Jumanne, 16 Februari 2016

Dunia inapokulazimisha uache tabia mbaya !


Ilikuwa mwaka 1973,nikiwa sekondari ya serikali,kidato cha pili. Na dhahama hilo lililtokea nikiwa likizo nyumbani Korogwe,Tanga.
Kipindi hicho mtoto kufaulu ililuwa jambo la ujiko sana..hata jamii ya kijijini kwetu ilikuwa ikiniheshimu sana.

                                                      Kufaulu shule za Kijijini lilikuwa jambo la kifahari

Wakati huo ndiyo naanza kubalehe,nilikuwa nampenda sana dada mmoja aliyekuwa akisoma darasa la saba. Shida ni kwamba alikuwa anabanwa sana na familia yake hivyo kuonana ilikuwa taabu ingawa naye alishakubali maombi yangu.

Siku moja ya Jumapili tulikutana kanisani na tulipotoka tukapanga mpango,ambapo aliniambia nimfuate nyumbani kwao usiku wa saa 8! Nalimwuliza kwa nini muda huo akajibu,kuwa kwao huchelewa kulala hadi saa 6 usiku,hivyo saa 8 wanakuwa wameshazama kwenye usingizi mzito.Nikakubaliana naye.

Kwangu kutoka haikuwa shida kwani nilikuwa naishi mabanda ya uani. Nilipofika kwao,nilijibanza karibu na mlango wa ua na ndipo nilipoona mlango wa ua ukifunguliwa taratibu,na mtoto akatoka. Ingawa kulikuwa na gizagiza nilitambua alikuwa amevaa khanga,nami nikamrukia na kumkumbatia kwa mahaba.Akanivuta ndani kwa fujo kidogo,badala ya mahaba,nikashangaa lakini nikahisi itakuwa ni sababu ya woga.

Aliniingiza uani kwao ambako hakukuwa na taa,lakini ghafla taa ziliwashwa! Nilistuka kwani niliona kuna kikundi cha watu pembeni. Halafu nilipomwangalia kwa makini yule niliyedhani ni yule binti,nilitamani kupiga yowe kwani alikuwa ni mama yake mzazi!

"Haya mkwe wangu sema utanipa mahari kiasi gani nikupe binti yangu"alisema mama yule. Nilipotazama kwa makini lile kundi pembeni,nilitamani ardhi ipasuke kwani alikuwa ni baba na mama yangu na kaka yangu mkubwa! Nikiwa nimeduwaa,nilijaribu kuangaza bila mafanikio nikimtafuta yule binti.. Kwanini hakuwepo sikupata majibu.

Lakini baba yangu alikuwa na majibu... Kwani alikuja na kunibana mbavu,akanidunda sana kama mbwa mwizi!ilibidi waliokuwepo pale kuingilia.. Kaka yangu mkubwa naye aliniwasha vibao hevi kama vitatu vya haraka. Nasema hevi maana niliona nyota nyingi sana!

Wakati huu yule binti aliletwa akaamriwa kulala chini,nami nilale chini. Hapo tulitandikwa sana bakora. Wakati huo majirani walishasikia zogo lile na walishajaa uani pale..Tulichapwa na tulilia kama watoto wanaonyonya!

Baada ya adhabu hiyo,baba alichukua tenga na mauchafu-chafu mengine ambayo naamini alikuwa ameyaandaa,akanifunga mwilini na kuniambia twende nyumbani. Wakati huo aliwaomba majirani wanizomee. Nilizomewa njia nzima na huku wengine wakinirushia mchanga! Walikuwa wakiimba "msomi malaya,msomi malaya"
Hadi nafikishwa nyumbani nilikuwa hoi. Kufika asubuhi habari ile ilishaenea karibu kijiji kizima. Kwa kweli nilijisikia fedheha sana.Bahati na likizo ilikuwa ndiyo inaishaisha.

Baadaye nilikuja kujua ni mdogo wa yule binti,ambaye walikuwa hawaelewani,alikuwa amejificha huku akisikiliza mpango wetu,na akaenda kumwambia mama yake,mpaka yakatokea hayo yaliyotokea..

Hata hivyo baada ya kuwa nimeanza kazi,yule binti alikuja kuwa mpenzi wangu.

Hakuna maoni: