Mavuno ya zabibu ni dunia na shinikizo la divai linahusiana na ghadhabu
ya hukumu ya Mungu, itakayowafikia wakazi wa dunia. Ni umwagikaji wa damu wa kutisha.
MASWALI:
- Nini maana ya majina haya:
(a) Joka la zamani ________________________
(b) Ibilisi ________________________________
(c) Shetani ______________________________
- Mpina Kristo atakapotoka atafanya nini?
- Nabii wa uongo atamsaidiaje mpinga Kristo?
- Kahaba mkuu ni nani?
- Namba ya mnyama 666 itatumikaje?
- Nini tabia za 144,000 walio pamoja na mwanakondoo? (Uf. 14:1-5)
SOMO LA 13: MATUKIO YA MWISHO WA
DHIKI KUU:
A. MAANDALIZI YA VITASA SABA.
1.
ISHARA KUU YA TATU
–Ufu. 15:1-8
Lengo la 1: Itambue ishara kuu ya
tatu. Eleza umuhimu wake.
Ishara kuu inayotolewa hapa
ni ya malaika wenye vitasa saba ambayo ni mapigo ya mwisho. Ishara mbili zingine ni: Mwanamke aliyevikwa
jua (Ufu.12:1) na Joka kubwa jekundu lenye pembe kumi na vichwa saba (Ufu.
12:3). Ishara kuu ya tatu ni ya muhimu
kwa sababu inahitimisha hasira na hukumu ya Mungu.
2.
KUMWAGWA
KWA VITASA VYA GHADHABU YA MUNGU – 16:1-21
Lengo la 2: Eleza vitasa saba vinawakilisha nini na athari juu ya
wanadhamu:
Kitasa 1: Madonda mabaya
na ya kuumiza yawapata wanadamu walio na Alama ya mpinga Kristo.
Kitasa 2: Viumbe hai vyote
baharini vinakufa.
Kitasa 3: Mito na
chimchemi za maji zageuka damu
Kitasa 4: Jua likawaunguza
wanadamu
Kitasa 5: Giza kubwa juu
ya utawala wa mpinga Kristo
Kitasa 6: Vita vya
Harmagedonia.
Kitasa 7: Ngurumo na
tetemeko Babeli na miji ya mataifa yaangushwa. Visiwa na milima ikatoweka, mvua
ya mawe kubwa ilinyesha.
Matokeo ya mapigo haya watu waliendelea na mioyo migumu na kumtukana
Mungu.
KAHABA MKUU – 17:1-18
Kahaba mkuu ni mji
ule mkuu ulio na mamlaka juu ya wafalme wote.
Hii itakuwa ni Kanisa la uongo ambalo litakuwa na nguvu ya ushawishi kwa
viongozi mbalimbali duniani, katika miaka 3 na nusu ya mwanzo ya dhiki kuu
itamsaidia mpinga Kristo ili kupata madaraka.
Lakini mpinga Kristo atakapopata nguvu na kufufuka au kupona jeraha lake
atafanya hila ya kumwangamiza. Wakati wa kipindi cha miaka 3 na nusu ya
mwisho mpinga Kristo atataka kuabudiwa na wote.
Hili kanisa la uongo litashiriki katika kuwaua watakatifu
watakaopingana naye.
B. PEMBE KUMI - 17:10-15
Lengo la 3: Elezea juu ya pembe kumi:
Mstari
wa 10 unazungumzia wafalme saba, watano wameanguka na mmoja bado. Watu wanaamini kuwa ni falme za Misri,
Ashuru, Babeli, Uajemi na Umedi, Ugriki iliyokuwa bado kuanguka ni Rumi. Wa saba
unakuja ni jumuiya ya mataifa kumi.
Mpinga Kristo atakuwa ni mfalme wa nane.
Pembe kumi ni mataifa kumi yenye nguvu za kisiasa na watamsaidia mpinga
Kristo na kupingana na Yesu Kristo.
C. KUANGUKA KWA BABELI NA MIFUMO YA
KISIASA NA KIUCHUMI:
HUKUMU YA
BABELI - 18:1-24
1.
Mji wa kisiasa na kiuchumu wa Babeli unatafsiriwa
na wasomo kuwa unawezekana ni mji halisi ambao ni makao makuu ya mpinga
Kristo. Pia unafikiriwa kuwa ni mfumo wa
kisiasa na kiuchumi wa mwanadamu.
2.
Maangamizi ya Babeli yanaonyesha kuanguka mifumo ya
kisiasa na kiuchumi iliyotokea katika historia yote ya mwanadamu kama
tulivyosoma katika Dan. 2 na 7, lazima mifumo ya falme za dunia hii
kubatilishwa na kuondolewa ili ufalme wa Kristo uje.
3.
Mungu ndiye suluhisho la matatizo yote ya kijamii
na kiuchumi ambayo yamesababishwa na dhambi ya mwanadamu.
4.
Mifumo ya kidunia na mpinga Kristo wataangamizwa.
D. KUJA MARA YA
PILI KWA YESU:
1.
SHUKRANI KWA AJILI YA
HUKUMU JUU YA BABELI.-Ufu. 19:1-5
Lengo la 4: Wataje wale wanaotoa
sifa kwa Mungu mbinguni na kiini cha sifa zao.
(a) Wale wanaotoa sifa na shukrani ni umati wa watu wengi, wazee ishirini na
nne na viumbe hai wane – Mungu anawatia moyo.
(b) Kiini cha sifa kwa wale wanaomsifu Mungu mbinguni ni>
(i)
Kuangusha uasi wa shetani na hukumu ya haki ya
Mungu
(ii)
Tabia na asili ya Mungu chanzo cha ukombozi.
(iii)
Kuanzishwa kwa ufalme wa Mungu katika historia ya
mwanadamu.
2.
HARUSI YA
MWANA-KONDOO – 19:6-10
Lengoo la 5: Elezea karamu ya harusi ya Mwanakondoo na vazi la Bibi
Harusi
Karamu ya Harusi ya
Mwanakondoo inatangazwa katika Maandiko, ila haielezwi kwa undani.
·
Ni wakati wa kuunganika kwa Yesu Kristo na watu
wake
·
Itafanyika katika wakati ambao Mungu amefanya
·
Wale tu walioalikwa watahudhuria Harusi hiyo, wale
waliookolewa.
·
Mavazi ya Bibi Harusi ni matendo mema ya watakatifu. Kukaa na kumtii Yesu Kristo.
3.
KUFUNULIWA
KWA MASIHI - 19:11-21
Lengo la 6: Elezea wajibu wa Masihi aliyepanda farasi mweupe.
Yesu Kristo ni wakala wa
ghadhabu ya Mungu na tumaini la waamini.
Yesu anamwaga hukumu juu ya waovu, lakini wakati huo ni chanzo cha
faraja na utukufu kwa watu wake wanaoshuhudia utawala wa haki. Yesu anakuja mara ya pili pamoja na
watakatifu wake. Anakuja akiwa mfalme wa
wafalme na Bwana wa Mabwana, Anakuja akiwa jemadari kuanzisha kweli na haki,
kuhukumu mataifa na kufanya vita dhidi ya uovu.
·
Kuwatawala kwa fimbo ya chuma – maana yake
kuwaangamiza mataifa.
·
Anakanyaga shinikizo la mvinyo – maana yake hukumu
ya kutisha.
KARAMU YA MUNGU - 19:17-18
Lengo la 7: Elezea karamu ya
Mungu.
Hii ina mahusiano
na vita ya Har-Magedonia, Mungu atawaangamiza watu waovu wengi wakati wa vita
hivyo kiasi kwamba watahitajiwa ndege wala nyama wengi ili kusafisha uwanja wa
vita. Hii ni kwa sababu itakuwa vigumu
kuzika watu.
HUKUMU YA MPINGA KRISTO NA NABII WA UONGO – 19:19-21
Lengo la 8: Elezea hukumu ya wanyama wawili waovu.
1.
Mpinga Kristo atakusanya majeshi yake ili apigane
na Bwana Yesu na majeshi yake.
2.
Majeshi ya mpinga Kristo yatashindwa vibaya, mpinga
Kristo na Nabii wa uongo watatekwa na kutupwa ziwa la moto.
3.
Majeshi au watu waliopigana wakiongozwa na mpinga
Kristo waliuawa.
MASWALI:
- Taja matukio yanayotokea wakati wa vitasa saba
- Kuanguka kwa Babeli kuna maanisha nini?
- Nani watakuwepo katika karamu ya Harusi ya Mwana kondoo?
- Nini hatma ya mwisho ya mpinga Kristo na nabii wa uongo?
SOMO
LA 14: UFALME WA KRISTO WA MIAKA ELFU NA
ULIMWENGU UJAO:
A. MIAKA ELFU:
1.
KUFUNGWA
KWA SHETANI – 20:1-3
Lengo la 1: Orodhesha mojawapo ya
hali ya kiroho itakayokuwepo wakati
Wa miaka elfu. Kwa nini kutakuwa na
mafanikio?
Mojawapo ya hali ya kiroho ambayo itakuwepo wakati wa utawala wa miaka
elfu ni ya kutokuwepo kwa udanganyifu hapa duniani. Hii ni kutokana na kufungwa kwa shetani huko
kuzimu kwa kipindi chote cha miaka elfu.
2.
UFUFUO
WA KWANZA – 20:4-6
Lengo la 2: Taja watakaohusika
katika ufufuo wa kwanza.
Kwanza kuna watakatifu
watakaofufuliwa kabla ya dhiki kuu. Pili
ni kundi la waamini watakaofufuliwa baada ya dhiki kuu ili kutawala pamoja na
Kristo. Hawa ndio walioteswa na kuuawa
wakati wa dhiki kuu. Watashiriki katika
kutawala pamoja na Kristo.
3.
MAONI MBALI
MBALI KUHUSIANA NA MILLENIA:
Lengo la 3: Eleza maana ya Millenia na kueleza maoni mbali mbali.
Neno Millenia linatokana na
lugha ya Kilatini likiwa na maana ya miaka 1,000. Sasa kuna maoni mbali mbali
kuhusiana na millennia , nayo ni:-
(a)
Post Millenialism - Yesu atakuja wakati
ulimwengu umejiandaa Kumpokea
(b)
Amillenialism -
Hakutakuwa ufalme wa miaka elfu wakati wa kurudi kwa Yesu mara ya pili.
(c) Premillenialism -
Ulimwengu utakabiliwa na utawala wa Masihi- Yesu wa kipindi cha miaka elfu
wakati Yesu atakaporudi mara ya pili
(Ufu.20) unasema kurudi kwa Yesu mara ya
pili kutafuatiwa na kufungwa kwa shetani
kuzimu na ufufuo wa wenye haki ambao watatawala pamoja na Kristo kwa muda wa miaka elfu.
4. HALI
KATIKA UTAWALA WA MIAKA ELFU:
Lengo la 4: Eleza hali na maisha yatakayokuwepo wakati wa millennia.
Mambo haya yatakuwepo katika
kipindi hiki:-
(a) Amani duniani pote hapatakuwepo na vita wala jujifunza vita (Zab. 46:9;
Isa. 2:4; 9:6-7; Mika 4:3-4)
(b) Maendeleo makubwa ya kiuchumi – (Isa. 65:21-24; Amo.9:13-15; Mika 4:4-5)
(c) Haki itatawala (Isa. 11:13-15; Yer. 23:5)
(d) Watu wote watamjua Bwana (Isa.11:9; Habak.2:14; Zek.8:21-23)
(e) Wanyama waondolewa ukali, watakula majani (Isa. 11:6-9; 65:25)
(f) Nchi itarudishwa hali yake ya kwanza na kuzaa sana (Isa. 35:1,2; Amo.
9:13-15; Eze.36:8-12)
(g) Maisha marefu (Isa.65:20-22)
(h) Mabadiliko ya dunia ya kupokea mwanga wa jua na Mwezi (Isa.30:26)
Lengo la 5: Taja wakazi wa ufalme
wa miaka elfu.
Kutakuwa na aina mbili ya watu: Kwanza watakatifu
waliokuja na Yesu ambao watatawala pamoja na Kristo. Pili, ni watu wenye miili hii ya kawaida
ambao walikuwa waaminifu wakati wa dhiki kuu na wale watakaozaliwa wakati wa
miaka elfu . (Mt. 25).
B. BAADA YA MIAKA ELFU.
1.
UASI WA MWISHO WA SHETANI - Ufu. 20:7-10
Lengo la 6: Eleza sababu za
shetani kufunguliwa na matokeo yake.
Shetani atafunguliwa kutoka
gerezani baada ya miaka elfu ili awajaribu watu waliozaliwa wakati wa
millennia. Hii itawkuwa nafasi yao ya
kuchagua kumtii mungu au shetani. Watu
wengi watamfuata shetani na kuizingira kambi ya watakatifu. Kabla ya kuishambulia kambi, moto utashuka kutoka mbinguni na kuwangamiza.
Shetani atatupwa katika ziwa la moto.
HUKUMU YA MWISHO MBELE YA KITI CHEUPE- 20:11-15
Lengo la 7: Eleza kweli kuhusiana
na hukumu ya mwisho.
Katika wakati huu watu wote waovu watafufuliwa na kusimama mbele ya kiti
cheupe ili kuhukumiwa.
(a) Mtu asiyeandikwa jina katika kitabu cha Uzima atahukumiwa.
(b) Wote waliomkataa Yesu na wokovu wake watatupa katika ziwa la moto wa
milele
(c) Mauti na kuzimu zilitupwa katika ziwa la moto.
Jehanam ni moto mkali usiozimika kamwe, tanuru la moto ambako watu
watasaga meno na kuomboleza. Pia hii
ndio mauti ya pili (Mt. 22:13; 25:30; 13:42,50; Mk. 9:43)
C. MPANGO MPYA - Ufu. 21-22
1.
MBINGU MPYA NA NCHI MPYA – Ufu. 21.
Lengo la 8: Eleza maana hasa ya mbingu mpya na nchi mpya.
Kulingana na somo hili ina
maana ya kuwa mbingu na nchi ya sasa zitaondolewa. Baada ya kuja mbingu mpya na nchi mpya (Isa.
51:6; 2Pet.3:7,10-12). Nchi ya sasa
inaondolewa kwa sababu imechakazwa na kunajisiwa na dhambi. Nchi mpya haina bahari.
2.
YERUSALEMU
MPYA – 21:2-22:5
Lengo la 9: Eleza jinsi mji ulivyo:
(a) Mji huu unaitwa ni Bibi Harusi kwa sababu Mungu atakaa pamoja na watu
wake.
(b) Mji una milango 12 ambayo inawakilisha taifa la Israeli. Pia una misingi 12 ambayo inawakilisha
kanisa. Hii ni kuonyesha umoja wa
watakatifu wa A/Kale na A/Jipya.
(c) Mji ni mraba wenye mapana, marefu na wimo sawa wa maili 1,500. Ukionyesha kuwa utakuwa na makao ya kutosha
ya watakatifu wote wa vizazi vyote. Pia
mji unajawa na utukufu na utakatifu wa Mungu.
(d) Mji hauna hekalu kwa sababu Mungu na Mwanakondoo ndio hekalu lake.
(e) Hakuna usiku katika mji huo
(f) Barabara zake ni za dhahabu.
(g) Kulingana na Wanatheolojia, mji huu utakaliwa na watakatifu wote kabla
ya dhiki kuu.- yaani walionyakuliwa kabla ya dhiki kuu na wale watakaofufuliwa
baada ya dhiki kuu.
(h) Nchi mpya itakaliwa na watu wote ambao waliishi katika ufalme wa miaka
elfu na walimkataa ibilisi na ushawishi wote. Inasemekana watakuwa mataifa
wanaongozwa na wafalme. Wafalme hao
wataenda Yerusalemu kumtukuza Mungu kwa yale anayofanya katika nchi mpya (Ufu.
21:24-26)
(i) Wakazi wa mji wa Yerusalemu ni washindi waliovumilia taabu na adha mbali
mbali
(j)
Hawa hawataingia katika nchi hiyo:
§ Waoga ambao wanaogopa kumkiri
na kumfuata Yesu Kristo Aliye hai (Mk. 8:35; 1Thess. 2:4)
§ Wasioamini – hawa ni pamoja na wakristo ambao wameanguka dhambini.
