Kabila ya wabondei ni miongoni
mwa makabila kadhaa ya wakazi wa Mkoa wa
Tanga, Makabila mengine ni Wazigua, wanguu, wakilindi, wasambaa, waluvu, ambao
kihistoria wana asili moja yaani waseuta kama nitakavyoelezea baadaye, Makabila
mengine yaishiyo mkoani Tanga ni wasegeju, wadigo na wadaiso ambao wao sio
waseuta na wenyeji kabisa wa inchi ya Tanga kihistoria ni Wambugu na wandorobo.
Waseuta ni kina nani?
Waseuta ni jina la umoja
linalowakilisha makabila ya mkoa wa Tanga ambayo asili yao ni moja, makabila
hayo ni wazigua, wanguu, wakilindi, wasambaa, waluvu na wabondei, wameitwa
hivyo kwa sababu ya kiongozi wao wa zamani (Mkale) aliyeitwa Seuta ambaye
alikuwa mtawala aliyewapigania na kuwalinda dhidi ya uvamizi wa wareno kabla
hawajatawanyika, kwa sasa makabila hayo hutambika tambiko lao kwa matwala huyo
au mtemi au chifu aliyeitwa Seuta.
Jina SEUTA ni muungano wa maneno
mawili ya kibondei SE – Baba na UTA- ni Upinde kwa hivyo Seuta ni “Baba wa
Upinde” wengine husema “mwana wa Upinde”, alizaliwa na Baba yake aliyeitwa Kuba
Kaluli (seuta Kaluli) ambaye pia alikuwa mzimu wa zamani sana, na mama yake
alikuwa binti wa kifalme aliyeitwa Musi au wengine walimuita Mchemno ambaye
kaka yake alikuwa mfalme aliyeitwa Sekalingo, Seuta alianza kutawala akiwa na
Umri wa miaka 12 alikuwa na akili za kupita kawaida mbunifu na pia alikuwa
Mganga, moja ya maswala ambayo anakumbukwa sana Seuta ni namna alivyoweza
kuwapiga Wareno kwa kutumia Upinde na Mishale na kuwauwa vibaya ingawa wao
walikuwa na Bunduki.
Seuta alizaliwa huko Kwediboma
katika tarafa ya Mgera wilayani Kilindi zamani Handeni umaarufu wake ulitokana
na akili zake za kupita kawaida za ubunifu wa kuwashinda wareno waliokuwa
wamekuja kuivamia inchi ya waseuta kwa kusudi la kuchimba madini na ili kupata
watu wa kuwachimbia madini waliwaonea wenyeji na kuwakamata kwa nguvu ili
wawachimbie madini watu walipogoma waliwaua na kuwachomea moto vijiji vyao
jambo hili lilimuudhi sana Seuta na waseuta kwa ujumla kwani ukandamizaji huu
wa Wareno haukukubalika.
Wareno walikuwa na ngome kubwa
huko Mombasa lakini walikuwa wakisambaa kutafuta mali waseuta walipanga vita
ambavyo vilipiganiwa katika eneo la Mto Ruvu, wareno walitumia Bunduki na
mizinga na vita hii iliwakalia vibaya waseuta kwani milio tu ya bunduki ilikuwa tishio kubwa kwao na hivyo walirudi
kwa kiongozi wao kutafuta ushauri, Seuta aliwashauri kuwa wanainchi waviache
vijiji vyao na kila kijiji wanachokiacha sehemu ambazo Wareno wangepita
wavichome moto na kuchafua maji, pia waharibu mashamba na vyakula kisha
wajifiche vita hivi vilijulikana kama vita vya kuvunja mawe ya kusagia chakula
“Nkondo ya kitula nyala” aliwambia
kila wanapoharibu watambike na kuvunja mawe ya kusagia, Wareno walipoona kuwa
askari wa Seuta wamekimbia waliendelea kuwafuatilia lakini walikuta maji yamechafuliwa, hakuna
chakula na watu wamekimbia hali hiyo
iliwashitua na wakakata tamaa kwa kuwafuatilia watu wasiowaona na pia njaa
ilikuwa ikiwatesa wakiwa wamechoka na
hofu ya njaa na magonjwa na silaha nzito
ndipo Seuta alipoamuru kuwanyeshea mvua za mishale na wareno wengi sana
na vibaraka wao walikufa na kuanza kukimbia wakirudi Mombasa wakiwa wameshindwa
vibaya na hivyo Seuta alipata sifa kubwa sana kama mtu aliyekataa ukandamizaji
na mwenye akili aliyekomesha kabisa uonevu na kuwashikisha Adabu na uganga wake uliaminika na watu walihofu
kuwavamia waseuta na Tangu kifo chake ndipo waseuta wote walipoanza kutambika
wakisema “Mtunga Katungile hale........Waseuta na Ugone.......”
Chimbuko la waseuta.
Kabla ya kuanza kuelezea kwa
maneno chimbuko la waseuta ni vema ukaangalia mti huu wa familia ya waseuta
ulikoanzia kwa umakini unaweza pia kuona katika Biblia kitabu cha Mwanzo 36;1- 4
ABRAHAMU
ISAKA
HETHI ESAU ARAMU
WAHITI
WA ARAMU
ADA BINT ELON MHITI
Basemathi BINT ISHMAEL
Muungano wa Wahiti na Waaramu
HITTIO-ARAMAIO
KANAANI-KAPADOKIA-ZAGROS
MAZIGULA WA UMBA WA HITTIO ARAMAIO
INCHI YA UMBA au VUMBA
WAZIGUA-WASEUTA
NCHI YA Nguu/Kilindi
Wanguu
Wazigua
Wakilindi Wasambaa Wabondei na
Waluvu
CHIMBUKO LA WASEUTA
Ni vigumu sana
kuzungumzia chimbuko la Wabondei pekee bila kuzungumzia waseuta wote kama
ulivyoona katika kielelezo hicho hapo juu wabondei ni sehemu ya waseuta na kwa
ujumla historia ya waseuta inaanzia mbali sana kama jinsi ambavyo umeona katika
mti huo wa familia na chimbuko la Waseuta hapo juu.
Waseuta ni
kabila ambalo asili yake ni Waaramu ambaye ndiye Baba yao mkuu. Aramu ambaye alikuwa ni mjukuu wa Nabii Nuhu,
Nuhu alimzaa Shemu, Hamu na Yafeth. Hamu akamzaa Kushi (Ethiopia) Misri na Putu
(Libya) na Kanaani, Shemu alimzaa Eberi ndiye Baba wa Waebrania na Elamu na
Ashuru na Arfaksadi na Ludi na Aramu;
unaweza kuona chanzo cha Aramu katika Mwanzo
10;6-23. Kwa hiyo waseuta kwa upande wa Baba ni Waaram (Aramaites) na kwa upande wa Mama
tunatokana na Esau mwana wa Isaka wa Ibrahimu, Esau alimuoa au alioa Binti wawili
wa kikanaani ambao walikuwa ni wana wa Hethi Muhiti na hivyo kupatikana muungano
wa wahiti na waaramu HITTIO-ARAMAIO
ambao nchi zao zilikuwa ni Kanaani, Kapadokia na baadaye Zagros katika milima
ya Armenia ya leo au kaskazini ya Iran ya leo ni wazi kabisa pia wazee wa
zamani katika matambiko yao wamekuwa wakitaja HITTIO! Au HETHIO wa SEUTA!
