Somo la Nne
Vijana na Tatizo la Upweke!
Upweke ni mojawapo ya tatizo kubwa sana la
mwanadamu Upweke kwa lugha ya kiingereza “ Isolation”
ni kutengwa mbali na wengine,ni uhalisi wa kuwa mwenyewe ni kutengwa na wengine,
It is a state of being isolated or sepatation from others,The fact of being
alone and separated from others. Tatizo hili kwa mujibu wa biblia lilijitokeza
mara tu baada ya kuumbwa Adamu hata kabla ya anguko la mwanadamu, Hivyo swala
la mwanadamu kutokupenda kuwa pekee ni la kimaumbile (Mwanzo 2;18).Upweke hushusha moyo,hukatisha tamaa huleta huzuni na
kufanya mtu asione umuhimu wa maisha,Ni kwa sababu hii Mungu alisema si vema
huyo mtu awe peke yake, na kwa kuwa vijana ni moja ya kundi linalotatizwa na
swala hili hapa mwandishi wetu atakuwa akidadavua namna ya kukabibliana na
tatizo hili, katika somo hili nitazungumzia maeneo makubwa matatu yafuatayo;-
- Tatizo la Upweke.
- Fundisho katika Upweke.
- Namna ya kukabiliana na tatizo la upweke.
Tatizo la Upweke!.
Kama
nilivyokwisha kugusia awali kuwa upweke ni moja ya matatizo yanayowakabili watu
wengi sana duniani wakiwemo zaidi vijana, Kadiri ulimwengu unavyoendelea ndivyo
na jinsi tatizo la upweke linavyozidi kukua duniani, Huko ulaya anaeleza Binti
mmoja wa kitanzania anayeishi nchini Ujerumani alipoulizwa kuwa angependa
kuishi ulaya baada ya kumaliza masomo yake? Binti huyu alisema kwa haraka
nitarudi nyumbani,na nisingependa kuishi ulaya,Sababu kuu aliyoitoa binti
huyu aliyekuwa akihojiwa na shirika la habari
la kiingereza BBC, alisema ni upweke! Alisema yeye hukutana na marafiki zake
akiwa shuleni tu na inapofika mwishoni mwa wiki “Weekend” anachokisikia ni
milio ya ndege tu,watu wengi huelekea kwenye majumba makubwa ya starehe na
mitaa huwa kimya,na unakuwa na wakati mgumu na unapopata japo barua pepe yani
E-mail kutoka kwa rafiki zangu wachache niliowaacha Tanzania ninakuwa kama
nimepata Dhahabu. Hii inatufundisha kuwa kumbe unaweza kuishi katika nchi
nzuri, jumba zuri au katika mazingira mazuri sana au hata katika Bustani kama
ilivyokuwa kwa Adamu pale Eden lakini
kama ukiwa mpweke maisha hayo yanakuwa hayana maana, kwa ajili ya upweke watu
wengine hufikia hatua hata ya kutaka kujiua kwa kukosa matumaini.
Wengi wanapoulizwa sababu ya upweke hutoa
sababu nyingi kati ya hizo kubwa zaidi ni hizi, Kukosa kazi, Maumbile ya upole
sana au aibu sana, kuchokozwa, Kukatishwa tamaa, Kutofikia malengo, Unyanyapaa,
Kujichukia, Hali ya kujiona duni, Kukataliwa na jamii, mazingira mume au
mchumba au jamaa na ndugu wa karibu, kutengwa, Kuugua, Kufungwa gerezani,
kufiwa na jamaa, ndugu mzazi au mtu uliyempenda sana, Talaka, kukosa hamu ya
moyo na kutokujisamehe baada ya kufanya dhambi.