§ Waamini wote wanaosema wanamfuata Yesu, lakini wanaishi katika dhambi
(1Kor. 6:9,10; Efe. 5:5-7; Gal. 5:19-21)
§ Hawa wote watatupwa katika ziwa la moto
(k) Watakatifu watamwona uso wake –
hili ndilo lengo la historia ya ukombozi.
Watamwona Yesu Mwanakondoo kwani wataishi naye. (Mt. 5:8; 1Yh. 3:2)
(l) Mti wa Uzima ambao ni halisi unaonyesha mfano wa Roho Mtakatifu na
Uzima, baraka na nguvu za kiroho zitokazo kwa Mungu. (Isa. 44:3; Yn. 7:37-39)
D. HITIMISHO - 22:6-21
Lengo la 10: Eleza mambo muhimu yaliyomo katika Hitimisho;
1.
Anathibitisha kuwa unabii huu ni wa kweli kwa sababu umetolewa na Bwana
wa roho za Manabii ambaye aliwaongoza Manabii kunena
2.
Yesu anasema anakuja upesi na amebarikiwa yule
atakayezingatia Unabii huu.
3.
Kila mtu
atapokea kulingana alivyotenda hapa duniani.
4.
Baraka ni kwa wale wanaoshika amri zake ambao
watapewa haki ya kuuendea mti wa uzima na kuingia mji wa Yerusalemu mpya.
5.
Watu waovu wanaosema uongo na wauaji watatupwa
katika ziwa la moto wa milele
6.
Roho Mtakatifu na Bibi Harusi (Kanisa) wanafanya
kazi ya kuwaalika watu kupokea Neno la wokovu.
7.
Kuna hukumu juu ya watu ambao wanachagua sehemu
Fulani na kuziacha zingine katika unabii huu.
Hivyo hivyo kwa wale wanaongezea mawazo yao juu ya Neno.
8.
Yohana anaitikia kuwa uje Bwana hii inamaanisha:
(a) Wakristo wa kweli wanaomba na wanahamu ya kurudi kwa Bwana kwani ndipo
ukombozi wetu utakamilika.
(b) Siku ya kurudi Yesu imekaribia ambapo atarudi katika utukufu wake.
Je, mpendwa uko tayari kunyakuliwa?
MASWALI:
- Taja matukio mbali mbali yatakayotokea kabla ya Yesu Kristo kutawala?
- Eleza maana ya millennia kuhusiana na maoni ya:
(a) Post millennialism _______________________
(b) Amillennialism __________________________
(c) Premillennialism ________________________
- Mambo gani yatakuwepo wakati wa utawala wa Kristo wa miaka elfu moja?
- Jehanam ni nini?
- Eleza kwa kifupi kuhusiana na mbingu mpya na nchi mpya.
Maoni 3 :
bwana yesu asifiwe! ubarikiwe sana kwa kazi nzuri ya kutusaidia kuelewa kitabu cha DANIELI na UFUNUO.ila nina swali,kuna sehemu umesema katika yale majuma 70 israeli watafanya agano na mpinga kristo ila ufafanuzi kutoka DANIELI 9:26-27 inaeleza kwamba yesu kristo ndiye atakayefanya agano na watu wengi sio ISRAELI NA MPINGA KRISTO!ZAIDI ATAKOMESHA SADAKA NA DHABIHU,MAANA YAKE YESU KRISTO KAMA KUHANI MKUU WA HEKALU LA MBINGUNI KUPITIA DAMU YAKE ILIYOMWAGIKA MSALABANI NA KUSULUBIWA KWAKE ANAKOMESHA SADAKA ZA MAFAHARI NA WANYAMA WENGINE ZILIZOTOLEWA NA WANA ISRAELI KWA AJILI YA ONDOLEO LA DHAMBI, NA YEYE KUWA MPATANISHI MKUU KATI YA WANADAMU NA MUNGU SAWA NA 1timotheo 2:5. sasa sijaelewa maelezo uliyoyatoa kuhusu israeli na mpinga mkristo,naomba ufafanue hapo!
Kiukweli somo lako liko vizuri ila hujafafanua kuhusu Yale madini yalioandikwa ktk kitabu cha ufunuo21:18-20,Lakini nikiri wazi wewe ni mwalimu mzuri mno tens mwenye viwango vikubwa sana
Waebrania 4:12
Chapisha Maoni