Ni wazi kabisa kuwa hii ilikuwa kabila ya zamani ya wahiti waliokaa Asia ndogo
katika Anatolia jimbo la Kapadokia na Kuwa Mwaka 262 K.K wahiti walifukuzwa na
wazungu waitwao Hansin a Sakson na ni katika wakati huo Hekalu la Diana huko
Efeso lilivunjwa. Hivyo inchi yao ya kwanza ni Kanaani au Israel maeneo ya Gaza
na Edom na hawa ndio waliompa Ibrahimu makaburi ya Makpela kwaajili ya kumzika
sara Wahiti ndilo kabila ambalo Esau mwana wa Isaka alikoolea Mwanzo 26;34-35.
Kundi la
kwanza la Waseuta ambao walikuwa wana asili ya waaramu na wahiti waliondoka
kanaani wakati wa Mashambulizi ya Nabii Yoshua aliyekuwa mrithi wa Nabii Musa,
Yoshua alikuwa na kampeni ya kuwaangamiza wakanaani na kwa kweli aliwamaliza
wengi sana na hivyo wengi wa wakanaani wakiwemo waamori, waharati, wayebusi na
wahiti walikimbia kabisa nchi zao na wengine walikuja Afrika hata hivyo wengi
wa waseuta walibaki salama katika nchi ya Edomu
kwa sababu Mungu alikuwa amemuamuru Yoshua kutokuangamiza uzao wa Esau kwa kuwa
ni ndugu wa Israel, wengi waliokuwa wakanaani wengine walikimbilia Afrika
Mashariki na kujenga miji kama Barawa, Lamu, Shungwaya, Malindi, Mombasa, Umba,
Pemba na Unguja, Tanga, Pangani, Saadani, Bagamoyo na Mzizima, Mafia, kilwa,
Mikindani mpaka maeneo ya Msumbiji, Angola, Kongo na Uganda wakati huu
inakisiwa ilikuwa miaka 1200 K.K. Hittio Aramaio walikaa juu ya Israel katika
inchi ijulikanayo kama Syria leo au Shamu na maeneo ya kusini Mashariki ya
Israel ndiyo Inchi ya Edom ng’ambo ya mto wa Yordan.
Kundi la Pili
la waseuta lilisonga mbele kuelekea Kapadokia nyakati za utawala wa Mfalme
Daudi ambaye aliwapiga wakanaani wakiwemo Washami, Waaramu, Waedomu na Wamoabu
na wadameski, sababu ya Daudi kuwapiga hawa ndugu zao ni kuwa walijiunga na
Wafalme wengine maadui wa Daudi ili
wampige, Hivyo Mfalme Daudi aliona ni vema kuvunja ile ahadi ya kutokuwapiga
ndugu zao Daudi akiwa na Jemadari aliyeitwa Yoabu waliwapiga vibaya kwa mfululizo wa vita miezi sita vipigo hivyo
viliwatia hofu na kuwafanya kutawanyika na kujificha mbali kama Misri, Paran,
Midian Uajemi na Uamedi na hivyo kutawanyika katika nchi za Washirazi (Waajemi).Baada
ya kufa kwake Daudi baadhi walirudi katika nchi yao lakini baadhi walibaki huko
juu katika milima iliyoitwa Zagros ambazo ni safu za milima katika inchi
iitwayo Armenia na Iran ya leo.
Nchi za Asili za Waseuta.
Kanaani/Israel
Hii ndio inchi
ya kwanza walioishi wahiti na baaada ya Esau kuoana na binti wa Kihiti waliishi
katika Inchi ya Edomu ambayo ilihusisha maeneo ya Syria na sehemu ya kusini ya
Israel yaani Gaza na Edomu ng’ambo ya mto wa Yordani Dameski ulikuwa mji wao wa
kwanza na baadaye walipanda juu Hata Antiokia ya Pisidia ndio Anatolia au jimbo
la Kapadokia
Kapadokia.
Hii ni inchi
ya pili ya waseuta ambapo waliishi katika jimbo hili huko Asia ndogo kwa mujibu
wa utafiti wa maswala ya uchimbaji wa mambo ya kale eneo ambalo wahiti hao
waliishi linaonyesha ushahidi kuwa walikuweko katika eneo hilo miaka 1340 kabla
ya Kristo Kama utakavyoona kwenye ramani chini eneo lililotiliwa Rangi ni eneo
ambalo jamii ya wahiti waliishi eneo hili linaweza kuchukua inchi za Syria na
Uturuki na ugiriki lakini nyakati za zamani hakukuwa na Ramani zilizoko leo
Nchi ya Anatolia Cappadokia Uturuki ya sasa ilikuwa nchi ya asili ya Waseuta zamani .
Ramani hii
inaonyesha jimbo la Anatolia au kapadokia zamani likithibitishwa na watafiti wa
mambo ya kale kuwa ni eneo lililokaliwa na wahiti miaka 1340 Kabla ya Kristo.
Zagros
Kutokana na
usumbufu Fulani walioupata toka kwa wazungu jamii hii ilikimbilia kwenye inchi
ya tatu na kuishi katika safu za mlima Zagros ambayo imesambaa kaskazini mwa
Irani ajemi na Armenia ya leo, Milima ya zagros imesambaa kuanzia kusini
magharibi ya Iran hata kusini mashariki ya Sirvan kati ya mto Dilaya na Mto
Shiraz wengi wa watu wanaoishi pemba na Zanzibar na visiwa vya commoro ni jami
ya watu walioishi huko Uajemi katika mto huu shiraz hii ndio asli yao. Safu ya
milima ya zagros ina urefu kati ya Km 900 au mail 550 urefu na upana wa mail
150 sawa na Km 240 eneo kubwa zaidi kwa leo ni Iran na ni kama inatengeneza mipaka
ya inchi ya Iran na mataifa mengine, ndani yake kuna vilima vyenye urefu kati
ya futi 12000 na mingine imefunikwa na barafu, maeneo haya yana rutuba na mito
yenye kutiririsha maji na hupata mvua zenye ujazo wa mill 40 mara kwa mara.
Tamaduni zinazofunika
maeneo haya ni zile tamaduni za zamani za ki- Mesopotamia na kiuajemi au kimedi
pia kwa sehemu kuna tamaduni za Kirumi wakazi wake wengi walikuwa ni Waashuru
wa Kikristo, Wakurd na waturuki na wengi walikuwa wafugaji na maeneo hayo pia
yanachimbwa mafuta katika sikuza leo, ni kwa sababu hiyo nchi za zamani za
Waseuta zinakuwa ni Kanaan-Kapadokia na Zagros, Jina hilo Zagros ndio asili ya
Jina Wazigua, kwani watu waliwaita Wazagros, Mazigulat, na baadaye wazigua.