Kwa ujumla kunaweza kukawepo sababu nyingi
zaidi ya hizi zinazopelekea watu kujihisi Upweke,upweke usipodhibitiwa unaweza
kusababisha misukumo mingiyenye madhara kwa vijana upweke unaweza kupelekea mtu
kujiingiza katika kufanya dhambi kwani upweke na dhambi ni jamaa walio karibu
sana ni mapacha yaani alipo upweke
dhambi naye hayuko mbali mtu anaweza hata kujiingiza katika ukahaba wa
kupindukia na sababu ikiwa ni upweke na watu wasijue ni kwanini,upweke unaweza
kukufanya utumie dawa za kulevya,upweke unaweza kukufanya uone kuwa kila mtu
anakuchukia,upweke unaweza kukufanya ujiuwe, na unaweza kukufanya uwe mlevi na
sababu kadhaa wa kadhaa nilipowahoji watu kadhaa waloopitia katika tatizo la
upweke kuwa walijisikiaje,hisia walizokabiliana nazo zilikuwa nini, haya ndiyo
majibu ya baadhi yao, Ahaa unakuwa hauna raha hata! unahisi hufai na unavunjika
moyo,Unahisi mambo ni mabaya tu,unakuwa hupendi watu unahisi watu hawakupendi
wala hawakujali, Unalala hovyo tu, au unakosa usingizi unahisi hovyo maumivu si
maumivu uchovu si uchovu, kazi huwa haziendi, unaweza usione umuhimu hata wa
kula, Uwezo wa kufikiri unapungua, unarudia mawazo yaleyale, unatamani
ukazurule,Unahisi heri ufe,Unaweza kuua,Unahisi hata Mungu hana msaada
unamlaumu Mungu, n.k.
Unaona Kama watu tena wengi wao ni wale
waliookoka wanaweza kuhisi matatizo kama hayo hapo juu basi ni lazima tukubali
kuwa upweke si tatizo la kupuuzia lazima tukubali kuwa tatizo hili ni baya si
wengine wanataka kujiuwa au kuuwa au kumlaani Mungu je ni jambo jepesi hili?
Kwa nini kuna upweke? Kwa nini huwa tunausikia upweke ni fundisho gani
tunalipata katika Upweke hilo sasa linatupa kutafakari kipengele kinachofuata
fundisho katika Upweke.
Fundisho
katika Upweke.
Ni muhimu kufahamu kuwa ingawa upweke ni
tatizo kubwa kiasi hiki bado ndani yake tunajifunza mambo mengi ya maana katika
maisha na ambayo ni muhimu kuyazingatia, Mtu mpweke ni kama kaa la moto
lililotengwa peke yake toka katika makaa mengine ya moto hivyo ni rahisi
kuzimika, hivyo mtu mpweke yumo hatarini zaidi, lakini upweke una kitu gani
Upweke unatufundisha mambo mengi na ya
muhimu yafuatayo miongoni mwa hayo ni;-
- Tunahitaji kuwa na ushirika na watu wengine wa Mungu (Mithali 18;1) Biblia inasema hivi “Ajitengaye na wenzake hutafuta matakwa yake Mweyewe,Hushindana na kila shauri jema”Ni muhimu kufahamu kuwa Mungu hakutuumba kama kisiwa ili tuishi wenyewe tu tunahitajiana sanasana hivyo hatuwezi kukabili matatizo yetu wenyewe kila mmoja anahitaji ushirika wa mwingine, linapojitokeza tatizo hili ni wakati muhimu wa kurejea zile stadi za maisha na kujihoji kuwa tunahusiana vipi na wengine? Kwa nini kwa sababu wakati mwingine sisi wenyewe tunaweza kuwa ndio sababu ya hali tunayoipitia na kama hivyo ndivyo basi tujifunze kuwatafuta wengine wako wapi na tufanye ushirika nao (Filipi 2;1-4,Waebrania 10;24-25).
- Upweke unatufundisha kuwa tunahitaji ushirika na Mungu.
Ni
muhimu kufahamu kuwa upweke unaweza kukabiliwa vizuri kama una uhusiano mzuri
na Mungu, lazima tuuchunguze uhusiano wetu na Mungu kwani maisha ya dhambi
huweza kutufanya tuhisi upweke kwa sababu tumetengwa na Baba yetu wa
kimbinguni, Hivyo kama tumefanya dhambi uhusiano wetu na Mungu huingia dosari
na ni Budi kuungama na Kuutafuta Uso wake yeye
amesema hivi “Tazama mkono wa Bwana haukupunguka hata ashindwe kuokoa
wala sikio lake si zito hata lisiweze kusikia lakini maovu yenu yamewafarikisha
ninyi na Mungu wenu Na dhambi zenu zimeuficha uso wake Hata hataki kusikia” (Isaya 59;1-2).Mungu ametoa mwaliko wa
kukaribia kwake kwa toba (Isaya 1;18-19)
Adhabu kubwa na ya juu kabisa dunuani ni kutengwa na uso wa Mungu (Mwanzo 4;13-16).Kama unapitia hali za
namna hii fanya kama mwanampotevu zingatia moyoni mwako rudi kwa baba yako na
kwakuwa yeye ni mwema atakupokea (Ebrania
12;14,Mwanzo 3;8-10)
- Upweke unatufundisha kuacha Kiburi na ubinafsi ili tunyenyekeane.
Upweke unatufundisha kuwa hatuwezi sisi
wenyewe na hivyo tuwanyenyekee wenzetu na kuwatumikia, Biblia inasema atakaye
kuwa mkubwa kati yenu ni lazima awe kama yule atumikaye, tunapowatumikia
wengine watatunena vizuri na hivyo tutakuwa na furaha, tuwasalimu wengine na
kuwafanyia mema kila mwanadamu ni dhaifu hivyo tuchukuliane na kukubali
kuwaheshimu wengine yale ambayo tunataka kufanyiwa na wengine ni muhimu sisi
tukiwa wa kwanza katika kuyatimiza (Marko
10;43-45,Efeso 5;19-21)
Namna
ya kukabiliana na tatizo la Upweke!.
Sasa tumeona jinsi upweke ulivyo na mambo
Fulani ya msingi unaotufundisha unafundisha mambo mazuri sana ya muhimu lakini kama hatuyajui hayo bado
upweke unabaki kuwa tatizo kubwa sana na bado litatupasa kujua jinsi ya
kuukabili kama nilivyogusia kuwa upweke ni ndugu pacha na dhambi lazima tujifunze
namna ya kuutawala katika mtazamo chanya.
- Tumia Upweke Kama nafasi ya kukaa Na Mungu.
Kumbuka kuwa watu wengi ambao wametumiwa
na Mungu na hata kufanya ugunduzi mkubwa sana duniani na kuacha falsafa
mbalimbali duniani walikuwa wapweke sana, lakini moja ya njia iliyowafanya
kufanikiwa waliamua kuutumia upweke walionao kumtafakari Mungu.
Musa alikuwa mpweke
,alikataliwa na watu wake ,alifukuzwa na farao akitafutwa kuuawa alikwenda
mbali na nduguzake na kuchunga kondoo za mkwewe Ruthu jangwani aliutumia upweke
kuomba na kutafakari na haimaye kuona maono ya Mungu akimtaka akawatoe ndugu
zake katika utumwa mzito ni jambo la
kusha ngaza watu wanaweza kumkataa mtu lakini akawa mwenye kipawa kikubwa
chenye kuwafaa wengine! Kukataliwa si mwisho wa maisha yako angalia Biblia
inasema hivi “Musa huyo
waliyemkataa,wakisema ni nani aliyekuweka kuwa mkuu na mwamuzi?Ndiye aliyetumwa
na Mungu kuwa mkuu na mkombozi kwa mkono wa yule malaika aliyemtokea katika
kile kijiti” (Matendo 7;35-36). Muda haungeweza kutosha kukupa shuhuda za watu
walioishi maisha ya upweke na wakautumia upweke wao na Mungu na wakakamilisha
mambo makubwa duniani Daudi alikuwa maporini mara nyingi, Yusufu,Samsoni,
Yohana mbatizaji,Eliya n.k. lakini si hivyo tu bali hata viongozi wa dini
nyingine kama Islamu watakubali kuwa Muhamad alikuwa na tabia ya kukaa peke
yake jangwani akifunga na kuomba hata alipopata maono,Budha mwanzilishi wake
Gautama aliishi pekee porini akitafakari kweli kadhaa kuhusu maisha ikiwa ni
pamoja na kujiuliza kwa nini wanadamu wateseke na akaangaziwa kumbe kuutumia
upweke kutafakari mambo ya kiroho ni afya muhimu ya kiakili na kimwili, basi
wakati mwingine tunapokutana na magumu upweke ni dawa ya kutatua tatizo hili (Mwanzo 28;10-15,32;24)Yesu Kristo
aliuutumia muda wa upweke kutafakari na kuomba akiongozwa na Roho kumbe upweke
unaweza kuwa sababu ya nguvu nyingi za kiroho na udhihirisho wa karama na
utendaji wa R oho mtakatifu na kujifunza kuisikia sauti ya Mungu.
2. Usikawie kuoa,
upweke mwingine unaweza kudhibitiwa kwa kuamua kuoa au kuolewa
Ingawa ni wazi kuwa si wakati woote kuoa au kuolewa kunaondoa upweke lakini
Mungu alitibu tatizo la Adamu la upweke kwa kumpa Hawa (Mwanzo 24;62-67,26;8) Isaka alipata utulivu baada ya kuoa.
Kwa wale waliomwamini Mungu
kamwe hatupaswi kuishi kama watu wasio na matumaini (1Thesalonike 4;13-18) Kama watu wametukosea tumwachie bwana yeye
Ndiye alipaye kisasi dhidi ya waonevu wetu samehe usiwe na uadui na mtu,Tumia
upweke kuabudu kuomba,kutafakari kwenda kuwatembelea watu na kujadili maswala
nyeti kuhusu dini,siasa na taifa lako au kuuliza maswali ya muhimu kuhusu maisha
au mambo usiyoyajua,tumuombe Mungu aondoe kiburi na ubinafsi au tabia zozote
zinazotunyima marafiki , Tuache kujiona, Mabinti wa Lutu walifikia hatua ya
kuzaa na baba yao kwa sababu hawakuwa na majirani waliishi peke yao hawakuwa na
jamaa ya karibu ni naamini kuwa Mungu atakubadilisha ili utumie nafasi za
upweke Kwa faida na Si kwa hasara kama unapenda michezo shiriki michezo fanya
mazoezi jichanganye cheza hata bao au karata n.k hususani unapokuwa na muda wa
kufanya hivyo Endapo una Computer kuna michezo Games ambayo inaweza kukuchangamsha
akili Neema na amani na Upenda wa Bwana ukae nawe amen!.
Mwanafalsafa Plato ni moja ya
Wanafalsafa wakubwa sana Duniani (428-347 k.k.) alikuwa mbunifu na mwenye mvuto
sana katika Falsafa alikuwa mtaalamu wa fizikia,Siasa na hisabati,alizaliwa
huko Athene Ugiriki,Babaye aliitwa Arston toka katika familia za kifalme
alikufa mapema na hivyo mamaye aliolewa na baba wa kambo,Plato aliishi maisha ya
upweke alitamani kuwa mwana siasa lakini alikataliwa na viongozi wa kisiasa
wakimuona kuwa ni mzushi na kuwa hana mawazo sahihi bali muongo na
aliyekosea,alifuata falsafa za Socrates na alipofariki Socrates alikimbia
akiogopa kuuawa lakini baadaye alirudi Athene na kuanzisha chuo kikuu katika
taaluma za Sayansi, Fizikia, Hisabati na siasa ,Ni mtu anayeheshimika
ulimwenguni leo.Unaonaje angeamua kujiua? Hakukata tamaa wewe pia usikate tamaa
kwani Mungu amekupa kitu cha ziada!.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni