Ijumaa, 26 Februari 2016

Neema Juu ya Neema!



Yohana 1:16 “Kwa kuwa katika utimilifu wake sisi sote tulipokea Neema juu ya Neema”  Nyakati hizi tulizonazo ni nyakati ambazo kwazo, tunaweza kutumiwa na Mungu katika mazingira mbalimbali kwa viwango vya juu kutokana na kuweko kwa Neema au kuishi kipindi kiitwacho kipindi cha Neema, si rahisi sana kuelewa umuhimu wa neema mpaka imefafanuliwa kwako kwa kina na mapana na marefu.


Tunasoma hivi katika maandiko Matendo 4:33 Na mitume wakatoa ushuhuda wa kufufuka kwake Yesu  kwa nguvu nyingi na neema nyingi ikawa juu yao wote, Matendo 14:26 Na kutoka huko wakasafiri,kwe nda Antiokia, Huko ndiko walikoombewa neema ya Mungu kwa ile kazi waliyokwisha kuitimiza.  Kwa nini neema inaonekana kuwa ilikuwa kitu cha muhimu nyakati za kanisa la kwanza? Na kwanini nyakati hizi za leo tumeanza kupuuzia au kutokuwa na ujuzi wa umuhimu wa neema katika Maisha yetu na huduma.

Tutajifunza somo hili kwa kuzingatia vipengele vitatu vifuatavyo:

1.       Maana ya neema
2.       Neema juu ya Mashujaa wa Imani
3.       Umuhimu wa Neema katika maisha yetu na Huduma

Maana ya neema.
Neno Neema  maana yake ni wema wa Mungu suiopimika kumuelekea mwanadamu, au upendeleo wa Mungu pasipo kustahili, kwa maana nyingine ijapokuwa sisi ni wenye dhambi  na tunastahili hukumu ya Mungu, Mungu anatuangalia kwa Rehema na upendo na kutokutuhesabia kuwa ni wenye dhambi, hata hivyo Neema pia ni  uweza wa utendaji wa Mungu kwa mwanadamu aliyedhaifu, ni namna ambayo Mungu anakuwezesha kufanya mambo makubwa sana ya kutisha na kushangaza na watu wakafikiri kuwa umeyatenda wewe kwa uwezo na uhodari wako lakini kumbe nyuma yake Mungu anakuwezesha 2Thesalonike 2:16-17, Neema pia ni nguvu inayotuwezesha sio tu kukubaliwa na Mungu bali pia kupokea nguvu ya kuishi maisha yanayompendeza pasipokutumia akili yetu au nguvu zetu, kuchaguliwa kwetu kuwa miongoni mwaoa watakaourithi wokovu pia kunatokana na Neema ya Mungu Waefeso 2:8-9. Ni upendo wa Mungu unaotolewa Bure bila sababu au bila matendo ya kisheria ya kidini tunayoweza kufikiri kuwa yangelitupatia haki kwa Mungu, Waefeso 1:4-6 kwa hivyo kwa mtu aliyeokoka sio tu kuwa unapokea neema na upendeleo pasipokustahili lakini pia unawezeshwa kuishi maisha yanayompendeza Mungu na hivyo kutufanya sisi kuwa kiumbe kipya mbele za Mungu 2Wakoritho 5:17. Neema ya Mungu iko katika maisha yetu ya kila siku na utumishi wetu na hivyo tunapaswa kuiishi na kuitegemea Hata kwa wale wasiookoka bado wema huu wa Mungu upo juu yao na upendo huu lakini upendo huu ni wa kawaida kitaalamu unaitwa “Common Grace” Neema ya Kawaida , kwa wanaompokea Yesu kama Bwana na mwokozi wa Maisha yao inaitwa neema juu ya neema “Special Grace” Neema ya pekee au ya zaiada au maalumu Neema hii unapookoka unapaswa kuikulia kuendelea kuitumia katika mazingira mbalimbali 2Petro 3:18.

Neema juu ya Mashujaa waimani
Watu wote tunaowaona kuwa walikuwa mashujaa wa imani kamwe katika maandiko hawakuweza kuyafanya waliyoyafanya wenyewe bali uweza wa neema ya Mungu ulikuwa juu yao, wote tunafahamu kuwa Mungu alipomuagiza Musa aende Misri kuwadai Israel haikuwa kazi rahisi Kutoka 3:11-13,4:1-13, Misri ilikuwa ni tawala ya Dunia ya wakati ule ni taifa kali na katili chini ya utawala wa Farao utawala uliokuwa chini ya mamlaka ya kishetani na mapepo Farao mwenyewe alijipandisha katika daraja la uungu, kila taifa la dunia ya wakai ule walimuogopa, Kisha Mungu eti anamwambie Musa aende, Musa alijua wazi kuwa sio kazi nyepesi kama Mungu anavyotaka na alijaribu kuikwepa, ilikuwa ni kama anaelezwa ndoto na maruweruwe ambayo hayangekuja yawe na ukweli halisi kwa kujua hayo Musa alikiri wazi kutokuuuweza mzigo huo alitoa udhuru mara tano ambao bila shaka ulikuwa una uhalisia kabisa kuwa hawezi
1.       Kutoka 3:11 Mimi ni nani hata niende kwa farao?
2.       Kutoka 3:13 Wewe unayenituma Ni nani?
3.       Kutoka 4:1 hakuna mtu hata mmoja atakayeamini kuwa umenituma
4.       Kutoka 4:10 Mimi sio mnenaji mzuri hata kidogo
5.       Kutoka 4:13 tafadhali tuma mtu mwingine bhana,
Ukweli ni kuwa Musa alikuwa hawezi, lolote ni uweza wa Mungu tu na hahadi yake kuwa nitakuwa pamoja nawe ilimaanisha wazi kuwa Neema ya Mungu ilikuwa juu nya Musa na ndio iliyomuwezesha kufanya Haleluya! tuna Mungu wa ajabu sana kama tutaitegemea neema yake kumbe ndiyo inayotubeba katika mambo mengi tuyatendayo
Tunasoma katika Waamuzi 6:1-24 Jinsi Mungu alivyomuita Gideon ili akuwaamua Israel dhidi ya wamidian ni wazi kuwa katika binadamu waoga na dhaifu naweza kusema hakujawahi kuwako mtu muoga kama Gideon masimulizi ya Ndoto iliyompa ushindi Gideoni inaonyesha kuwa eti ni mkate wa ngano unaangusha hema za wamidian, Gideoni mwenyewe alitambua kuwa yeye ni mdogo sana na kabila yake ni ndogo sana  na alikuwa mwoga sana lakini pamoja na hayo Neema ya Mungu ilimfanya Gideon kuwa mtu wa tofauti.
Mtume Paulo na watumishi wengine  nyakati za kanisa la kwanza walifahamu sana umuhimu wa Neema hawakuwaacha watu waende hivihivi Matendo 15:40 waliwaombea neema, Kanisa la antiokia lilifahamu umuhimu wa neema kuwa hatuwezi kwa Nguvu zetu lakini Mungu akiwa pamoja nasi neema yake ikiwa juu yetu tutatenda mambo makuu sana , Paulo mtume alipitia dhiki na Mateso mengi na hatazri za aina nyingi ambazo zote zilikaribisha mauti karibu naye ni wazi kuwa kupona kwake katika kila aina ya mateso na mapito hakukutokana na uweza wa kawaida wa kibinadamu bali kulitokana na neema ya Mungu 2Wakoritho 11:22-33, Hata alipokuwa dhaifu na kumuomba Mungu amfungue majibu ya Mungu yalikuwa Neema yangu inakutosha 2Wakoritho 12:9 kumbe sasa tunaweza wote kuona umuhimu wa neema ya Mungu katika maisha yetu, kila aina ya mapito na majaribu na mateso tunayoyapitia tutaweza kuvumilia na kushinda tu endapo tutajikinga na kuitegemea neema ya Mungu.

Umuhimu wa Neema katika maisha yetu na Huduma.
Unaweza kuona sasa katika maisha yetu kadiri tunavyotembea na Mungu, siku hadi siku katika huduma zetu na maisha yetu ya kawaida tutakutana ma maswala na changamoto nyingine ngumu sana , hali za kukatisha tamaa na kuchoka, mapambano na matukio magumu, ili tusikate tamaa tunahitaji neema ya Mungu, ni neema pekee itakayotuwezesha kuishi na Mume, mgumu, bosi mgumu, mke mgumu, watu wagumu, wachokozi, wakorofi, wenye kutufuatafuata, wabishi, changamoto mbalimbali zote hizi zinatupasa, kuitumainia neema ya Mungu ili tuweze kustahimili na kuendelea kumtegemea Mungu, tunawezaje kuipata neema hii ni kwa kuomba na kumsihi Mungu atupe Waebrania 4:14, Mungu anaweza kutujaza kwa neema ili tuweze kuwa hodari katika kila tendo jema, kumbe hata kutenda kwetu vizuri kunategemea na jinsi tunavyojiachia katika neema 2Wakorotho 9:8 “Na Mungu aweza kuwajaza kila Neema kwa wingi, ili ….mpate kuzidi sana katika kile tendo jema!

Bwana ampe neema kila mmoja wetu kuishi kwa kuitegemea neema katika ulimwengu huu wa sasa katika jina la Yesu amen!
Na. Mtumwa asiye na faida
Rev. Innocent Kamote

Maoni 1 :

Unknown alisema ...

Mungu akubariki kwa fundisho zuri. Ninajengwa sana na mafundisho yako, na yamekuwa msaada sana katika huduma yangu.