Inchi
hii hapo juu ndio milima ya Zagros huko Uajemi na Armenia hii ndio inchi ya tatu
ya asili ya Hittio Aramaio Zagros
Juu
ni ramani ya Armenia ambayo kusini inapakana na Iran na Kusini magharibi
Uturuki na mashariki ni inchi nyinginezo zenye uhusiano na Urusi ya zamani hii
ndio inchi ya tatu ya Wahiti wa Kiaram walioishi katika milima ya Zagros.
Kwa hiyo kwa asili
inchi yao ilikuwa shamu au Syria na Yordani kwa mipaka ya nyakati hizo na
walijulikana kama Hethio - Aramaio kwa maana ya asili ya Kiaramu na asili ya
Esau aliyeoa mwanamke wa kihiti mji wao uliitwa Anatolia katika jimbo la
Kapadokia walipokuwa wamekimbilia Armenia katika safu za milima ya Zagros huko
shirazi au uajemi, Wagiriki waliwaita Zigra au Zagroth watu hawa baadaye
walikimbilia Afrika na kuingia kwa majahazi katika pembe ya Afrika inchi za
Somalia, Ethiopia, Sudani na Afrika Mashariki na kufika katika inchi ya Umba au
vumba kutokana na sababu mbalimbali na uonevu, inchi hii ilikuwa kati ya Lamu
na Tanga mpaka maeneo yanayouzunguka mto Umba, wengine waliteremkia Ethiopia na
Somalia katika maeneo ya shungwaya
na wasomali waliwaita Mashungula, Mzungu mmoja aliwaita Wasegua na wazungu wa
Kireno waliwaita Mozungullos kwa sababu walishindwa kutamka jina lao vema la
asili Mazigra au Mazagros au Mazigula hivyo kimsingi watu hawa sasa
walijulikana kama “Zigras – Hittio –
Aramaio” kwa msingi huo sasa jina Wazigua ni Kiswahili cha Neno Zigras au
Mazigulat, ushahidi wakitafiti unaonyesha kuwa wengine walikuja wakiwa na
majina ya kiasili ya huko Uajemi kwa mfano Kiongozi wao wa kwanza walipofika
Umba aliitwa CHAMBIKE WA VUMBA na alipokufa alitawala mwanawe aliyeitwa
MWANACHAMBI kisha Walifuata wanachambi wengine asili ya jina CHAMBIKE ni “CAMBYSES”
AU KAMBISESI ambaye alikuwa mtawala wa uajemi mwaka 528 K.K. ambaye ni mtawala
aliyefuata baada ya kufa kwa baba yake Mfalme KORESHI au Cyrus, Cambyses
alitawala uajemi yote ikiwemo Armenia kati ya miaka ya 600-559 karne sita kabla
ya kuzaliwa kwa Masihi alikuwa ni mwana wa Koreshi aliyepokea utawala wa Baba
yake Huko Kaskazini mwa Shushan Ngomeni huko Elam, alimuoa Bint wa mfalme
Astyages mmedi na kulingana na Mwanahistoria wa kigiriki Herodotus Cambyses
alimuoa bint wa Astyages ambaye kupitia yeye alimzaa mtoto aliyekuja kuwa
mfalme mkubwa baadaye na kuitwa Koreshi mkuu wa II.
Wazigua walikuja na jina Kilo wakimaanisha KORESHI jina hilo kilo linatumika hata leomiongoni
wa wazigua, ufalme huo wa Uajemi au ushirazi ulianza kati ya 546 - 446K.K. aidha
kwa kuwako kwao kusini mwa Israel ilikuwa ni rahisi kwao kufika katika inchi ya
Wafilisti katika ukanda wa Gaza na
wale waliokuwa na rangi ile ya asili wakati mwingine waliitwa Mgaza jina hili
Mgaza ni moja ya majina waliyokuja nayo kutokana na mji wa Gaza na katika jamii
hizi pia wako wanaoitwa CHAMBI.
Kwa msingi huo
niwazi kuwa asili ya Neno zigua ni Zagros au Zigras waingereza waliwaita watu hao Hethio au Hittets na Aramaio au waaramu
Aremeans kwa hiyo wazigua waliitwa majina hayo kutokana na asili yao au majina
ya inchi walizoishi kwa hiyo wao ni Waedomu au Waesau au Hethio – Aramaio
majina haya walipewa kabla ya kuja kujulikana kama Waseuta baadaye na kupata
matawi ya waseuta ambao ni wanguu, wazigua,waluvu, wabondei, wakilindi, pia
baadhi ya wazigua waliopotea ni wasonjo, walugulu, wakwere na baadhi ya wankodongo na baadhi ya wanyamwezi.
Alama kuu ya waseuta ni upinde na mshale
WASEUTA KATIKA NCHI MPYA YA NGUU AU HANDENI.
Nilieleza
mwanzoni kuwa Makundi ya Zigras – Hittio
– Aramaio wengi walikimbilia katika nchi iitwayo Umba ambayo iko kati ya
Lamu na Tanga, katika bahari ya Afrika Mashariki hii ndio nchi ya kwanza kwa waseuta kuifikia
walipotoka kanaani na Armenia hapa waliungana na wenyeji wengine na waswahili
na kukawa na ustaarabu mkubwa sana hata
hivyo eneo kubwa la nchi hiyo ya umba kwa sasa iko Kenya, Mahali hapo palikuwa
ni pazuri kwa uunganishaji wa miji ya Lamu, Mombasa, Pemba na unguja na hata
kilwa, watu kutoka Bara walikuja na Pembe za Tembo, Shaba, chuma na kadhalika na waliwauzia Waarabu, Wamisri, Wagiriki,
wachina na wazungu ambao wao walileta
shanga na nguo na sahani Biashara hizi zilikuwa na mvuto mkubwa sana na
ziliwavutia wazungu waliokuwa wakorofi yaani Wareno ambao kwanza walituma
wapelelezi kama Batholomayo Diaz na Vasco Dagama ambaye alifika Mombasa na
Malindi kati ya tarehe 7th
April 1498 na hakupata ushirikiano katika miji yote Isipokuwa Sultani wa
Malindi alimpatia viongozi wawili wa kumsaidia kufika Bara Hindi Mei 28th
1498 na hata ilipofika miaka 1500 B.K Wareno wengi walikuja Afrika ya Mashariki
wazungu hao walikuwa wakorofi na waliiharibu nchi kwa ugomvi na vita na kuwatoza watu kodi kubwa sana wengi wa
watu walianza kuwakimbia, Wareno walikuja Afrika mashariki na kusambaa mpaka
Msumbiji na Angola lakini walijenga makazi huko Mombasa katika mji wa Mvita
yaani mji wa vita wakajenga ngome kubwa
ya Askari iliyoitwa Ngome ya Yesu au (FORT JESUS) ambayo iko Hata leo haya
yalifanyika kati ya mwaka wa 1592-1598 ngome hii iko hata leo mjini Mombasa.
Ngome ya Yesu (Fort Jesus Mombasa) ilijengwa na wakoloni wa kireno mnamo
miaka ya 1590 kwaajili ya kulinda biashara zao na shauku ya kutawala eneo hilo
leo ni moja ya makumbusho ya kihistoria katika pwani ya Kenya, Mjini Mombasa
Kutokana na
ukatili wa Wareno wanaichi wengi wa Afrika Mashariki hawakuwapenda kabisa
wareno, Wareno walipigana na Mazigula ambao wao walikuwa ni kabila kubwa na
hawakupatana kabisa na wareno na hivyo
watu wa Umba walishindwa na na
wakasukumwa mbali wakiongozwa katika kukimbia kwao na walisaidiwa na wenyeji
Wambugu ambao hawakua na wivu na wageni hao walikimbia zaidi ka Km 1600 na
ndipo walipokimbia na kufika Nguu, kundi lingine lilikimbilia katika milima ya
pare mpaka inchi ya mlima mweupe yaani Kilimanjaro hawakukaa wakaendelea mpaka
Sonjo baadaye walirejea kwa kupitia Irangi Kondoa na kurudi katika inchi ya
Nguu na kukutana na wenzao kiongozi aliyewaongoza alikuwa Mmbugu aliyeitwa
Malando Bin Mbogo ambaye alikuwa mwenyeji wa Inchi na kiongozi mwingine aliitwa
Maita, Kundi lingine lilipotelea na kubakia katika maeneo ya Loliondo na maeneo
ya mlima wa Mungu Oldonyo Lengai na kubaki katika inchi ya Sonjo huko Masaini
na wakajiita wasonjo kwa sasa wameathiriwa na desturi za Kimasai lakini ni ndugu
zetu na hufanana na wazigua na hawaongei kizingua bali kisonjo.
Wazigua
awalipofika Nguu walikutana na makabila mengine ya watu waliokimbia vita na
kuchanganya Damu, kabila la kwanza kabisa kuchanganya Damu na Mazigula ni
Wagala hii ni kwasababu Hethio - Aramao waliwahi kukaa huko Ugala huko Kenya
wakitokea Ethiopia na Somalia walikokaa kwa Muda na hawa wagala wana Pua Ndefu
na ndivyo unavyoweza kuona baadhi ya wasonjo na hata baadhi a wazigua wana pua
ndefu, kabila zilizochanganyika na wazigua huko nguu ni pamoja na Wazorwi,
Washana toka Botswana,Walozi, waemba , wangoni, wachewa, Watonga na wanyasa na
kadhalika Hata hivyo tamaduni na Lugha ilikuwa ileile ya wazigua moja wa nyimbo
za wakale zinazothibitisha kuwa walichanganya Damu na wagala zinasema hivi “Msi na Mgalla Mwadungana Hahi? Mpula ya
Mgala kulengela!” yaani mwenye nchi na Mgala mlichanganyikia wapi? Na Pua
ya mgala imechongoka!.
Utawala wa
Kireno haukudumu kwani walitimuliwa na mataifa mengine ya ulaya na wakakimbilia
Angola na Msumbiji ingawa waliendeleza tabia yao ya vita na wenyeji, waarabu wa
Omani walitokea na kunyang’anya mamlaka yao yote, waarabu walitawala kwa amani
na kupatana na wenyeji na walistawi wakifanya Biashara wengi wa waarabu wana
asili ya Kiaram katika wakati huu wa Amani kulijitokeza kiongozi mmoja
aliyejiita mwanachambi akitaka kuendeleza utawala wa Mazigula katika inchi ya
Umba aliandika Barua na kuisambaza ili kuwataka wazigua wote kurudi katika
Inchi ya asili waliyofikia yaani Umba kwa hiyo kukaweko kusudi la kurejea Umba
na hapa ndipo ulipotokea Mgawanyiko mkubwa miongoni mwa Wazigua
Kundi la Kwanza.
Baada ya
kabila nyingi kusikia kuwa Wareno wamepigwa walirudi makwao lakini jamii ya Hittio
Aramaio Zigulats hawakuondoka lengo lao lilikuwa kurudi Umba, lakini kundi moja
lilikakataa kurudi Umba na kubaki katika inchi ya Nguu iliyoko huko Kilindi au
Handeni ya zamani, kumbuka Inchi ya Nguu pia ilikuwa ikiitwa Kilindi wao waliobaki
katika inchi hii waliitwa WANGUU,
mji mkuu wa Nguu ni SONGE kwa sasa ndio Wilaya ya kilindi, Tarafa zake ni Tatu
Kimbe, Mgera na Kwekivu.wanguu waliitwa hivyo kutokana na kilima kiitwacho
nguru au nguu baadhi ya wanguu hupatikana katika wilaya kama kilosa Morogoro
Mpwapwa na Kongwa huko Dodoma na hivyo
kuchanganyika na walugulu kwa kiasi hivyo walugulu wana asili ya uzigua Baadhi
ya hethio aramaio zigulat walibaki katika nchi ile ya Nguu na kuchukua nchi za
Wandorobo ambao walikuwa wenyeji wazigua walichukua inchi hizo na kwa utulivu
walianza kupanda mazao pamoja na kuwinda
wanyama kwa kuwa wengi walikuwa wawindaji waliwinda wanyama na kuzichanja nyama
na kuzianika na ndipo eneo lile waliloishi kwa uwindaji liliitwa “Chanika” yaani kuanika baadaye mfumo wa
maisha ulibadilika na walianza kuhamasishana kupanda mazao Handeni na ndipo
pakapatikana Jina HANDENI jamii kubwa ya hawa waliobaki hapa waliitwa kwa jina
la asili ZIGULATS au Mazigulats kutokana na jina la Kiyunani ZAGROS hao ndio wazigua hata sasa miji yao mikubwa
ni Kwamkono,Misima, kideleko, Chanika, Kwalukonge, kwediboma, kwedibangala kwa
seuta,kwa mgumi, Bomani n.k. Zumbe waliotawala zigua ni pamoja na Zumbe Mohamed
Mdoe ukoo anaotoka mkuu wa Wilaya mmoja
aitwaye Athmani Mdoe, Tarafa zao ni Chanika, Handeni, Magamba, Mazingara,
Kwamsisi, na Mgambo hata hivyo inchi za Uzigua nyingine ni pamoja na Pangani,
Bagamoyo, Mbwewe, Msata, Saadani, na miono huko walichanganyika na Wadoe na
Wakwere kwahiyo wakwere ni ndugu zetu walugulu huko Morogoro walitokana na ukoo
wa wazigua na mkale wao aliitwa Samwelugulu huyu alikuwa mzigua na ndiye baba
wa walugulu
Kundi la Pili
Katika inchi
ya Handeni kuna kilima ambacho kiliitwa Kilindi hili ndio jina la wilaya mpya a
kilindi kwa sasa iliyogawanywa tarehe 9/5/2002. Kilima hicho maarufu kiko
katika tarafa ya kwekivu, kundi la wazigua wengine walikwenda kuishi na wenyeji
wa Milima ya Usambaa na kusambaa katika milima yote ya Usambara na hivyo walibadili
jina la asili la wazigua na kujiita wasambaa,
inchi yao kwasasa ni Lushoto, Maramba, Muheza, Magoma, Korogwe, Mlola, Mtae na sehemu
za Upare wenyeji wao sasa wanaweza kuongea Kisambaa lakini wenyeji wao ni
Wambugu ndio wenye inchi.
Muonekano wa
mlima kilindi na mlima nguu mlima kilindi huonekana kama mtu aliyebeba mtoto
mgongoni na ukiwa umeuinamia mlima nguu na kuacha pengo linaloweza kupitwa
katikati hivi ndivyo unavyoonekana ukiwa chanika na kuutazama kwa upande wa
magharibi
Kundi la Tatu
Hawa ni kundi
la wazigua walioitwa wanguu hili ni kundi dogo ambalo baadaye liliamua kuhamia
Usambaa kiongozi wao akiwa MBEGA aliitwa Mbega kwa sababu Yeye alikuwa Bado ana
Rangi ya asili ya Esau alikuwa mwekundu kama mwarabu na hata baba yake Mbega
alikuwa na Rangi hiyo ya asili walipanda milimani na wakajulikana kama Wakilindi kwa hiyo wakilindi pia ni
waseuta wengi hawapendi kuitwa vinginevyo kwa sababu ya kujivunia Rangi yao,
Mbega kwa kuwa alikuwa Hodari na mwenye kuwinda wanyama kama Esau alikuwa na
Busara na alikuwa mwamuzi mzuri na mwenye maajabu kadhaa hivyo wasambaa
walimuomba awe mtawala na aliwatawala na wazao wake ndio kina Kimweri,
Zumbe Kimweri ndiye aliyekutana na
wazungu na makasisi wa CMS Dr.Krapf na Rebman
ambao walipitia Mombasa mwaka
1848 na kufika Vuga ya Usambaa na
kuonana na Zumbe Kimweri wa IV na walimsifu kwa uongozi wake, Bwana Rebman
alielekea Kilimanjaro na kuona mlima mweupe na ndiye aliyetoa taarifa ulaya
kuwa Afrika ina Mlima wenye Barafu kama kwao kwani wazungu walifikiri Joto lililoko
Afrika sio rahisi kukuta Jambo kama hilo,
Mazumbe Kimweri inaonekana walitawala kwa Muda mrefu kwani Zumbe
aliyekutana na Dr.Krapf alikuwa Kimweri wa IV aliyefariki mwaka 1860 Kimweri
alizaa sana watoto wengi na rangi za asili zilijitokeza hao ndio WAKILINDI . Dr. Krapf baada ya maongezi
na Kimweri alianzisha Dini Huko Tongwe akitokea Unguja kwa Sultani Said.
Kundi la nne
Katika makundi
yote lilikuweko kundi moja ambalo lilipania kurudi katika Inchi ya asili na
kufika Pwani yaani Umba lakini lilikumbana na vikwazo vingi sana zikiwemo vita
za wavamizi wapya kutoka Kenya ambao wao sio Hettio Aramaio hawa walikuwa
Wadaiso, wasegeju na wadigo pia kwa hofu ya wageni wengine walifika katika mji
wao mkuu wa zamani ulioitwa New Fort-Umba au umba mpya Ngomeni, waliishi maeneo
mbalimbali hata kufika Pwani kama Tanga ambayo iko chini ya umba ya zamani
ambako ni Horohoro mpaka sehemu za Kenya, Wazigua hawa walisambaa kutoka mji
mkuu wa zamani yaani Umba na sehemu za Mbwego, ambako huitwa Magila leo, pia
waliishi maeneo ya Mkuzi ambako kulikuwa na fundi maarufu wa kucheza njuga
aliyeitwa Saudimwe na mwanae Kidungwe, walisambaa sehemu za jaila ambako ndio
Misozwe leo, Bwembwera na tongwe, Makasisi Krapf na Rebman waliweka Msalaba
huko Hemvumo wakiwa wamepachagua kujenga kituo cha kazi za kimisheni walipokuwa
wakitokea Vuga kuomba Ruhusa ya Zumbe Kimweri wa IV na wakipita kutokea Unguja Hemvumo
au Msalabani ndio Magila, Askofu Frank Wetson alijenga shule kubwa kiwanda
kutoka hemvumo au Magila pia wazigua hawa wako sehemu za Amani hawa nao kama
wasambaa walibadili jina na Kujiita wabondei yaani “Valley Peoples” mji wao
mkuu kwa sasa ni Muheza jamii hii yawazigua ndio wenye ardhi njema zaidi kuliko
makundi mengineyo na ndio chimbuko la elimu na Uanglican wa High church katika
mkoa wa Tanga.
Kundi la Tano
Hawa ni
wazigua walioamua kuishi kando ya Mto Ruvu au Mto Pangani, wakati wazigua
wakisogea mbele kuelekea inchi nyinginezo kama Sambaa na Bonde hawa waligundua
mto ambao wazungu waliuita River na wao waliuita Ruvu hawa walifanya shauri la
kujenga kandokando ya mto huu na wengine
waliishi katika visiwa vidogo vya mto huo na kuvuka kwa kutumia mti ulioitwa
Ulalo au Vilalo kwa kizigua ili kuwawezesha kufanya shughuli kutwa nzima na
usiku walirudi kisiwani na kuondoa ulalo ili maadui wasiwapate kwa sababu ya kuishi miaka mingi kando ya mto
huu na kujifunza kuvua samaki wakaitwa waruvu
au waluvu kwa sababu hiyo sasa
Wanguu, wakilindi, Wazigua, waruvu, wasambaa na wabondei ni kabila moja la
waseuta wenye asili ya “Hethio Aramaio
Zagros” lakini hivi ndivyo inchi zao na miji yao na falme zao na zumbe zao
na kolwa zao na kaya zao zilivyoweza kupatikana hata leo.
Kundi la sita
Hili ni kundi
la wazigua waishio Somalia, wazigua wanayo inchi nyingine iliyo nje ya Tanzania
nchi hii huitwa CHAMAMA ambayo iko
Somalia zamani ilijulikana kama Zigua la Kismayu jimbo hilo limepewa hadhi ya
kuwa wilaya huko Somalia katika mkoa uitwao JUBADDAHOOSE au lower Juba au Juba
ya chini mkoa huu unapakana na nchi ya Kenya, mkoa huo una wilaya nne Kismayu,
Badada, chamama na Afamadow Jina Chamama ni jina la kizigua cha kale zaidi
wakimaanisha majani yafananayo na mpunga kwani wazigua walikuta majani mengi
ambayo huota ndani ya maji ambayo kwa kizigua huitwa Nchacha na aina hii ya
majani huonekana katika inchi zote za waseuta, wazigua waliokwea Somalia miaka
kati ya 550-600 iliyopita na kushindikana kurudi nyumbani wakasema hapa tumefika
wakaya Bwila au Bwira na hivyo wao waliitwa Wagosha wa Juba kwani mto Juba
hupita Karibu na Chamama huko Somalia, Hata jina la wilaya nyingine Kismayu
lina asili ya Kizigua SIMADYAKULANGA yaani kisima cha juu na kwa Kiswahili
ndiyo Kisimayu au kisima cha juu na huu ndio mji wa mkoa wa Juba.
Wazigua katika inchi ya Unyanyembe
Kwa mujibu wa Chifu Abdala
Fundikira Marehemu uchifu wa unyanyembe ulikuwa ni uchifu wa wazigua, sababu
kuu ya kundi la wazigua kwenda kutawala unyanyembe ilikuwa ni kujifunza na
kuonyesha uhodari katika maswala ya uganga na uchawi, Inaelezwa kuwa Wanyamwezi
walikuwa wakijivunia sana Uganga na wazigua walikuwa ni waganga Hodari wakati
Fulani katika inchi ya Uzigua walishindana katika maswala ya uganga na
ikasemekana kuwa wale watakaoshinda watawatawala wenzao, Wazigua waliwashinda
wanyamwezi na hivyo kundi la Mshujaa na wake zao na watoto waliamua kusafiri
kwa njia ya bonde la Ufa wakapita Dodoma, Kondoa na kufika Itigi, Hapo
waligwanyika katika makundi makuu manne moja lilipotelea kondoa, kundi la waganga hodari liliendelea Hata
kufika unyanyembe na kushinda katika maswala ya Uganga na hivyo wanyamwezi waliwatawaza
kuwa watawala Machifu hao wa Unyamwezini
wote walitoka katika ukoo huu wa wazigua na kuitawala inchi ya Unyanyembe
machifu hao ni I pamoja na Chifu Kitwanga, Mputa, mpopo, Kabundi, nsoso,
Mmanywa, Mgalula, swetu, Fundikira 1, Mwasele, kiyungi, Isike (Isike alikuwa
mwana wa kiyungi alikuwa maarufu zaidi wakati wa utawala wa wajerumani kwa vile
alipambana nao na wakamshindwakatikamwaka 1889 alipata utawala kwa kuwaua
nduguze wa tumbo la Fundikira ili yeye atawale hawa wote walitoka zigua kwa asili),
Nyaso, Kalunde 1, Said Fundikira, Kiyungi2, Mkasiwa, Fundikira 2, Na Abdala
said Fundikira. Ni kwa sababu hiyo wazigua na Wanyamwezi ni Watani wa jadi na
husaidiana katika Misiba na kujua kwanini msiba umetokea hii ni kwa sababu ya
uhusiano wa Karibu wa wanyamwezi na Wazigua wote,tangu wakati huo wanyamwezi na
wasukuma wakawa watumwa wa Mazigulas.
TAARIFA SAHII KUHUSU MBEGHA (MBEGA)
Ni mtemi wa waseuta waitwao
wakilindi Habari zisizo za uhakika zilikuwa zinaonyesha kuwa Mbega alitokana na
ukoo wa Waarabu yaani baba yake alikuwa Mwarabu kutoka ukoo wa El-Kindi Mwaka
wa 1938 iliwahi kuonyeshwa sinema ambayo ilionyesha kuwa Mbega alikuwa Mwarabu
pamoja na Baba yake sinema hii iliwaudhi sana watu kwani ilkuwa sio sahii,
sinema hii ilionyesha pia kuwa Mbega alikuwa kigego na kuwa alikimbilia vuga
kwa sababu aliua mtu Haya hayakuwa maswala ya kweli.
Mbega alizaliwa katika kijiji cha
Kigurunde jirani na mlima kilindi na Baba yake aliitwa Mliga Bin Mgweno na jina
la Kaka yake Mbega aliitwa Mauya (muya) na dada yake aliitwa Nenkondo Mboza na
Mama yake aliitwa Mzigwa bint Kimweri, mjomba wa Mbega aliitwa Shebuge majina
yao yote haya ni ya kinguu, kwahiyo Mliga alipooana na Mzigwa walizaa watoto
hao watatu yaani Mauya(Muya), Mbega na Nenkondo ni wazi kuwa Baba yake Mbega
alikuwa na Rangi ya asili ya Inchi tuliyotokea Rangi ya Esau hivyo alikuwa
mwekundu kama waarabu na Mbega pia alikuwa mwekundu hii ndio rangi inayofikiriwa
kuwa ni ya kiarabu, Lakini kwanini tunakanusha kuwa Mbega hakuwa mwarabu sababu
ni kuwa mbega alikuwa mwindaji Hodari sana alikuwa akiwinda wanyama wengi sana na
hata nguruwe aliwaua na kuwala hili lingekuwa jambo la kustaajabisha na kuudhi
dini a Baba yake kama angekuwa mwarabu, pia inasimuliwa kuwa wakati mbega
anaishi Waarabu na Wazugu walikuwa hawajafika kilindi.
Kuondoka kwa Mbega huko kilindi
na kukimbilia Sambaani kulitokana na kutoa zawadi ya kipande cha nyama kwa siri
kwa mke wa mjomba wake aliyeitwa Musi alikuwa mzuri na mke kipenzi wa mjomba
wake shebuge, hii haikuwa kawaida kwani kawaida yake ilikuwa kila wakati
anaporudi mawindoni humpa mjomba wake Nyama ambaye yeye humpa mkewe, Musi
aliificha nyama hiyo lakini shebuge aliiona na aliuliza kwanini Mbega amefanya
hayo hali ilikuwa mbaya na mwanamke alipiga kelele kuwa Mbega anataka nife! Nyama
hiyo ilikuwa ya mbaa na ilihesabika kuwa imeharimishwa kwa wakilindi, Mbega
aliposikia hayo alidhani kuwa atauawa na
aliposikia vishindo vya miguu ya mjomba wake alikimbia na siku ya kwanza
alilala katika pango la jiwe katika mlima Ngareni wakati huu alikuwa amemchukua nduguye
Nenkondo siku ya pili walikwenda kujificha
katika msitu mmoja uitwao Komwejimbu kisha walikwenda kulala Maurwi na
kukaa kwa siku kadhaa kisha wakaendelea Ntalawanda Karibu na makuyuni hapo
walikaa Muda mrefu na kujulikana na watu huku akiendelea kuwinda.
Mjomba wake Shebughe alipopata habari alituma watu na shekulwavu
mtoto wa mama yake mkubwa ili kumrudisha
lakini mbega alikataa na alikataa hata kumuachia Nenkondo akihisi kuwa
mjomba wake atatuma watu wengi zaidi kumkamata aliamua kuvuka mto na kuelekea
milima ya Usambara huko Vuluni na baadaye alipanda juu zaidi, alijulikana kwa
akili zake nyingi na Busara za kuamua watu pia alikuwa Hodari sana na ndipo
wasambaa walimfanya kuwa mtawala wao na makao yake makuu yakawa Vuga ambao
ulikuwa mji mkuu wa wasambaa, Uzuri wake aliokuwa nao na rangi ya asili ndivyo
vilimfanya aitwe Mbega, anakumbukwa kwa kuvuka mto ruvu katika eneo ambalo watu
waliotaka kumfuatilia walishindwa kuvuka na wengine kufa maji na pia
anakumbukwa kwa ugunduzi wa Dawa ya Nguvu za kiume iitwayo MBOMBO ambayo
inapatikana kwa wingi Mombo, Mombo ni jina lililotokana na mti wa Mmbombo
wazungu walishindwa kutamka mbombo na wakatamka Mombo na ndio pakaitwa hivyo
hata leo Dawa hii hupatikana Mombo sokoni hata leo inasemekana kuwa Mgunduzi wa
dawa hiyo ni Mbega. Kutokana na damu hii ya Mbega baadhi ya watu hufikiri kuwa
kuna damu ya wajerumani dhana hiyo sio kweli.Wasambaa walimuita mtawala wao
“Simba mwene” yaani mfalme samba kutokana na uhodari wake na uwezo wake wa kuwinda
nguruwe pori, Mbegha alipofariki utawala ulishikwa na mwanae Bugheambaye naye
alilirithiwa na Kinyashe ambaye ndiye baba wa Zumbe Kimweri, wakati wa Kinyashe
aliimarisha utawala wake na kuwa na nguvu zigua nzima mpaka maeneo ya pangani,
alikuwa na nguvu kisiasa na majeshi na pia alikuwa na watumwa na wachungaji wa
ngombe na mifugo aliwashinda wazigua na kutawala maeneo yote yam to Pangani na
milima ya Usambara, baada ya kupanuka kwa biashara Afrika Mashariki mnamo karne
ya 19 inchi ilitawaliwa na Waarabu wa Oman ambapo Sultani alikuwa na makao
makuu huko Zanzibar milima ya usambara na safu za milima ya Kilimanjaro
zilifanyika kuwa moja ya maeneo ya msafara wa watumwa ambao walichukuliwa
kutokea mlango wa bandari ya Pangani, hata wakati wa utawala wa Kimwei ye
nyumbai miaka ya 1835 utawala wa zumbe ulipata nguvu zaidi na watu wake
walijihusisha na kuuza watumwa, zumbe huyu alikuwa na wake 300 akitawala kutoka
Vuga mji wake ukizungukwa na vijiji vingi vya wanawe na wakeze huku akiwa na
watoto wenye nguvu na uwezo alikuwa na utawala wa amani, alikuwa na watu
mashujaa walioweza kukusanya kodi kutoka kwa viongozi mbalimbali, alisifiwa
kuwa ni kiongozi hodari na mmishionary Krapf kimweri alifariki mapema miaka ya
1862 baada ya kifo chake kulitokea mapigano kadhaa kwa ajili ya madaraka na
hatimaye mwanaye Kimweri Mputa Magogo alitawala huyu ndiye alikuwa Mtawala wa
mwisho “sambamwene” ambaye alifariki miaka ya karibuni (2000).
Pichani ni Sultan Sayyid
Said alifanya biashara na wazigua na wasambaa wakati wa utawala wa Zumbe
Kimweri, yeye alitawala Zanzibar na Pemba pia ukanda wa Pwani ndani ya bara kwa
upana wa Km 45 na hivyo Muheza ilikuwa chini ya utawala wa sultani na ndio
maana baadhi ya wazigua na wasambaa wa pwani walisalimiana “Mwinyi” na
kuitikiana “mwinyi” n Saidi neon hilo mwinyi ni la kiutawala kama lilivyo neon
Zumbe likiwa na maana ya ubwana au ukuu au mtawala, linaweza kutumiwa pia kwa
watu wanaoheshimiana “eee zumbe ee tatee” n.k
Ramani ya Taifa la
Tanzania na mipaka yake na mkoa wa Tanga
HISTORIA YA MKOA WA TANGA.
Tukiacha masimulizi ya namna makabila haya
muhimu ya mkoa wa Tanga yalivyoanza na chimbuko lake sasa ni vema tukauangalia
mkoa wa Tanga wenyewe na wilaya zake ambao ndio nchi ya Wazigua yaani wanguu,
wakilindi, wazigua, wabondei na waluvu, Moa huu una Maswala kadhaa muhimu
yafuatayo
Eneo la mkoa
Mkoa una eneo la 27,348 km² na uko Kaskazini Mashariki
mwa Tanzania ukipakana na Kenya upande wa Kaskazini, Bahari Hindi upande wa
mashariki na mikoa ya Morogoro, Manyara na Kilimanjaro. Mpaka upande wa kusini
unafuata mto wa Mligaji.
Kuna wilaya 8 ambazo ni Lushoto,
Korogwe, Muheza, Mkinga, Handeni, Kilindi, Pangani na Tanga Mjini. Eneo
linalofaa kwa kilimo ni 17,000 km².
Tanga ni kati ya mikoa midogo ya Tanzania ikiwa na msongamano mkubwa wa wakazi
ndani ya eneo lake.
Wilaya za Mkoa wa
Tanga
Ramani Wilaya au manisipaa Wakazi (2002) Tarafa Kata Kijiji Eneo km²
Wilaya ya
Handeni 393,931 13 23 102 13,209
Wilaya ya
Korogwe 261,004 4 20 132 3,756
Wilaya ya
Lushoto 419,970 8 32 137 3,500
Wilaya ya Muheza 279,423 6 27 140 4,922
Wilaya ya
Pangani 44,107 4 13 23 1,425
Tanga mjini 243,580 4 21 23 536
Jumla
1,642,015 37 136 557 27,348
Wilaya ya Handeni imegawanywa kuwa wilaya mbili za Handeni
na Kilindi; Muheza iligawiwa kuwa wilaya mbili za Muheza na Mkinga
Ramani ya Mkoa wa Tanga.
Ramani ya Mkoa wa Tanga kama
inavyoonekana hapo juu Pamoja na wilaya zake isipokuwa Mkinga ambayo iko pamoja
na Muheza ilikuwa bado haijaonyeshwa mipaka yake katika Ramani
ASILIYA JINA TANGA.
Kwa kuwa tunawazungumazia Waseuta
na wabondei katika kitabu hiki ni muhimu pia tukaangalia asili ya mjiwa Tanga,
kwa ujumla kama nilivyogusia mwanzoni kuwa wabondei ndio lilikuwa kabila
lililokuwa limepania kurudi pwani au vumba
na hatimaye kufika katika mji waliouita mba Mpya yaani ngomeni, baada ya
kukutana na vikwazo kadhaa hata hivyo walifanikiwa kufika Pwani katika mji
uitwao Amboni, Kwa msingi huo Basi chanzo cha Jina Tanga kilitokana na mbondei
mmoja aliyeitwa Semwiimi Gwando ambaye
aalitokea katika ukoo wa wabondei waitwao wankumbi huyo alitokea sehemu za
nkumbi na Mgambo upande wa Amboni ambapo palikuwa na mkwaju ambao ulikuwa na
umbo la mtu mwenye maziwa
Semwiimi Gwando alikuwa na shamba
lake na kwa kibondei shamba maana yake ni Tanga ilitokea kila alipokuwa akienda
shambani kwake watu wakimuuliza Waita hahi? Yaani unakwenda wapi alijibu naita
Tanga akimaanisha shamba, Baada ya miaka mingi walikuja wageni ambao walimuoma
sehemu ya shamba lake ili wapate kulima akawapa mahali paitwapo He-Mkwakwa,
hiii ndio asili ya Mkwakwani, Semwiimi Gwando aliyehamia Tanga na familia yake
na kukawa maskani yake hii ndio Tanga, baadaye watu wengine kutoka ambaoni
walihamia na kukaa katika maeneo kama Kisosora, chumbageni na mafuriko. Jina
Tanga likawa ndio jina la mji wa Tanga na makao makuu ya mkoa wa Tanga.
Inasemekana Hata asili ya Jina
Tanganyika ambalo lilibeba asili ya Taifa hili kabla ya muungano lilitokana na
na asili ya jina Tanga na wajerumani walipofika Tanga sehemu za ndani zaidi
ziliitwa nyika na ndipo waliposema huko ni Tanganyika
ASILI YA JINA MUHEZA.
Makabila mapya kutoka Kenya
yalikuja pwani ya Tanga makabila hayo ni ya Wadaiso, Wasegeju na wadigo kwa
ujumla hili ni kama kabila Moja na kwa asili walitokea Kenya lugha
wanayoizungumza yaani kidigo kwa asili ni kidaiso walionekna mara ya kwanza
wakivuka mto Umba na kuja Tanzania wakitokea Kenya mtu wa kwanza kuwaona
aliwaona wamekunja nguo zao juu ya magoti na huenda waliitwa jina hilo na
wabondei kwani kukunja nguo juu au kupandisha nguo juu kwa kibondei ni Kusega
kwa hivyo walikuwa wamesega nguo zao juu hivyo waliitwa wasegea juu na jina hilo ndilo lilikuja kuzaa jina
wasegeju nchi zao ndio Daluni, Bwiti huko Maramba jina wadaiso lilikuwa jina la
asili la huko walikotoka lakini hata hivyo wengi leo huongea Kiswahili na
kidio jina digo lilitokana na Baba yao
aliyeitwa DIBWA au Digo na walilipa
kabila jina la wadigo kutokana na heshima yake kwa msingi huo wadaiso,wasegeju
na wadigo ni kabila moja.
Hawa walipokuja kutoka Kenya
walianza kugombea Inchi na wabondei na kuanza kuwasukuma na mwanzoni
walionekana kufanikiwa kuwasukuma nyuma wabondei ndipo wenzao walioishi kwa
wingi huko Mkuzi , ngomeni na Magila na sehemu nyingine walisimama kiume na
kuwapiga vibaya katika eneo la Mkanyageni, Huko ndiko kulikokuwa na Ngome ya
wabondei wakiwaambia wadigo kuwa Hapa Mmekwisha au mmefika Hanu Mheza na jina hilo ndilo likawa maarufu
kwaajili ya inchi yote ya Bonde ambayo wabondei waliipigania kwani ni inchi
nzuri yenye Rutuba ambayo hawakutaka wadigo waichukue inci hii ndio yenye neema
kubwa ya matunda, minazi, maembe,machngwa matamu sana Mafenesi na wazungu
walipokuja waliipenda nchi hii na kuchukua masahamba mengi na kuyafanya ya
mkonge au Katani
NEEMA KATIKA KABILA LA WABONDEI.
Moja ya makabila ya waseuta
yaliyopata neema kubwa tofauti ni Kabila la wabondei, baada ya wageni kupata
kibali kwa Zumbe Kimweri huko Vuga walianzisha misheni huko Hemvumo Magila na
kujenga shule na Hospitali. UMCA ilikuwa imehama kutoka Zanzibar kwenda Magila
katika Jimbo la Tanga mwaka 1875, jambo hili lilichangia sana kuleta elimu kwa
watu wa Tanga hususani kabila hili la wabondei, kumbuka kuwa Waarabu
walitangulia miaka mingi na kueneza uislamu kwa kabila kadhaa za mkoa wa Tanga,
kwa kuhofia ugumu wa wadigo ambao waling’ang’ania sana dini ya kiislamu na kwa
heshimaya sultani wa Zanzibar wazungu waliingia ndani na kuanzisha misheni zao,
Ukristo ulianzishwa na kustawi katika nchi ya Wabondei, na vivyo hivyo nafasi
za elimu kwa watoto wa Wabondei. Katika lile wimbi la kuwania nafasi za elimu,
watoto wengi wa Kiislamu walibatizwa. Ni jambo la kawaida miongoni mwa Wabondei
kukuta majina kama Peter Saidi au John Ramadhani, Samuel Jumaa, Andrew jumaa
n.k. Wabondei wengi walikwenda Makerere College na Minaki teaching College n.k.
Siasa za kizalendo zilipoanza baada ya Vita Kuu ya Pili, Wabondei walikuwa
wamejaa katika utumishi wa serikali ya kikoloni. Gurudumu la historia ya
Tanganyika likizungushwa na baadhi ya Wabondei, maarufu miongoni mwao wakiwa
watu kama Martin Kayamba aliyejikomba sana kwa wakoloni, George Magembe mtu
ambae huku alikuwa hayuko wala kule hayuko, hujui kama yupo na wazalendo au na
wakoloni, Stephen Mhando; mzalendo mwenye msimamo mkali na na mdogo wake Peter.
Wabondei walikuwa ndiyo walimu,
makarani, wakalimani mahakamani na maofisa wa ustawi wa jamii katika serikali
ya kikoloni maafisa elimu n.k. Hili lilikuwa tabaka maalum la Waafrika,
waliosomeshwa na wamishonari kuitumikia serikali ya kikoloni na katika kufanya
hivyo kulitumikia Kanisa na Ukristo, uhusiano ambao ulikuwa wenye manufaa kwa
pande zote mbili zilizokuwa zikishirikiana.Wazungu walifaidika kwa kuwapata
wabondei nao walifaidika kwa kupata elimu nzuri na maisha mazuri ukilinganisha
na waseuta wengine.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni