Alhamisi, 11 Februari 2016

Mfululizo wa masomo yahusuyo Uongozi wa Kanisa 2



****************************************************************

                     Somo; Faida ya kuwa kiongozi wa kanisa.
        Wanafunzi wa Yesu waliitikia wito wa Mungu na wakawa tayari kuwaongoza kondoo,na wakawa tayari kuacha vyoote walivyokuwa navyo ili kutekeleza wito huo Hata hivyo waliuliza Tutapata nini Basi (Mathayo 19;27).Kila mmoja wetu angependa kuwa kiongozi wa kaniasa kama angefahamu faida za kuwa kiongozi wa kanisa kwa sababu hii somo letu la pili katika mfululizo wa masomo ya shule ya uongozi ni Faida za kuwa kiongozi wa kanisa,tutajifunza somo hili kwa kuzingatia vipengele vitatu vifuatavyo;-

                    *Gharama za kuwa kiongozi wa kanisa
                    *Kukwepa uongozi wa kanisa
                    *Faida za kuwa kiongozi wa kanisa

*Gharama za kuwa kiongozi wa kanisa
1.Gharama za kuchukua udhia,Mizigo na mateso ya kondoo.
Kuwa kiongozi wa kanisa  ni tofauti kabisa na kuwa kiongozi wa mataifa yaani  kuwa kiongozi wa serikali au shirika la umma au kampuni Fulani,mtu anapokuwa kiongozi katika shirika,au kampuni Fulani au serikalini uongozi huo kwa kawaida huambatana na maslahi Fulani heshima na marupurupu au maslahi makubwa na kupata raha au kustarehe zaidi,Uongozi wa kanisa ni tofauti kabisa,huu ni uongozi wa kitumishi ni kuwatumikia kondoo wa mungu kwa kuchukua udhia na mizigo yao na kukubali mateso ya aina yoyote ile nyakati za biblia mtu aliyekuwa kiongozi alikuwa akikabiliwa na kuuawa wakati wowote (1Timotheo 3;1…) Lengo la uongozi huu ni kurahisisha matatizo ya kondoo wa bwana ili waweze kuingia mbinguni.hivyo hatupaswi kutumaini maslahi yoyote hapa duniani isipokuwa kutazamia malipo yetu mbinguni,Yesu kristo alikuwa ni kiongozi atumikaye ,kiongozi wa kanisa naye anapaswa kutumika bila kutegemea faida za kidunia kama ilivyo kwa viongozi wa kawaida wa duniani (luka 22;24-27).Kuwa kiongozi wa kanisa ni kukubali kubeba mizigo ya watu na kuwafanya wapumzike (Mathayo 11;28) kubeba mizigo ni kubeba huzuni zao,na masumbufu ya aina yoyote ile ili waone raha katika safari yao ya kwenda mbinguni (Kutoka 18;21-22) ni kuwa kama mama au baba anaye beba mizigo na udhia wa watoto wanaohitaji malezi ni kama mtumwa anayebeba mzigo wa bwana wake ili yeye atembee kwa raha,kazi ya maongozi ya kiroho si kazi nyepesi ni nzito ina lawama huwezi kuwapendeza woote na hawawezi kuridhika na lolote utakalowafanyia, watakuteta, watasema kuwa huwajali, watakulalamikia na kukulaumu, watakupiga mawe na wakati mwingine watakukataa na itakupasa kuendelea kuwatumikia bila kujali haya yaliwapata wengi wa viongozi waliokuwa viongozi wakubwa akiwemo Musa (Hesabu 11;11-15;kumbukumbu 1;9-18).
     Kiongozi katika kanisa hapaswi kuwaza juu ya malipo ya kazi anayoifanya  ni viongozi wachache sana wa kanisa ndiyo watapaswa kutunzwa na kanisa kwa mapato ya kanisa hawa ni wale tu wanaokuwa wameacha shughuli nyingine ili wapate muda wa kulihudumia neno kama ilivyokuwa pia wakati wa kanisa la kwanza (Matendo 6;2-4). Ingawaje  hata Paulo na barnaba kwa kipindi Fulani ilibidi wafanye kazi  ili kupata mahitaji yao na ya wale waliokuwa wakiwaongoza (Matendo 20;33-35;!Thesalonike 2;9) mtume pauilo alifanya hivi ili kupata mahitaji ya wale aliokuwa akiwaongoza hivyo viongozi woote ambao wanamsaidia mchungaji inawalazimu kufanya kazi kama zile za kaisari ili kupata mahitaji yao na kukulisaidia kanisa aidha ni muhimu kukumbuka kuwa Paulo alifanya vile ili kutoa kielelezo kwa Wathesalonike ambao walikuwa hawataki kufanya kazi (2thersalonike 3;6-9).
2 Gharama za kujikana nafsi zaidi kwa ajili ya kondoo.
    Viwango vya mungu kwa kiongozi wa kanisa ni vya juu zaidi kuliko vile vya kondoo wa kawaida,yako mambo ambayo yatakuwa halali kwa kondoo wa kawaida kuyafanya lakini yasiwe halali kwa kiongozi wa kanisa kuyafanya, Kwa mfano nyakati za agano la kale ilikuwa ni halali kwa watu wa kawaida kunyoa nywele zao,Kurarua mavazi yao na kuomboleza walipopatwa na misiba (2samuel 1;11-12,ayubu 1;18-20). Hata hivyo kuhani au kiongozi  wa kanisa wa nyakati hizo yeye hakuruhusiwa  kufanya hivyo au kufanya mambo mengine kadhaa wa kadhaa ambayo wengine walikuwa wameruhusiwa kuyafanya (Walawi 21;10-15) Hata wanawe Haruni; Nadabu na Abihu walipokufa Haruni kiongozi wa kiroho hakuruhusiwa, kuomboleza,kuwazikana kunyoa nywele zake (Walawi 10;1-7) Kwa msingi huu kiongozi wa kiroho kwakweli anapaswa kujikana nafsi yake  kwa ajili ya wengine (Yohana 10;11;Marko 8;35)Wakati mwingine itakugharimu kuwa wa mwisho kuondoka kanisani wakati viongozi wengine wako majumbani (Mathayo 14;22-23)Wakati mwingine inaweza kukugharimu kutokwenda likizo endapo kufanya hivyo kunaonekana kutaathiri utendaji wa kazi ya Mungu.
 Kukwepa uongozi wa kanisa
   Baada ya kuwa tumefahamu  mzigo huu mkubwa wa kuwa kiongozi wa kanisa watu wengine waliookoka ,hutafuta visingizio mbalimbali vya kukwepa uongozi wa kanisa na kuona bora wawe kondoo wa kawaida katika kanisa (Kutoka 4;10;13;Yeremia 1;4-6) Hawa watakuwa ni watu wasiofahamu faida za milele zinazoambatana na kuwa kiongozi wa kanisa,hii ni sawa na mtoto anayetoroka shuleni kwa madai eti kuwa masomo ni magumu,mwanafunzi wa jinsi hii atakuwa hajui faida zinazoambatana na kusoma,mkulima  anayekubali taabu ya kilimo huwa wa kwanza kufurahia apatapo chakula tele,wale wanaokwepa mzigo wa kilimo  hupata shida baadaye .(2Timotheo2;6;Mithali 28;19).
Faida za kuwa kiongozi wa kanisa
   Isaya alipomwambia na Mungu  “MimI hapa nitume mimi” nakuanza  kufanya kazi ya Mungu kama kiongozi wa Kiroho,hatimaye alifikiri kuwa anajitaabisha bure na kutumia nguvu zake bure bila ya faida,lakini baadae akakumbuka faida au thawabu  zinazoambatana  na kuwa kiongozi wa kiroho hivyo aliendelea kumtumikia mungu  mpaka mwisho alipouawa kwa kukatwa misumeno (Isaya 49;4,Ebrania 11;37).sisi nasi ni muhimu kufahamu kuwa kuna faida za kuwa kiongozi wa kiroho katika kanisa na hili litatutia moyo kumtumikia Mungu kwa gharama yoyote Faida hizi ziko katika makundi makuu mawili
1. Faida za Duniani.
 Ziko ahadi nyingi za Mungu alizozitoa kwa kiongozi wa kiroho yeyote anayemtumikia Mungu ni wajibu wetu kumkumbusha Mungu wakati woote wa utumishi wetu (Isaya 43;26);-
  • Kuheshimiwa na Mungu(Yohana 12;26), Mungu anapokuheshimu hukupa kipaumbele
  • Kuna kula na kushiba (Kumbukumbu 11;13-15;Isaya 65;13).
  • Atabariki chakula chako na maji yako, atakuponya, hapatakuwa na aliyetasa wala mwenye kuharibu mimba na hesabu ya siku zako ataitimiza (Kutoka 23; 25-26).
  • Mungu atakuponya katika hatari yoyote kubwa itakayokuja au inayokukabili (Daniel 6;16,20-22)
  • Mungu atakuwa pamoja nawe katika kazi yote ya utumishi mpaka kazi yake itakapomalizika (1Nyakati 28;20).
2. Faida za Milele
  • Kung’aa kama nyota milele na milele (Daniel 12;3)
  • Atakuwa na daraja njema (1Timotheo 3;1,12-13 na Ufunuo 21;14)na katika utawala wa Kristo miaka elfu duniani watapewa utawala (Luka 19;15-19).
  • Kuna taji ya utukufu isiyokauka (1Petro 5;1-4)
  • Kuna taji isiyoharibika(1 Koritho 9;23-25)
  • Atakuwa miongoni mwa wale waliobarikiwa (Mathayo 25;34-40)
  • Atalipwa mshahara mkubwa mbinguni na kujaa furaha tele (Yohana 4;35-36).

Hakuna maoni: