Naitwa Salome Shemazua mkazi wa
Pongwe Jijini Tanga nina umri wa kati ya miaka 35, ni mshichana mwenye umbo
zuri la kibantu ambalo linaweza kumvutia mwanaume yeyote mwenye akili timamu na
mwenye kupenda wanawake wenye uasilia yaani wale wasiopenda wanawake vimbaumbau
wale wanaoijifanya eti wana menteini na kukondesha vipaja vyao kaa kuku wa
kisasa, mimi ni kibonge bwana umbo nambari nane lakini hata hivyo sijaolewa.
Hiyo sio shida kwani wote tunajua kuwa kuolewa nako ni majaliwa.
Tanga mkonge Hotel
Hata hivyo katika kubangaiza hapa
na pale katika shughuli za maisha nilitokea kupendwa na baba mmoja hivi wa makamo
sikuwa na muda hata wa kuuliza umri wake
ingawa alionekana kama angeweza kunizaa na huenda pia ningeweza kuwa
mwanae wa pili au watatu hivi, nilikutana na baba huyu pale Texas motel moja ya
baa maarufu hapa Pongwe, baba huyu aliyekuwa anafanya kazi saruji kiwanda cha
simenti kilichopo karibu na mji wa Pongwe alitupa ndoana yake kwangu nami bila ya fedheha sikuwa na hapana nilimkubalia, wenyeji wangu walikwisha kunipa
stori kuwa wanaume wa saruji wana pesa kama njugu kutokana na mishahara mizuri
wanayolipwa na kiwanda hicho ambacho huchangia mapato ya kutosha katika jiji la
Tanga niliona nami nimepata wangu wa kumchuna, Nilijitahidi sana kumpagawisha
baba Yule kimapenzi kama unavyojua hapa Tanga waja leo waondoka leo nilimpagawisha na mambo ya kipwani,
nilijituma hasa nikijua kuwa hii ndio nafasi ya kumfanya baba huyu ajikite
kwangu na kumsahau bi mkubwa, hasa
ukichukulia kuwa Alisha mwaga malalamiko kibao kuhusu bi mkubwa kuwa hajitumi
na ni mshamba na kuwa hata kimaumbile mimi nimemzidi bi mkubwa kwa kila idara
alidai mzee huyu kuwa bi mkubwa huyo ni kafupi na kamekomaa na ukikaona ni kuwa
hata mkononi hakajai sikujua kwanini sasa alimuoa au alilazimishwa lakini
niliona vyovyote iwavyo shuhuda hizi zinanipa ujasiri wa kujituma kuliko, na kumuonyesha
kuwa na sisi wenye maumbile ya kibantu mchezoni nasi hatujambo nikijipindua
hivi na vile kuonyesha manjonjo kwa
ujumla nilifanikiwa sana kumroga Baba Yule wa bara huko, hapa simaanishi
maswala ya kishirikina namaanisha jinsi nilivyofanikiwa kumfisadi kimapenzi
baba Yule,
Kujituma
kwangu hakukuwa bure kwani alinihamisha kwenye nyumba ya kupanga na kunijengea
kajumba kangu kazuri maeneo ya Ambangulu kwa wale wanaoijua Pongwe kule Tanga,
nilijengewa kajumba potabo kwani kana vyumba vitatu na kila kitu ndani yaani
selfu konteini niliendelea kujidekeza na
kupewa kila kitu nilichokitaka ingawa
nilimsikia Buzi wangu akilalamika kuwa ana maswala ya Ada ya watoto na kuwa na
majukumu mengine huko kwa bi mkubwa, mi sikujali kwani niliendeleza ufisadi
wangu bila kujali kuwa kuna kafamilia kanaumia
ingawa kaubinadamu kanaponijia
huwa najiuliza je ningelifanyiwa miye ingekuwaje? Lakini Mapepo ya
ukatili yaliponivaa sikujali nilijitia moyo acha huyo bi mkubwa akome, Mungu
ametuleta duniani tukomeshe wanawake wachovu wasiojituma kwa nini amtese baba
wa watu ? mtu unapata bahati ya kuolewa halafu uinaichezea kweli upele anapewa
asiye na kucha nilijitia moyo kuhalalisha upashikuna wangu na ufisadi kiwembe
na nilitiwa moyo kwani wanawake wengi pale Pongwe hizo ndo issue zetu wengi ni
nyumba ndogo.
Siku moja iliyopelekea kuelezea
kisa hiki kama waswahili wasemavyo
“Mwizi zake arobaini” au za mwizi arubaini, Nilipatana na mzee wangu
Yule kwamba tukatese huko maeneo ya
Raskazone njia ya kwenda hospital kuu ya Mkoa bombo karibu na daraja upande wa
kulia ambako kuna hotel moja maarufu siku hizi nyuma kidogo ya shule ya
sekondari ya mkwakwani sipendi kutaja jina la hoteli hiyo kwa maslahi ya mwenye
hoteli hata hivyo kwa wenyeji wa Tanga watakuwa wamenipata vilivyo lakini hata
kabla ya kwenda hoteli, Bwanangu Yule aliniambia nitangulie mjini na kupitia
saluni kisha yeye angenipitia akitokea Saruji anakoishi akiwa na usafiri wake, Nilitangulia na rafiki
zangu kadhaa waliokuwa wakienda mjini nao kwenye mishemishe zao tuliingia
saluni moja karibu na stendi kuu ya mji wa Tanga katika barabara maarufu kama
Taifa rodi, saluni hii inapendwa na watu wengi sana hususani wakiwemo wale
wanaotokea Pongwe hasa kwa sababu ya utaalamu wao pia wa kusuka rasta, na pia
kuandaa maharusi, kama iliyo ada tulikutana na wanawake wengine kadhaa wengine
wakihudumiwa na wengine wakisubiri, tulipofikia hatua ya kuhudumiwa kama unavyojua mambo ya umbeya wa saluni
tulianza na mada mbalimbali za kisiasa, umbeya udaku na mengineyo kedekede na
baadaye ilikuja mada ya uchunaji mabuzi, hapo ndipo nilipodakia kama
nimefikishwa kwani mimi sio mzuri sana kwenye maswala ya siasa za Tanzania
nilizichoka kwani niliona kama tunazugwa tu
hivyo sikuwa na interesti na siasa tangu alipostaafu Mkapa na hata
kufatilia Bunge nilifuatilia alipohutubia Kikwete ile hutuba yake ya bungeni ya
kwanza kabisa, kwa hiyo eneo hili utafikiri nilipewa maiki nilieleza kuwa
kuchuna mabuzi kunalipa, kulikuwa na mama mmoja mfupi aliyeonekana kama
amekomaa hivi alionekana kupinga mada ya maswala ya waume za watu na kuonya
kuwa inatesa sana wale walioolewa. Nilimkatisha mama huyo na kuanza kumsomesha
kama mtoa mada mkuu huku nikiungwa mkono kwa herufi kubwa mada hii ilinigusa utafikiri
ndio mwenyekiti wa kamati Fulani huko Bungeni
nilionyesha faida kadhaa za kufaidika kutokana na kuchuna mabuzi, huku
nikitamba juu ya kajumba nilikojengewa
na aina ya simu maarufu kama blakiberi niliyonunuliwa na buzi na
nilionyesha wazi jinsi wanaume wa saruji wanavyojua kuhonga na kuwa hata pale
saluni buzi wangu atanipitia kwenda kutesa maeneo ya Rasikazone na kuwa atalipa
hata hela ya gharama yote ya pale saluni, nilitoa mada siku hiyo utafikiri
kungwi wa kicheni pati niliwaponda sana wanawake wachovu na kueleza pia kuwa
buzi wangu anasema kuwa ka mwanamke kake kamekondeana na kukomaa kama nyigu na
kuwa hata kwenye mkono hakajai hakana intateiniment na kwa mkwara mkubwa wakati
mwingine niliwasiliana naye kumuulizia hani kuwa yuko wapi na mbona anachelewa
ili mradi tu kuwapagawisha wanasaluni pale, Mama Yule kimbaumbau aliyekuwa na nywele nzuri sana nyingi lakini
kanyimwa nyama mwenye uso uliionekana kama ana mapito hivi kama wasemavyo watu
wa dini Fulani ambao hujidai wanaimani kali,
alinyamaza kimya kama amelowa maji, nilimwaga sera na hatimaye
alionekana kuunga mkono kama mbunge aliyepotea kutoka kambi ya upinzani, hilo
lilinipa kichwa na kujiona kama ninatawala saluni kwa muda wana saluni wenyewe
walikuwa bize kutushughulikia wakiwa kimya
na wengi walikuwa wakinisikiliza jinsi nilivyojimwaga na kumkandia mke
mwenza ambaye nilikuwa simfahamu. Mwisho ikawa kama wote tumeshughulikiwa na
wengine walikaa vitini kwaajili ya kuhudumiwa.
Niliinua simu yangu aina ya
blakiberi niliyohongwa na kumjulisha dalingi wangu kuwa niko tayari na kuwa aje
alipe tuondoke, kwa kawaida anaijua saluni hiyo kwani hiyo haikuwa mara ya
kwanza, lakini kwa vile siku ile nilijimwaga sana kila mmoja alikuwa na hamu ya
kumuona huyo buzi ni wa aina gani, alikuja mzee Yule na gari yake ya kifahari
aina ya mark tu saluni grandi alipoteremka
aliingia mojakwamoja saluni na
nilimkimbilia kwa busu na mdeko wa nguvu “hai hani karibu umekuja nchukua
eh njoo basi hani unlipie kisha ndo tuondoke”, jambo la kushangaza siku ile ni
kuwa baba Yule katika hali isiyokuwa kawaida yake alikuwa kama ananitaaliza, au
kunishushua kwa lugha za kitanga, Busu langu la siku ile lilikuwa pia
limechanganyika na ishara ya kuwaonyesha kuwa huyu nitakayembusu ndiye kama
vile alivyofanya mtume mmoja wa Bwana Yesu aliyeitwa Yuda Iskariote, lakini
kama nilivyokugusia awali mwitikio wa shuga dady Yule ulikuwa kama amepigwa
ganzi na ghafla mama Yule kimbaumbau alisimama kama afande na kuanza kuteremsha matusi mazito sana yakielekea kwa baba Yule huku akilalamika kuwa watoto wamefukuzwa ada
wameshindwa kwenda shule, nyumbani tunashindia dagaa na maharage tu kumbe wewe
unajengea Malaya zako, kila mmoja alikuwa anashangaa na idadi ya watu ilianza
kuongezeka pale saluni matusi yalimwagika kama mvua na hatimaye nikageukiwa
miye na yalimwagikia upande wangu na nilipojaribu kujibu huku nikiwa nashangaa
nilipokea mkong’oto mkali nikiambiwa Malaya wewe firauni mkubwa nikiambiwa
ukome wewe kuchukua waume za watu nilishangaa mama huyu niliyekuwa naye saluni
inakuwaje ana mamlaka kubwa kiasi hiki ndipo akili ilianza kunijia kuwa huku
ndio kufumaniwa, Viungo vilinilegea kipondo kile kilipelekea kuchaniwa nguo kiasi cha kuwa uchi, watu niliokuwa nao saluni
walianza kupata majibu kuwa kumbe mwenye mali halisi alikuwa ni mwanamke Yule nilizomewa
kama paka mwizi, ilikuwa ni aibu ya mwaka siwezi kusahau jamani umbeya wa saluni bwana kumbe nilikuwa
najimwaga kwa mwenye mali,wanaume za watu shoga nimekoma,unataka kujua
yaliishije we mbeya sana mijimacho ka chura mbona ulipoacha kunyonya maziwa ya
mamako mi sijakuuliza? Si uliacha bila kuambiwa sasa ulitaka niendelee kusumbua
nyumba za watu mkong’oto ule ulikuwa kama zile stori za betina na zena katika
magazeti ya sani zamani.kwa sasa nimeamua kujishughulisha na shughuli
ndogondogo za kibiashara, nimeachana na maisha ya kupenda dezo kumbe bure ni
gharama.
Na Rev. Innocent Kamote
Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni